Mkurugenzi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Justine Mwandu, amejitokeza kufafanua shutuma za taasisi hiyo kuuza nyumba zake kwa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na kukwepa wakazi wanaoishi humo.

Mwandu amesema uuzwaji wa nyumba na kuachishwa kazi kwa wafanyakazi wa shirika hilo, ilikuwa ni mikakati ya Serikali kuliunda upya shirika hilo na hakukuwa na ukiukwaji wa taratibu wala unyanyasaji kama inavyodaiwa.

Kauli hiyo ya Mwandu inakuja siku chache baada ya NIC kulalamikiwa na Rose Roezer, aliyekuwa mfanyakazi wa shirika hilo, kuwa shirika limekiuka taratibu za uuzwaji wa nyumba na kumnyanyasa. Nyumba zinazolalamikiwa ni zile zilizopo katika viwanja Namba 75-78, Kitalu 45 B, Kijitonyama, kandokando ya Barabara ya Bagamoyo, Dar es Salaam. Vilevile Rose anadai kuwa hata kutoendelea kwa ajira yake ulikuwa ni unyanyasaji uliofanywa kwa makusudi na uongozi wa shirika dhidi yake.

Katika mawasiliano ya Mwandu na mwandishi wa habari hii yaliyofanyika hivi karibuni jijini kupitia barua yenye kumbukumbu Namba: NIC/MD/1/2014 ya Oktoba 27, 2014 ilielekezwa kwa mwandishi.

Mwandu anasema: “Mlalamikaji Rose alikuwa mfanyakazi wa Shirika akiwa na mkataba wa ajira ya mkataba wa miaka mitatu yaani kuanzia mwaka 2010 hadi 2012, ambapo mkataba wake wa ajira ulimalizika. Kama ambavyo unafahamu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kulifanyia marekebisho makubwa Shrika la Bima la Taifa na kuliunda upya,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Katika moja ya mikakati ya kuliunda upya shirika ilikuwa ni kuwaachisha kazi wafanyakazi wote. Hivyo mnamo Februari 2009, iliwaachisha kazi wafanyakazi wote 506 ili kupisha uundwaji huo. Barua hiyo ya Mwandu inasema kwamba Rose alikuwa ni mmoja wa walioachishwa kazi na kuomba upya na baadaye kufanikiwa kuajiriwa katika masharti ya ajira ya mkataba wa miaka mitatu mnamo mwaka 2010 kwenye NIC mpya.

Anasema wakati Rose akiwa mfanyakazi wa NIC, alikuwa akiishi katika moja ya nyumba za wafanyakazi wa shirika zilizoko Kijitonyama. Baada ya mchakato wa kurekebisha Shirika kuanza, nyumba hizo za wafanyakazi pamoja na nyinginezo zinazomilikiwa na NIC nchi nzima, ziliuzwa kwa mashirika na taasisi za umma kwa maagizo ya Serikali.

Baadhi ya wafanyakazi wa iliyokuwa NIC ya zamani walioachishwa kazi mwaka 2009, akiwamo Rose walifungua kesi mahakamani kupinga kuuzwa kwa nyumba hizo pamoja na madai mengine ya wao kupewa kipaumbele cha kuzinunua nyumba hizo walizokuwa wanaishi.

“Kesi waliyoifungua bado iko mahakamani katika Mahakama Kuu-Kitengo cha Ardhi. Namba ya kesi hiyo ni 64/2013. Katika kesi hiyo, wadai ni Evans Buhire, Rose na wengine,” anasema.

Mwandu anaongeza kuwa madai ya Rose ya kuwa uuzwaji wa nyumba hizo ni ukiukwaji wa taratibu, pamoja na kutoendelea kwa ajira yake kuhusishwa na unyanyasaji hayana msingi na ni upotoshaji.

Wakati huo huo Rose naye akizungumza na JAMHURI anasema, mauzo ya nyumba hizi hayakufuata utaratibu na sheria za kuuza nyumba za umma. Kuna uchakachuaji wa hali ya juu umefanywa katika mauzo ya nyumba hizi. “Kwanza inashangaza tamko la Serikali la kuuza nyumba lilitoka Oktoba 15, 2009. Tamko hilo lilitoka wakati ambao nyumba zimeshauzwa. Nyumba ziliuzwa Oktoba 8, 2009. Kingine hapa ni kwamba nyumba hizi ni mali ya umma, hivyo zilitakiwa ziuzwe kwa zabuni, kitu ambacho hakikufanyika,” alilalamika.

“Hakukuwa na zabuni yoyote iliyofanyika, walipeana nyumba kimyakimya. Wakazi tuliomo ndani ya nyumba hizi tulitaarifiwa tu kuwa nyumba zimekwishauzwa, kitu ambacho si utaratibu na kinyume cha sheria za nchi. Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1993 (Public Corporation Amendment Act, 1993), Kifungu cha 43 kifungu kidogo cha 1 (a) na (b) havikuzingatiwa,” anaeleza Rose kuhusiana na madai yake hayo kwa shirika hilo.

Taarifa zinaeleza kuwa mnamo Agosti 3, 2011, NIC ilitoa notisi ya siku saba ikiwataka wafanyakazi wake waliokuwa wakazi kwenye majengo hayo akiwamo Rose kuhama kumpisha mnunuzi wa majengo, huku ikiwatahadharisha kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya watakaokaidi agizo hilo. Taarifa zinaainisha kuwa notisi hiyo ilifutwa na shauri lililofunguliwa mahakamani.

Katika kuthibitisha madai yake, Rose ameionesha JAMHURI nyaraka kadhaa zikiwamo barua alizoandikiwa na NIC. Moja kati ya barua hizo iliyoelekezwa kwake ni ile yenye Kumb. Na NIC/ADM/PF/104 ya Septemba 9, 2011 iliyosainiwa na Anne Mbughuni kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Justine Mwandu.

Barua hiyo ilimweleza Rose kuwa: “Ulishauriwa, kama unataka kuendelea na mashtaka ya mwajiri usikubali ajira ya NIC, ila wewe ukatoa kauli kuwa umejitoa katika kesi hiyo. Barua yako kwa M. M and Associates Advocates na barua ya M. M and Associates Advocates kwa NIC zinaonesha kuwa hujajitoa katika hiyo kesi. Hivyo uliudanganya uongozi, na wakati huo huo, umekaidi agizo la mwajiri wako la kukutaka uhame katika nyumba ya shirika ndani ya muda uliotajwa.”

1374 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!