Banana kama baba yake (2)

Katika kuangalia safari ya kimuziki ya Banana Zorro, wiki iliyopita tuliona jinsi alivyoamua kuachana na bendi ya kwanza na kujiunga na Inafrica Band, na moja kwa moja kujikita katika kufanya kazi kama mwanamuziki anayejitegemea, yaani solo artist. Akiwa mwanamuziki anayejitegemea, Banana alifanikiwa kuingiza sokoni albamu yake ya pili iliyojulikana kama ‘Subra’ ikiwa na vibao kadhaa kama vile ‘Mapenzi Gani’, ‘Mama Kumbena’ na ‘Niko Radhi’ ambazo hadi leo bado zinafanya vizuri katika ulimwengu wa muziki ndani na nje ya Tanzania.

Nyimbo hizo zilimwezesha Banana kushinda tuzo kadhaa za Kilimanjaro Music Awards mwaka 2007. Alishinda katika kipengele cha Mwimbaji Bora wa Kiume pamoja na Wimbo Bora wa R&B (Niko Radhi).

Aanzisha bendi yake

Mahesabu yake ya kuachia nyimbo kwa mpangilio maalumu ndiyo yalimpa mafanikio kuweza kufikia malengo ya kuanzisha bendi yake iliyojulikana kama Banana Band au B. Band.

Mwaka 2008, mkali huyo aliyetikisa na wimbo ‘Nzela’ alimuoa Suzan. Mpaka sasa wawili hao wamejaliwa kupata watoto wawili, Landi na Jarmaine.

Mafanikio

“Kiasi chake, kila siku ninapambana kusogea mbele zaidi, kikubwa kwa sasa najivunia kuwa na bendi ambayo ina wafanyakazi 14, baadhi yao wanasomea muziki kutokana na kipato wanachokipata B. Band,” Banana alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema pale alipotakiwa kuelezea mafanikio aliyoyapata kupitia muziki.

Mkongwe huyo alianza muziki zaidi ya miaka 10 iliyopita, huku akiwa chini ya baba yake, Zahiri Ally Zorro. Familia yao ilikuwa ikijulikana kama yenye vipaji vya muziki.

Banana Zoro ametoa ufafanuzi juu ya kuwa kwake kimya. Anasema kuwa mashabiki hawapaswi kukariri maisha ya wasanii kwa kuwa wengi wamezoea kuonyesha maisha yao katika mitandao.

Kwa upande wake hajazoea kufanya maonyesho katika vyombo vya habari kuhusu maisha yake, lakini yuko vizuri sana na si kama ‘amefulia’ kama wanavyodai baadhi ya wapenzi wa muziki wake.

“Mafanikio ni wewe na dreams (ndoto) zako. Wakati unakua ulitaka kuwa na nini? Hauwezi kusema sijafanikiwa wakati haunijui kiundani, na mimi siwezi ku-display (kuonyesha) kila kitu changu katika mitandao, lakini I am good, I have my wife, my kids, my band (niko vizuri, nina mke, watoto na bendi),” anatamka Banana Zorro.

Anaongeza: “Mimi ndiye msanii wa kwanza kuwa na bendi yangu mwenyewe Tanzania na inafanya vizuri. Pia nimeajiri watu katika bendi yangu zaidi ya 20, ninafikiri hayo ni mafanikio makubwa sana.”

Hata hivyo, Banana Zorro anasema kuwa ni kweli kuna baadhi ya wasanii wakubwa walikuwa wanafanya kazi vizuri kabisa lakini ukiangalia maisha yao kwa sasa yanatia aibu kabisa.

Anasema wapo baadhi ya wanamuziki waliowahi kuwa na majina makubwa katika tasnia lakini hivi sasa hawajiwezi kabisa lakini kwa upande wake ni tofauti kwa sababu ana usafiri wake na ana nyumba yake na anaendesha maisha vizuri kabisa bila kumtegemea mtu.

Anasema jambo analolitafuta hivi sasa ni kupigana ili muziki wake utambulike kimataifa.

“Mimi nimenunua gari nikiwa na umri wa miaka 18. Mpaka sasa nina miaka 36 na hata hivyo siwezi kusema nina gari gani kwa sasa kwa sababu at the end of the day (mwisho wa siku) gari langu ni gari langu, sikimbizani na daladala tena ingawa kuna wasanii mpaka leo walikuwa wakubwa lakini bado wapo huko na wana hali mbaya. Sisemi kuwa kupanda daladala ni vibaya,” anabainisha.

Katika mipango yake Banana Zoro alipanga pia kuanzisha shindano lenye lengo la kupata wasanii wenye vipaji katika uimbaji, upigaji wa gitaa, kinanda na upulizaji wa tarumbeta. Banana anasema kuwa lengo la kuandaa tamasha hilo ni kuibua na kuendeleza vijana wenye vipaji hususan wanaotumia mtindo wa Rhumba lakini hawajui namna ya kutimiza malengo yao katika muziki.

“Nafasi ndiyo hiyo, vijana wenye ndoto za kuwa kama mimi wajitokeze kwa wingi ili waweze kutimiza lengo lao kupitia vipaji vyao,” anasema Banana.

Akizungumzia mipango yake ya muziki, Banana ambaye pia ni mmiliki wa B Band, anatarajia kuachia albamu yake mpya aliyowashirikisha wasanii mbalimbali akiwemo Young D na Young Killer.

Anazitaja baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo kuwa ni ‘Bado Kidogo’, ‘Samehe’, ‘Sahau’ aliomshirikisha Young Killer na ‘When She is Higher’ aliomshirikisha Young D.

Makala hii imeandaliwa kupitia vyanzo mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa simu namba: 0784331200,0767331200, 0736331200 na 0713331200.