Kikundi chajipanga kuhujumu mabilioni kupitia mikataba, zabuni zageuzwa kichaka cha rushwa

DG Eric, Mwenyekiti wa Zabuni wazima mchongo wa Sh bil. 6.34, cha juu kimeongezwa makao makuu

Rais Samia afyatua waliozembea, uchunguzi mkali waanza kubaini wachotaji

Ujenzi wa meli kichaka cha rushwa ya karne, madudu yaliyopita yaanza kuanikwa

NA MWANDISHI WETU

DAR ES SALAAM

Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa amecharuka kuhusu ufisadi unaosababishwa na udhaifu wa bodi katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), mambo mapya yameendelea kuibuliwa.

Bodi ya Zabuni ya Bandari hivi karibuni ilitegeshea wakati Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi na Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni ya TPA, Freddy Liundi, wakiwa ziarani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ikatoa zabuni ya ajabu ya kukarabati tag ya kuvuta meli kwa mabilioni ya pesa.

Uchunguzi wa JAMHURI unaothibitishwa na nyaraka mbalimbali umebaini kuwa tag inayoitwa Amikonish ilitakiwa kukarabatiwa. Miaka yote huwa tag zinakarabatiwa Mombasa nchini Kenya kwa gharama ya Sh bilioni 1.3. Tanzania imeamua kujenga chelezo ili zikarabatiwe hapa hapa nchini kupunguza gharama.

Bodi ya Zabuni ya TPA ilitegeshea viongozi hao hawapo ikaipa zabuni ya kukarabati tag hiyo jijini Dar es Salaam kwa bei ya ‘kutisha’.

Kampuni kutoka Kenya (jina tunahifadhiwa) ilikuwa ‘imeshinda zabuni’ ya kukarabati tag hapa nchini kwa Sh bilioni 6.34. Hapa ijulikane kuwa tag hii inatengenezwa Dar es Salaam, na si Mombasa. Ikitengenezewa Mombasa ilikuwa inagharimu Sh bilioni 1.3. Zabuni hii iliongeza Sh bilioni 5 juu ya gharama ya kawaida.

Liundi alipopelekewa kiasi hicho akamshauri DG Eric wakikatae kwa sababu ni kikubwa mno. 

“Kampuni hiyo hiyo ikashusha bei ya kuikarabati hiyo tag hadi Sh bil. 1.98. JAMHURI limeambiwa kuwa uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam uliomba Sh bilioni 1.1 kwa ajili ya kukarabati tag hiyo, ila ilipofika makao makuu, ikaongezwa Sh bilioni 5.23 kama ‘cha juu’. Tag mpya inauzwa Sh bil. 8.

“Kiasi cha Sh bilioni 1.98, nado nacho kilikuwa ni kikubwa, kwani kwa sasa tag inatengenezewa Dar es Salaam ambako kwa uhalisia inapaswa kutengenezwa kwa Sh milioni 600 tu.

Kundi la waliozuiwa kuchota hizi fedha, liliishaanzisha mpango wa kumchimba Eric na Liundi na kuwatisha ili wapate hizo fedha haraka kwa gharama isiyo na uhalisia.

Hata hivyo, katika mkutano wa Jumatatu wiki iliyopita wenye masilahi walishinikizwa kujadili zabuni hiyo tena ili ipitishwe, Liundi akawagomea na mpango huu ukafa.

Baada ya Rais Samia kukemea mpango huo wa wizi, JAMHURI linafahamu kuwa muda mfupi alipoondoka Bandarini, wakurugenzi walikutana na kuhoji nani amempelekea Rais taarifa za kukarabati tag kwa bei ya kutisha wakidai kati yao kuna anayewasaliti kwani hawakutarajia taarifa hizo zifike huko.

Mkurugenzi Mkuu Eric aliamua wafanyie kazi hoja na si kutafuta nani aliyetoa siri. JAMHURI limethibitishiwa kuwa uchunguzi umeanza kwa kutumia vyombo vya dola kubaini nani aliyeongeza bei ya ukarabati wa tag kutoka Sh bilioni 1.1 iliyopendekezwa awali hadi Sh bilioni 6.34.

Timu ya uchunguzi itapitia mikataba mbalimbali ambayo inatajwa kuwa mchezo wa kuweka “cha juu” umeshamiri ambapo Mkurugenzi Mkuu Eric amejipanga kukata mrija huo

Mwangwi wa Rais Samia Bandari

Rais Samia amegeuka ‘mbogo’ baada ya kushitukia upigaji mkubwa wa fedha za serikali kupitia zabuni ya ujenzi wa meli tano.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa gati namba ziro hadi namba saba katika Bandari ya Dar es Salaam, Rais amesema katika mkataba wa ujenzi wa meli hizo kumebainika kuna ‘madudu’. 

“Mtakumbuka kwamba Juni 15, mwaka huu, nikiwa ziarani Mwanza nilishuhudia kutiwa saini kwa mikataba ya ujenzi wa meli tano za Kampuni ya Kuhudumia Meli Tanzania (MSCL) na mkandarasi anayeitwa Yucel Tekin Shipbuilding ya nchini Uturuki.

“Katika kufuatilia utekelezaji wa ujenzi wa meli hizo mambo kadhaa yamejitokeza, la kwanza tuliona kwamba ndani ya mkataba ule mkandarasi ana wakala yupo Tanzania ambaye wakala yule anatakiwa kulipwa Dola milioni mbili za Marekani kwa kila meli tutakayojenga.

“Meli ya chini ilikuwa na dola milioni 1.9 za Marekani pamoja na malipo madogo yanayoenda kwa wakala aliyepo Tanzania. Nikaomba mkataba wa wakala nikaupata, kazi za wakala ni kufuatilia tenda zitakazotoka Tanzania, kuomba tenda na kujua nyaraka za tenda, lakini wakala analipwa kwa kila meli itakayotengenezwa Tanzania?

“Nikachukua hatua za kuagiza vyombo wamtafute wakala na waongee naye, walifanya kazi yao lakini na mimi nikamuita huyu mkandarasi aliyeshinda hii tenda akaomba radhi kuachana na wakala,” amesema Rais Samia.

Pia anasema lililojitokeza katika matayarisho ya kumfuatilia mkandarasi wa kujenga meli hizo yalikuwa yanatia wasiwasi na hakuonekana kwamba yuko tayari kujenga meli hizo.

Kutokana na wasiwasi uliopatikana, anasema serikali iliunda timu ya wataalamu kutoka sekta mbalimbali.

Samia anasema waliunda timu kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, mjumbe mmoja kutoka ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na mjumbe mwingine kutoka MSCL, mjumbe mwingine kutoka jeshini kitengo cha wanamaji na ilitakiwa iende Uturuki kufuatilia hadhi au hali ya huyo mkandarasi aliyeshinda hiyo zabuni ya ujenzi wa meli.

Anasema yaliyojitokeza ni kwamba katika kumtafuta huyo mkandarasi imegundulika Kampuni ya Yucel haina eneo lake la ujenzi wa meli (ship yard).

Badala yake imekuwa ikipata zabuni na wao ni madalali wanachukua zabuni wanatafuta kampuni nyingine kisha wanawapa kazi huku wao wakibaki kuwa madalali.

Rais Samia anasema mbali na maelezo kuwa kampuni hiyo ina fedha zinazotosheleza, ilibainika kuwa uwezo wake kifedha ni mdogo mno kwa sababu hadi timu inaondoka Uturuki walishindwa kutoa taarifa ya fedha walizonazo.

Rais amesema wasifu wa kampuni na uwezo wake katika ujenzi ni wa shaka kwa sababu haipo hata katika orodha ya wajenzi wa meli inayotolewa na Umoja wa Wajenzi wa Meli Uturuki.

“Na hiyo ndiyo iliyotuthibitishia kwamba hawa ni madalali, lakini pia haikuwa na wafanyakazi wenye sifa za ujenzi wa meli na wala haina mitambo ya kujenga meli na hadi sasa kampuni hiyo haijafanya lolote katika kazi hiyo ambayo tulisaini nao mwezi Juni mwaka huu.

“Eneo walilolitumia ni kampuni nyingine kabisa inaitwa Hicri Ercil Tersanecili Shipyard ambayo hata yenyewe ilipokaguliwa ilibainika ina uwezo wa kufanya matengenezo ya meli na kutengeneza boti ndogo ndogo.

“Lakini tujiulize tenda hii ilipotoka ilitolewa na bodi ya zabuni ya wizara husika au shirika husika, shirika lile lina bodi ya wakurugenzi ambao wamepitisha tenda hii.”

Pia anasema ana taarifa kwamba hata huyo mkandarasi alifanyiwa uchunguzi wa kina (due diligence) uliosema yuko vizuri (positive), lakini timu hiyo ilipokwenda hayo ndiyo yaliyobainika.

“Sasa haya tumeyabaini hivi karibuni, huko nyuma yametokea mangapi, waziri hili nalo ni mzigo wako naomba tena bodi iliyohusika, bodi ya wakurugenzi iulize tena kama hawa watu, hivi vikundi viwili bado vinafaa kukaa kwenye hili shirika kama miradi iliyokuwa ikipitishwa ni ya aina hii.

“Nimemwambia waziri achukue hatua ya kusimamisha hiyo tenda akishirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kunusuru fedha zetu zisiliwe na wajanja wachache,” amesema.

Rais Samia anasema anasema kinachosikitisha ni kwamba Mtanzania wa ndani anashirikiana na ‘wajanja’ wa nje kuchepusha fedha zote ambazo zingeenda kutekeleza maendeleo ya wananchi.

“Tuna uhaba wa madarasa, vituo vya afya, napita nikikopa, tunahangaika, tuna uhaba wa pembejeo za kilimo, tunatafuta fedha, lakini huku kuna wenye raha zao wamekalia fedha, wanapitisha miradi wanavyotaka na wanazitumia wanavyotaka.

“Bodi ipo, hizo sijui tender committee zipo, mambo ni kama hayo. Naomba waziri fanya marekebisho unavyoweza kwenye wizara yako. 

“Kama huwezi njoo tukae kitako, mimi, wewe na Katibu Mkuu Kiongozi tuone jinsi ya kufanya marekebisho katika wizara hii ili mambo yaendelee. Lakini fedha hii inatumika hivyo.

“Hapo hapo kukiwa na wafanyakazi tele wa ngazi za chini ambao maslahi yao na stahiki zao pengine hawapati kwa wakati au yako chini. Watu wale fedha hii wangepewa wangepata motisha ya kufanya kazi zaidi kuliko kuwavuta ninavyowavuta sasa, kazi ni kubwa malipo ni machache.

“Waziri nilikuweka kwa kukuamini naomba nenda kasimamie kazi hii kama ninavyotarajia. Na utakaposhindwa njoo uniambie dada nimeshindwa, nitaangalia mwingine labda ataweza kunisaidia. Lakini haya hayawezi kuendelea,” amesema.

Katika hatua nyingine, anasema kuna makundi ya watu wanajua wanayoyafanya ndani ya serikali, lakini yanageuka na kusema ufisadi umerudi katika Serikali ya Awamu ya Sita au mambo yako hovyo kumbe wao ndio wako hovyo.

Amesema mambo yale hayakufanyika ndani ya serikali yake, bali yalifanyika huko nyuma ila ‘gari bovu’ linaangushiwa awamu ya sita.

“Sitakubali. Nimeapa kusimamia haki za wananchi, nitasimama nao, nitasimama na kutetea haki za wananchi, sitakubali,” amesema.

Akaipongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kazi zinazoendelea, lakini akailaumu kwa yalitokea na wakashindwa kuchukua hatua.

Avunja bodi TPA, MSCL

Katika hatua nyingine, Rais Samia amevunja Bodi ya TPA na ile ya MSCL kwa kuwaondoa wenyeviti wake baada ya kutoridhika na utendaji wao.

“Kwa maana hiyo, uwezo wangu ndani ya wizara ni kuvunja hizo bodi, kumuondoa mwenyekiti. Kwa hiyo wenyeviti wote wawili wa bodi nimewaondoa.

“Waziri utafanya pale palipobakia, tenda na bodi hizo si uwezo wangu ni uwezo wako na watu wako. Nasubiri nione kitakachotokea. Hatuwezi kwenda na mambo haya. Halafu mnachukua lawama mnatupia kusiko husika, haiwezekani,” amesema Rais Samia.

Bodi ya Wakurugenzi wa TPA iliundwa na Mwenyekiti Profesa Ignas Rubaratuka, huku Makamu wake ni Dk. Delphine Magere. Wajumbe ni Malata Pascal, Dk. Jabiri Bakari, Masanja Kadogosa, Jayne Nyimbo, Mhandisi Ephrem Kirenga, na Eric Hamissi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa TPA.

Fedha nyingi za ukarabati 

Samia anasema jambo jingine lililojitokeza huko nyuma ni ukarabati wa tagi zinazovuta na kuongoza meli. 

Anasema ni kweli zina uchakavu na zinatakiwa kukarabatiwa lakini zilivyokuwa zinataka kukarabatiwa kwa Sh bilioni 6.6 kwa tagi moja wakati gharama halisi zikitengenezwa Mombasa nchini Kenya ni Sh bilioni 1.6.

“Sasa angalia tofauti moja ya kutoka shilingi bilioni 1.6 hadi shilingi bilioni 6.6 lakini kama tagi zile zitatengenezwa hapa nyumbani kuna uwezekano wa kutengeneza tagi moja kwa shilingi milioni 700,” anasema na kuongeza:

“Nikuelekeze mkurugenzi wa bandari na waziri, fedha zinazoshughulika kule na huku embu ziangalieni mziweke, muweze kujenga chelezo hapa mtachotengenezea meli zenu wenyewe. 

“Na kama kutakuwa upungufu mtuambie kwa sababu inaelekea sasa matengenezo ya meli na hizi tags kwenda Mombasa ndiyo chanzo cha watu kuvuta fedha jinsi wanavyotaka.”

Jingine anasema ni mradi aliouingilia mapema bandarini wa ujenzi wa matenki ya kuhifadhia mafuta baada ya kumpa wasiwasi kutokana na kutaka kugharimu mamilioni kadhaa ya fedha.

“Nikamwambia mkurugenzi mkuu nimekuleta hapo ulinde interest (maslahi) za taifa, huu mradi unanitia wasiwasi na naomba usimamishe,” anasema na kuongeza:

“Nakushukuru mkurugenzi ulinisikia, ule mradi umesimama na kama unahitajika ule mzunguko wa tenda uanze sasa hivi upya ili tuone sasa  tunajenga.

“Lakini jingine lililonitia wasiwasi ni kwamba serikali ina ubia na Kampuni ya Puma na pale Puma kuna matenki kadhaa ambayo hayajatumika au hayatumiki.

“Sasa kulikuwa na haja gani kwenda kujenga matenki mengine kabla yale yaliyopo ambayo serikali ina ubia 50 kwa 50 kutumia yale yaliyopo.

“Hii ilikuwa ni kichochoro na mradi ambao wajanja walikuwa wapige fedha hapo. Kwa hiyo nashukuru mradi umesimamishwa.

“Na ndiyo maana nimesema tunapokwenda kufanya kazi za bandari, mkurugenzi mkuu, wizara simamieni kazi zifanywe kwa weledi lakini pia kwa uadilifu.

“Najua kuna sehemu ambayo tunaendesha serikali wenyewe kuna sehemu tumekodisha au watu wengine wanaongoza shughuli huko lakini je,  ufanisi wa haya mapato yanayopatikana ni kiasi gani?

Kwa hiyo pamoja na jitihada zetu za kukuza miundombinu lakini naomba mamlaka zinazohusika ziongeze au zione njia nzuri ya kuendesha bandari zetu, zilete ufanisi na ziweze kujenga vizuri uchumi wa nchi yetu.”

Upotevu wa mapato

Kuhusu ukusanyaji wa mapato, Rais Samia amesema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha imetoa mwelekeo kwamba huenda mwisho wa mwaka TPA ikakusanya Sh bilioni 980.

Amesema fedha hizo zinaweza kuonekana ni nyingi, lakini bandari ikifanya kazi inavyopaswa inaweza ikakusanya fedha nyingi zaidi ya hizo.

“Nasema hivyo kwa sababu pamoja na makusanyo hayo kumekuwa na changamoto ya kuwepo kwa mianya mingi ya upotevu wa mapato.

“Mianya hii imetokana na kukataa kwa makusudi kuweka mifumo madhubuti ya ukusanyaji wa mapato na mifumo inayosomana baina ya TPA na TRA.

“Hizi mamlaka mbili hazisomani mifumo yao, kuna utata mwingi hata ndani ya mamlaka yenyewe kuna mifumo kadhaa kila mfumo na mambo yake kiasi kwamba inaruhusu wafanyakazi kuichezea na kudanganya kama nitakavyosema huko mbele,” amesema.

Pia anasema amepata fursa ya kupitia ripoti ya Ukaguzi Maalumu wa Kiuchunguzi wa Kimfumo (ERP) unaotumika ndani ya TPA uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Juni, mwaka jana na kutoka Machi, 2021.

Anasema ndani ya ripoti ile aliona fedha nyingi zilizotumika kuajiri kampuni za kuanzisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato zisizotoa tija iliyokusudiwa.

Kwa mfano, anasema Mamlaka bila ya kuwa na mpango mkakati wa TEHAMA na bila kushirikisha Mamlaka ya Serikali Mtandao iliajiri kampuni kadhaa kuweka mifumo ya ukusanyaji ndani ya bandari.

Anasema kampuni ya Soft Tech Consultant Limited iliajiriwa kwa mkataba wa Sh milioni 694 na kati ya hizo Sh milioni 600 zililipwa kwa kampuni hiyo, lakini haikumaliza kazi iliyotakiwa kufanya.

“Mkataba ukavunjwa na kwa maana hiyo Sh milioni 600 zimekwenda, kama mfumo ulianza kutumiaka au la! Lakini hilo lilitokea kazi haikumalizika.

“Iliajiriwa pia kampuni ya 21th Century System kwa dola milioni 6.6 za Marekani huku dola milioni 4.6 zililipwa na mkataba baadaye ukavunjwa bila kazi kukamilika.

“Ikaajiriwa pia kampuni ya S.A.P East Africa Limited kwa dola 433,000 za Marekani, lakini pia akaajiriwa mshauri mwelekezi, mshauri binafsi kwa dola 31, 920 za Marekani.

“Fedha hizi zote zimeingizwa katika mifumo, lakini tunavyozungumza leo ni kwamba mifumo ile bado haiko vizuri, inachezeleka, wafanyakazi wanaichezea, wanadanganya na mifumo haisomani na haikusanyi fedha kwa ukamilifu wake,” amesema Rais.

Mbali na malipo hayo, anasema ripoti inaeleza kulikuwa na malipo ya juu kwa wakandarasi hao bila kufuata sheria za ununuzi na matumizi.

Anasema ripoti ilieleza kwa kina jinsi kazi hizo zilizofanywa na fedha zilizotumika na watu waliohusika na uzembe huo na kupendekeza hatua za kuchukuliwa, lakini hadi sasa hakuna chochote kilichochukuliwa.

Akawaagiza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Mkurugenzi Mkuu wa TPA na TAKUKURU wakaisome ripoti hiyo na kama hawana atawapa.

“Kaitazameni mwangalie yaliyopendekezwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali halafu mchukue hatua. Na nasubiri kusikia hatua mlizochukua.

“Fedha nyingi zimepotea wakati tunachekeana na tunatazamana tu na bado waliotajwa kwenye ile ripoti wako maofisini ndani ya mamlaka ya bandari sasa hivi.

“Wapo maofisini wanaendeleza ubadhirifu na wizi wa mali ya umma, nataka ripoti ile ifanyiwe kazi na nipate kujua hatua mlizozichukua tena kwa haraka.

“Kama Mamlaka ya Bandari ingechukua hatua za kurekebisha yaliyosemwa, leo hii tarakimu za mapato tunayozungumza zingekuwa vingine, lakini vilevile ingetusaidia kupunguza ubadhirifu wa fedha za shirika.

“Nimesema mifumo hiyo inachezeka, hivi karibuni nina taarifa kwamba wafanyakazi wamechezea mifumo ile hasa wa sehemu za hesabu, kiasi ambacho ukisoma mfumo unaonyesha mizigo inayoshushwa imelipiwa na getini wanasoma mizigo imelipiwa na mageti yanaruhusu mizigo kutoka.

“Ukweli ni kwamba mizigo haijalipiwa, mkurugenzi naomba uwe macho na hayo mambo, vinginevyo! Mamlaka ya usimamizi wa bandari ina bodi ya wakurugenzi iliyoaminiwa kwamba itatoa maelekezo na kusimamia utekelezaji wa shughuli za TPA.

“Haya niliyoyataja yote yanatokea bodi ikiwepo inaangalia, na hakuna hoja wala hatua zinazoulizwa je, mmechukua hatua gani? Tujiulize, kuna nini? TAKUKURU, Mkurugenzi na waziri nataka mnijibu nijue kuna nini kilichojificha kwenye hilo wakati bodi iko hapo.”

By Jamhuri