Bomu la mafao

Kuna dalili za kukwama kwa kanuni mpya za ukokotoaji wa mafao ya wastaafu zilizotangazwa na serikali.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo imewatoa hofu wananchi kuhusu kanuni hizo ikisema inazisubiri zipelekwe bungeni hata kama zimekwisha kuanza kutumika.

Kanuni zilizotangazwa hivi karibuni zinamfanya mstaafu kulipwa asilimia 25 ya mafao yake baada ya ukomo wa ajira. Kiasi kinachobaki cha asilimia 75 kitalipwa kidogo kidogo kama mshahara kwa miaka 12.

Ikitokea mstaafu amefariki dunia, familia yake itaambulia malipo ya miezi 36 pekee, na kwa maana hiyo kiasi chochote kitakachokuwa kwenye mfuko wa hifadhi kitakuwa kimetwaliwa na serikali.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema kitendo kilichofanywa kimewashangaza wadau wengi.

“Bunge tumeshangazwa kama ninyi mnavyoshangaa kwa sababu taratibu za utungaji wa kanuni sisi huwa hatuhusishwi, ila kwenye sheria huwa kuna vifungu (provisions) kadhaa za kuwapa wizara husika na hiyo sheria mamlaka ya kutunga kanuni kwa mambo ambayo yanabadilika badilika.

“Mojawapo katika sheria hiyo iliamuriwa kuwa ile kanuni (formula) itakavyokuwa isiwekwe ndani ya sheria ila iwekwe ndani ya kanuni ili kutoa nafasi kama formula hiyo watu wataichoka iweze kubadilishwa kiurahisi, maana yake ukiiweka ndani ya sheria ya Bunge mchakato wake unakuwa mrefu, hata kama kuna makosa yamefanyika kurekebisha kwake huwa ni kazi sana.

“Kwa hiyo tukawakabidhi wenzetu [Serikali]. Kwa kawaida kanuni zinazolalamikiwa si hizo peke yake. Ziko kadhaa. Miaka ya karibuni tulianzisha Kamati ya Sheria Ndogo. Kanuni iko kwenye kundi la sheria ndogo, maana kanuni ni sheria,” amesema Spika Ndugai.

Kiongozi huyo wa Bunge amesema kama kanuni fulani inalalamikiwa sana na wananchi, kwa kawaida Bunge linaipokea na kuipeleka kwenye kamati, na mle kuna wanasheria wengi wanasaidia kupitia zile kanuni na wakati mwingine kutoa ushauri kwa Serikali. Wakati mwingine ikibidi wanatoa ripoti bungeni na Bunge linaielekeza Serikali.

“Kamati hii ndiyo peke yake ambayo inatoa taarifa zake bungeni mara mbili kwa mwaka. Kamati nyingine zote zinatoa mara moja. Tunafanya hivyo kwa sababu kanuni zinazotungwa nchini ni nyingi…halmashauri zote za wilaya, manispaa, majiji – wote wanatunga kanuni na maeneo mbalimbali wanatunga kanuni,” amesema Ndugai.

Amesema si rahisi Bunge kupitia kanuni zote, bali huwa linatoa kipaumbele kwa kanuni ambazo zinalalamikiwa sana. Kwa hiyo itakuwa vizuri kama kanuni hiyo inalalamikiwa Bunge likapata ushauri huo na kutumia nafasi yake katika kushauri kuepusha jambo kama hilo.

“Kilichokuwa kinasikitisha ni kuwa watu wote wanashambulia Bunge kwamba ndilo limepitisha, lakini hawasemi sheria hiyo namba ngapi, kipengele kipi hasa ambacho Bunge lilitunga ambacho kimesema hayo maneno.

“Wananchi wasikate tamaa, bado nafasi ipo. Mifumo yetu imewekwa katika namna hiyo kwamba tunaweza kushauriana, kurekebishana huku na huku,” amesema Ndugai.

Kumekuwapo ukokotoaji kama huu kwingineko duniani? Spika Ndugai anasema: “Hilo siwezi ku- comment, lakini ni swali ambalo kama likiletwa kwetu tulishughulikie ndiyo maswali ambayo watakuwa wanaulizwa wataalamu ambao wamekuja na fomula kama hiyo kwamba wapi fomula ya aina hii inatumika, msingi wake ni nini. Kwanini isiwe asilimia 75 apewe [mstaafu] ikabaki kidogo, au vinginevyo.

“Huenda wana maelezo ya kutosha walioweka kanuni hiyo. Huenda wana maelezo ambayo wakitupatia tunaweza tukaridhika, lakini kwa sasa wote tuko puzzled [tuko kwenye mshangao] kama mlivyo ninyi. Wote hatuelewi kwanini fomula hii imekuwa hivi.”

 Je, kanuni inalenga kulinda mifuko inayodaiwa kuwa na hali mbaya? Spika Ndugai anasema: “Bunge lijalo suala hili linaweza likapata nafasi ya kujadiliwa vizuri kwa sababu kinachofanyika sasa ni consolidation ya yale mashirika yaliyokuwepo kuja kwenye chombo kimoja cha wafanyakazi wa Serikali na chombo kingine cha wafanyakazi wa sekta binafsi.

“Katika kipindi hiki bila kupata taarifa kamili ya hali ikoje – kulikuwa na mashirika yanafanya kazi vizuri, mengine yalikuwa yanasuasua sasa katika kuyaweka kwenye mwavuli mmoja huwezi kujua.

“Inawezekana kuna mambo wenzetu wa Serikali wameyaona ambayo sisi hatujapata picha yake, ndiyo maana nasema siyo vizuri kutangulia boti, ni vizuri tuwe na uvumilivu mpaka wakati huo tutapata maelezo ya kutosha na tutawashauri wenzetu pale tunapoona kwamba panahitaji kuangaliwa vizuri zaidi. Taratibu zetu ni mpaka kikao kijacho, hapa katikati hatuwezi kulishughulikia.”

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, William Ngeleja, amezungumza na JAMHURI na kuwatoa hofu wananchi.

“Nampongeza Mheshimiwa Spika kwa kulitolea ufafanuzi na kuwatia matumaini wananchi kwa sababu kwa mujibu wa mfumo wetu wa utungaji wa sheria bado kwenye sheria hizi ndogo ambazo pia zinabeba hizi kanuni; ni kweli kwamba fursa ipo ya kufanya marekebisho yoyote kama itaonekana kwamba marekebisho yanaweza kuwa na tija, yakazingatia masilahi mapana ya Watanzania,” amesema Ngeleja.

Amesema kwa mfumo wa sheria, sheria ikishatungwa na Bunge inaacha wigo kwa waziri husika kwa niaba ya Serikali kutunga kanuni ambazo ndizo zinazowezesha utekelezaji wa majukumu ya kila siku yaliyoainishwa kwenye sheria.

“Hata kwenye hili kanuni zimetungwa, lakini kwa utaratibu zitakuja bungeni kupitia Kamati ya Sheria Ndogo ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Chenge, mimi ni makamu wake.

“Naungana na Mheshimiwa Spika kuomba wananchi na Watanzania wote kwa ujumla watulie. Bado fursa ipo kwa sababu nina hakika kwamba kwenye session zijazo za Bunge lazima litakuja.

“Kanuni zitaletwa bungeni na zikishawasilishwa, basi jukumu letu sisi kama Kamati ya Sheria Ndogo ni kuzichambua hizo kanuni.

“Nawapa matumaini wananchi, wawe wavumilivu, watulie, mfumo wetu wa kisheria unaruhusu hiyo fursa. Sisemi tutakwenda kubaini nini, lakini nasema fursa hiyo ipo ya kupitia tuone mahali ambako tunaweza kupafanyia kazi.

“Vilio hivi vya wananchi si siri, sisi sote tunasoma mitandao, tunasoma vyombo vya habari, tunasoma magazeti, tunaangalia televisheni …kila Mtanzania amesikia. Kwa sababu mambo hayaamuliwi kwa sababu ya yanavyozungumzwa sana, mimi naomba Watanzania watulie, tuna utaratibu mzuri katika nchi yetu,” amesema Ngeleja.

Kanuni kutumika

Kuhusu kutumika kwa kanuni kabla ya kupata Baraka za Bunge, Ngeleja amesema: “Huu ndiyo mfumo wetu wa sheria tulionao [wa kanuni kuanza kutumika kabla ya kupelekwa bungeni].

“Mfumo huu unatumika sana kwenye nchi zilizotawaliwa na Uingereza. Nchi nyingi zilizokuwa chini ya dola ya Uingereza zina mfumo huu. Ngazi ya kanuni au sheria ndogo serikali inatunga halafu inaleta bungeni, lakini ikijitokeza kasoro kubwa ya msingi inabatilishwa, inasimama hapo hapo tangia ilipowasilishwa bungeni.

“Ukitaka kubadilisha hilo linahitaji ridhaa ya Watanzania wote na mfumo wetu wa utungaji sheria. Si jambo la kubadilishwa na Bunge…lazima tuzungumze. Hii changamoto inatoa fursa ya kutafakari mfumo wetu wa utungaji wa sheria tulionao. Nchi nyingine zina mfumo ambao hizo kanuni haziwezi kuanza kutumika mpaka kwanza zipitiwe na bunge.”

Ngeleja anasema ufafanuzi anaotoa unazingatia mfumo wa kisheria nchini.

“Kwa hatua hiyo ya sasa serikali haijakiuka utaratibu wowote japo maudhui yake yanaonekana yana changamoto, tutajadili kwenye hatua inayofuata,” amesema Ngeleja.

Anasema sheria inataka kanuni zipelekwe bungeni. “Serikali haitakwepa hilo. Isipokuwa kwamba inazitunga na kuanza kutumika kabla ya kuzileta bungeni, ndiyo utaratibu wetu wa utungaji sheria.

“Sheria ndogo nyingi zimekuwa zikitungwa na kufanya kazi, lakini hili ni jambo tofauti ndiyo maana tunasema pengine tunaweza kutumia fursa hii kuangalia mfumo wetu. Na hilo linahitaji mjadala mpana kwa sababu huo mfumo nao una faida zake na una changamoto kama unavyoona.

“Wakati mwingine Serikali ina majukumu, kama haitapewa fursa ya kutunga hizi kanuni unaweza kukuta Bunge liko out of session – kuna jambo limejitokeza la muhimu litungiwe kanuni kwa muda mfupi ili litekelezeke, hakuna hiyo fursa kwa Serikali. Ni jambo la kujadili kwa upana. Kubadili mfumo tunahitaji kujadiliana kati ya Bunge na Serikali.

“Sisi tumesikia, tumeona hoja za wananchi, kwa hiyo tuamini hii si changamoto ya kwanza. Zipo changamoto zilishajitokeza tukazimaliza. Wananchi watulie. Sisi wote ni Watanzania kila jambo linafanyika kwa nia njema kama kasoro zimejitokeza zitashughulikiwa. Tunaomba wananchi watulie kwa sababu tuna utaratibu mzuri wa kimfumo,” amesema Ngeleja.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Anthony Mavunde, ameulizwa na JAMHURI  msimamo wa Serikali baada ya kusikia malalamiko ya wananchi, lakini hakuwa tayari kutoa maelezo ya suala hilo.

“Hili suala liko juu yangu, lipo ngazi za juu, nakushauri uzungumze na Mheshimiwa Waziri (Jenista Mhagama), yeye atakupa majibu,” amesema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Jenista Mhagama, alipopigiwa simu alitaka aandikiwe ujumbe mfupi. Hadi tunakwenda mitamboni alikuwa hajajibu maswali aliyopelekewa.

Kanuni ya ukokotoaji iliyotangazwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), imeibua malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, hasa wastaafu wakiona kanuni hiyo inalenga kuwakomoa na kuwafanya wafe wakiwa maskini.

Spika Ndugai amenukuliwa na Gazeti la Nipashe akimsifu Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya, ambaye pia ni Waziri Kivuli Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), aliyeibua suala hilo juu ya pensheni hiyo.

Bulaya anasema kikokotoo kipya kilichotungwa na Serikali ni kitanzi kwa wastaafu kwa kuwa hawatanufaika na fedha zao ambazo wamezitolea jasho kwa miaka mingi.

Bulaya anasema wabunge walitaka kikokotoo kiwepo kwenye sheria, lakini Bunge likaambiwa kitawekwa kwenye kanuni zinazotungwa na waziri kwa masilahi ya Serikali.

Bulaya anasema wadau waliwataka wabunge wakijue kikokotoo hicho na waliomba kisiwe 1/580 bali kiwe 1/540 au pungufu, lakini kilifichwa na hakikujulikana kwa watunga sheria hao.

Wananchi wengi kote nchini wameonyesha chuki za wazi juu ya kanuni hiyo wakisema inawakomoa bila kujali ukweli kuwa fedha za pensheni ni haki inayotokana na jasho la kazi zao.

Kwa mujibu wa Gazeti la Uhuru, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Jamii (SSRA), Irene Isaka, alisema mageuzi ya kisheria na kimfumo kwenye sekta ya hifadhi ya jamii nchini ambayo mwishowe yameunda mifuko ya NSSF kwa ajili ya wafanyakazi wa sekta binafsi na isiyo rasmi pamoja na PSSSF kwa ajili ya watumishi wa sekta ya umma.

Irene alinukuliwa akisema kuna wastaafu zaidi ya 7,000 ambao awali walipaswa kulipwa mafao yao ya mkupuo badala yake wakawa wanalipwa mafao ya kila mwezi, sasa watalipwa fedha zao hivi karibuni.

“Mageuzi haya ni mageuzi ambayo yataboresha maisha ya Watanzania na maisha ya wanachama wa hifadhi ya jamii…hivyo namshukuru sana Rais Dk. John Magufuli, chama cha waajiri, vyama vya wafanyakazi na kila aliyehusika kwenye mafanikio haya.

“Niwahakikishie wanachama rasilimali zote zikiwamo hazi za awala za hazina, hati fungani za serikali, hati za amana za benki na hati za viwanja vyote vimetunzwa vizuri Benki Kuu ya Tanzania (BoT)…hakuna kilichoharibika,” alinukuliwa Irene  na Gazeti la Uhuru.

Katika toleo Na. 227 la JAMHURI la mwaka 2016, kulikuwa na habari kubwa iliyohusu ‘kifo cha mifuko ya jamii’.

Sehemu ya habari hiyo ilisomeka: “Deni kubwa ambalo Serikali inadaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, linatishia uhai wa mifuko hiyo, kiasi cha baadhi kuanza kusuasua na hata shindwa kulipa mafao kwa wanachama wake, JAMHURI linathibitisha.

Hadi mwanzoni mwa mwaka jana, mifuko yote sita, ilikuwa ikiidai Serikali Sh trilioni 7.134 ambazo ni mikopo na riba. Deni hilo ni matokeo ya uamuzi wa Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, kukopa kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo. Pamoja na nia njema, sasa mzigo wa deni hilo unaonekana kuisumbua Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli, na tayari mipango imenza kufanywa na Serikali ili kuinusuru mifuko hiyo.

Fedha nyingi zilizokopwa zinatajwa kutumika katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kinachotajwa kuwa chuo cha aina hiyo kikubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mifuko hiyo ni: Mfuko wa Akiba wa Watumishi Serikalini (GEPF), Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Jamii kwa Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma (PPF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSPF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Vyanzo vya habari kutoka serikalini vimesema kutokana na Serikali ya Awamu ya Nne, ama kushindwa, au kusuasua kulipa; sasa deni hilo, likijumuishwa na riba, linakaribia Sh trilioni 10. Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2015/2016 ni Sh trilioni 22.

Imebainika kuwa Serikali ya Awamu ya Nne, kupitia Wizara ya Ajira, Kazi na Vijana ilishabaini na kukiri mtanziko wa ulipaji deni hilo, kiasi cha kuilazimu kutangaza ‘hali ya hatari’ inayolikabili taifa endapo deni hilo halitalipwa haraka.

Taarifa ya siri ambayo JAMHURI imeipata inaonyesha kuwa hali ni mbaya zaidi kwa Mifuko ya PSPF na LAPF. PSPF ililazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuwalipa watumishi wa umma ambao hawakuwahi kuchangia kwenye mfuko huo.

Vyanzo vya habari vimesema hali hiyo imeitisha Serikali, na tayari Rais John Magufuli, ameshaanza kuchukua hatua za dharura katika kuhakikisha kuwa deni hilo linalipwa ili kuilinda mifuko na kuwaondolewa usumbufu wastaafu kupata mafao yao.

Mwaka jana Wizara ya Kazi ilikiri kuwa hali ya Mifuko ya Jamii si nzuri, hususan kwa mifuko ya PSPF na LAPF ambayo katika kipindi cha muda mfupi iliaminika kuwa ingeshindwa kuwalipa wanachama wake, hivyo kusababisha matatizo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Kiasi ambacho mifuko inaidai Serikali kikiwa kwenye mabano ni: PSPF (Sh trilioni 4.828), NSSF (Sh trilioni 1.334), NHIF (Sh bilioni 458.6), PPF (Sh bilioni 288.6), LAPF (Sh bilioni 207.7) na GEPF (Sh bilioni 18).

“Madeni haya yanaathiri sana mtiririko wa fedha pamoja na uwezo wa mifuko kuhimili malipo ya mafao ya wanachama wake. Uwezo wa mifuko kuhimili malipo ya mafao kwa wanachama hupimwa kwa kulinganisha kiwango cha dhima dhidi ya mali za mfuko (liability vs asset).

“Kulingana na tathmini, deni kubwa la Serikali kwa Mfuko wa PSPF limechangia sana katika kuufanya mfuko huu kuwa na uwiano dhaifu wa dhima na mali ikilinganishwa na mifuko mingine ya Hifadhi ya Jamii.

“Uwiano kati ya dhima na mali (funding level katika Mfuko wa PSPF ni asilimia 10.1,” inasema taarifa ya siri ya Serikali.

Inaelezwa kuwa uwiano huo ni dhaifu na inakadiriwa kuwa mwaka huu mfuko huo huenda ukakosa kabisa uwezo wa kulipa dhima ya mafao kwa wanachama wake wanaostaafu na hivyo kutishia uendelevu wa mfuko.

Pamoja na changamoto ya madeni makubwa ambayo Serikali inadaiwa, nyingine inatajwa na Wizara ya Ajira, Kazi na Vijana kuwa ni baadhi ya mifuko kulipa mafao makubwa yanayoathiri mtiririko wa fedha za mifuko.

Wiki iliyopita, Bulaya alisema deni la serikali kwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii (NSSF na PSSSF) limepanda hadi Sh trilioni 8.