DAR ES SALAAM

NA CLEMENT MAGEMBE

Wafanyabishara katika soko la Kariakoo wameiomba Serikali kuweka mazingira mazuri yatakayowawezesha kuitumia bandari ya Dar es Salaam kwa ufanisi na kuboresha biashara zao.

Wakihojiwa na JAMHURI wiki iliyopita, wafanyabiashara hao wamesema kuwapo kwa mazingira hayo kutawachochea kuagiza kwa wingi bidhaa kutoka nje ya nchi, hivyo kuchangia ongezeko la pato linalotokana na kodi na ushuru.

Justine Massawe,mmiliki wa duka la nguo lililoko katika mtaa wa Agrey, amesema taratibu za ukusanyaji wa kodi hasa katika uondoaji wa mizigo bandarini, zimechangia kuwakatisha tamaa wafanyabiashara kuitumia bandari hiyo.

Amesema kikwazo kingine ni mbinu inayotumiwa na watumishi wa TRA wasiokuwa waadilifu, kusingizia mtandao wa kompyuta kuwa chini pindi wanapotoa mizigo, lengo likiwa ni kuongeza mapato yanayotokana na (mizigo) kuhifadhiwa kwa siku nyingi.

Massawe amesema tofauti ya kodi inayotozwa kwa mizigo inayofanana kwa aina na ukubwa, ni miongoni mwa mambo yanayowakwaza wafanyabiashara kuitumia bandari ya Dar es Salaam.

 “Nimewahi kuingiza mzigo kutoka nje ya nchi kwa kulipia kodi ya Sh milioni  60 kwa kontena, na nilipoleta mzigo wa aina ile ile na ukubwa wa kontena unaofanana na ule wa mwanzo, nikakadiriwa kodi ya Sh milioni 119, hiyo ni changamoto kubwa kwa wafanyabiashara,” amesema.

Amesema ilimlazimu kukopa fedha benki ili kulipia ongezeko la kodi hiyo na kwamba hadi sasa hajafanikiwa kulipa deni la benki. Hivi sasa, Massawe ameacha kufanya biashara ya kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi.

Mfanyabiashara huyo amesema wingi wa kodi zinazotozwa nchini unasababisha miongoni mwa wafanyabiashara kuhamishia mitaji yao nje ya nchi, huku wengine mitaji yao ikipungua na kubadili biashara

“Wapo wafanyabiashara waliokuwa wanaingiza bidhaa kutoka mabara ya Asia na Ulaya, lakini kwa sasa wananunua bidhaa kutoka Uganda na kuzileta hapa,” amesema.

UNYANYASAJI WATEJA

Massawe amesema mazingira ya biashara ya ndani si rafiki kwa wateja kutokana na unyanyasaji unaofanywa na polisi kwa kigezo cha kukagua nyaraka zinazohusiana na kodi.

Amesema hali hiyo ni tofauti na ilivyo kwa nchi kama Uganda na Kenya ambapo polisi hawana utaratibu wa kuwabughudhi wafanyabiashara au wanunuzi wa bidhaa.

“Suala hili tumeliripoti TRA lakini bado linaendelea hadi sasa na hiyo inachangia wateja wetu kutoka nje ya nchi, kutokuja kwenye hapa Kariakoo,” amesema.

“Hali ni mbaya sana, watu wamepungua sana katika soko hili,miaka michache iliyopita mizigo ilikuwa inajaa katika mitaa yote ya soko lakini kwa sasa mizigo inayoshushwa hapa ni michache sana,” amesema.

 Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Sylvester Kiondo amesema matatizo yanayowakabili wafanyabiashara ikiwamo kodi yanaeleweka, lakini watayashughulikia baada ya kuundwa na kuitambulisha bodi ya jumuiya hiyo.

Johnson Minja ni Mwenyekiti mstaafu wa JWT, amesema uhalisia katika biashara unadhihirisha kushuka, licha ya TRA kutoa takwimu za kupanda kwa mapato ya nchi.

Amesema hata mfumo unaotoa fursa kwa mamlaka kama polisi, madalali,halmashauri za wilaya, miji na majiji, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na nyingine kutoza fedha, unapaswa kurekebishwa ili kupunguza mzigo wa malipo kwa raia.

By Jamhuri