*Tuhuma za Kabwe zafumua kashfa ya ‘kuuzwa’ bustani

*Ni ya Mtaa wa Samora, ujenzi wafanyika usiku bila kibali

Wakati wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakitaka Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe, achunguzwe kutokana tuhuma za kuipatia kazi Kampuni ya Tanzania Buildings Works, taarifa mpya zinasema vigogo Manispaa ya Ilala nao wameingia katika kashfa ya ‘kuuza’ eneo la wazi.

Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili imezifanyika kazi takribani kwa wiki mbili, zinasema kwamba vigogo hao ‘wameuza’ eneo hilo la bustani lililopo katikati ya mitaa ya Samora na India jijini Dar es Salaam, ambalo hutumika kwa ajili ya bustani ya mapumziko.

Waliopewa eneo hilo la wazi ni Kampuni ya Easy Payment Limited. Kampuni hiyo imepata bustani hiyo kwa njia zinazoelezwa kuwa ni za kifisadi, Gazeti la JAMHURI, limeshuhudia.

Taarifa zinasema kwamba tangu enzi za ukoloni na baadaye Uhuru wa Tanganyika (Tanzania), eneo hilo lilitengwa na jiji kwa matumizi ya bustani ya kupumzika, na mwaka 2010 liliboreshwa zaidi na kuwekwa choo cha umma kwa sababu ya ongezeko la watu.

Madudu katika Jiji la Dar es Salaam yamekuwa kero kiasi cha wabunge kuomba mwongozo wa kutaka kuchunguzwa kwa Kabwe, kutokana madai ya kuipendelea kampuni hiyo ambayo imeelezwa kushindwa kutekeleza miradi ya ujenzi katika mikoa yote aliyoiongoza ikiwamo Mbeya na Mwanza na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni 3.

Akiomba mwongozo kwa Mussa Azzan Zungu, aliyekuwa akiongoza Bunge, Ijumaa iliyopita kutokana na kauli ya Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, wa kutaka kuchunguzwa kwa kampuni hiyo, Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, amesema mkurugenzi huyo chini ya uongozi wake ndiyo aliyetoa kazi kwa kampuni hiyo ambayo alipohamishiwa mkoani Mwanza pia aliipa kazi na kusababisha hasara kubwa.

Akitoa mwongozo, anatupia lawama Serikali kwa kutosikiliza malalamiko ya wananchi na kuwahamisha viongozi wabovu wanaotenda makosa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine.

Kuhusu bustani ya Samora, gazeti hili limebaini kuwa Februari 8, 2012 eneo hilo ‘lilivamiwa’ na Kampuni ya Easy Payment Ltd mara baada ya kusaini mkataba unaoelezwa kuwa ni kwa ajili ya kupaboresha huku viongozi wa Manispaa ya Ilala wakibariki.

Mafundi wa Kampuni ya Easy Payment Ltd wanafanya shughuli za kuendeleza eneo hilo usiku tu kwa kujenga mgahawa mkubwa ulipewa jina la Harold. Imeelezwa kwamba mkataba huo utadumu kwa kipindi cha miaka mitano.

Kitendo cha kampuni hiyo kuendesha shughuli zake za ujenzi wa jengo ndani ya eneo hilo bila kibali cha ujenzi, kimeelezwa na wananchi wanaoishi jirani na bustani hiyo kuwa ni mkakati wa baadhi ya viongozi kupora maeneo ya wazi yaliopo katikati ya jiji.

“Kama kweli kuna usafi kwenye mradi huu uendelezwe usiku tu na siku za Jumapili au mapumziko? Kiko wapi kibao cha ujenzi?” anahoji Elias John anayefanya kazi jirani na eneo hilo na kuendelea:

“Miaka minne iliyopita vilijengwa vyoo vya umma na kuliacha eneo hilo likiwa na mandhari nzuri, lakini sasa tunaona wamejenga uzio na jengo ambalo linadaiwa kuwa ni mgahawa, mashine za kutolea fedha (ATM), wamekata miti ya kivuli na kuzuia njia zote zilizopita katikati ya bustani hiyo.”

Anaeleza kuwa hali ya uvamizi wa maeneo ya wazi inatisha na Serikali isipokuwa makini, maeneo mengine muhimu  yatauzwa   kwa maslahi ya watu wachache.

Naye, Juma Suleiman anayefanya shughuli zake za biashara Mtaa wa India, anasema kuwa jambo linalowashangaza ni shughuli za ujenzi wa jengo la kudumu ndani ya bustani hiyo zinazofanyika kwa kuvizia nyakati za usiku bila kibali cha ujenzi huku Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, akitembelea mara kwa mara.

Kwa mujibu wa chanzo chetu kingine cha habari (jina tunalo),  walipeleka taarifa za uvamizi wa eneo hilo kwa Mtendaji Kata ya Mchafukoge, Yusuph Mkwawa, Julai 11, mwaka huu na alipopeleka amri ya kusitisha ujenzi wahusika hawakuipokea huku wakidai uongozi wa Manispaa unafahamu kinachoendelea.

“Julai 15 mwaka huu, tulimwona Mkurugenzi wa Manispaa na kumwomba asitishe shughuli za ujenzi unaoendelea ndani ya bustani hiyo, lakini hakuna kilichofanyika hadi sasa,” anaeleza mtoa habari huyo.

Mkwawa alipohojiwa kuhusu taarifa hizo akasema, “Nafahamu jambo hili. Nakumbuka mwezi Julai niliambatana na Ofisa Mkaguzi wa Majengo wa Kata hadi eneo la tukio ili kuwakabidhi nakala ya amri ya kusitisha ujenzi, lakini waligoma kuipokea kwa madai kuwa viongozi wa Manispaa wanafahamu suala hilo.”

Naye Ofisa Mkaguzi wa Majengo wa kata hiyo, Dotto Muhombolage, alipohojiwa na JAMHURI anaeleza kuwa Juni 23, mwaka huu, aliagizwa na mkuu wake wa kazi (Mhandisi wa Manispaa) kupeleka nakala ya amri ya kusitisha shughuli za ujenzi ndani ya bustani hiyo, lakini hakuna aliyepokea.

Muhombolage anaeleza baada ya wahusika kukataa kuipokea nakala hiyo, aliamua kubandika kwenye uzio wa mabati uliozungushwa katika eneo hilo ili wahusika wanaposoma wasitishe ujenzi huo.

“Kipindi hicho niliagizwa kupeleka nakala ya amri ya kusitisha ujenzi ndani ya bustani hiyo, unaofanyika bila kibali cha ujenzi, kulikuwa na mchanga na kokoto tu huku miti ya kivuli iliyopandwa muda mrefu ikikatwa yote na anayejenga ndani ya eneo hilo,” anaeleza.

Anasema Julai 2, mwaka huu aliagizwa tena na mhandisi  kupeleka nakala nyingine (remainder), nayo pia haikupokewa na wahusika na hivyo kuamua kuibandika  tena kwenye uzio wa mabati uliozungushwa katika eneo hilo.

Hata hivyo, alieleza kuwa hafahamu lolote kuhusu hatua zilizochukuliwa hadi sasa na anayeweza kuzungumzia hilo ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mgulumi.

Chanzo chetu kingine ndani ya Manispaa ya Ilala (jina tunalo), kimeeleza kuwa mkataba uliosainiwa baina ya uongozi wa Manispaa na Kampuni ya Easy Payment Ltd umejaa mashaka kwani haikuruhusiwa kujenga jengo la kudumu ndani ya eneo hilo la wazi.

Chanzo chetu kimeeleza kuwa mkataba wa kubadilisha matumizi ya eneo hilo ulioanza Januari 20, 2012 hadi Januari 2017 unadaiwa kughushiwa na uongozi wa kampuni hiyo kwa msaada mkubwa wa vigogo wa manispaa hiyo, kwa lengo la kujimilikisha eneo la wazi kinyume cha sheria.

“Hawa jamaa hawana kibali cha ujenzi ndani ya eneo hilo, mkataba wao unatia shaka na kinachofanyika eneo hilo ni uharibifu wa mazingira na mandhari ya jiji, na kinachotajwa kuwa kuweka vivutio na kuboresha bustani hiyo ni utapeli mtupu,” kinaeleza chanzo hicho.

JAMHURI ilipomtafuta Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Mgulumi, ili kuelezea uvamizi wa eneo hilo la wazi, hakuweza kupatikana, na alipotumiwa ujumbe mfupi (sms) wa maswali katika simu yake kiganjani hakutoa jibu lolote hadi tunaingia mitamboni.

Naye, Meya wa Manispaa ya Ilala, Silaa, anayedaiwa kukagua shughuli za ujenzi unaofanyika bila kibali nyakati za usiku, alipotafutwa na Gazeti la JAMHURI kwa simu yake ya kiganjani, anasema kwamba wanachokifanya ni kuendeleza tu maeneo hayo na kwamba tayari wamefanya uendelezaji hata eneo lililo jirani na Hospitali ya Ocean Road, jijini.

Aliyekuwa Mwanasheria wa Manispaa hiyo, John Wanga, ambaye ni miongoni mwa watu waliosaini mkataba huo unaodaiwa kuwa ni wa kitapeli, na sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema haelewi chochote na mwenye maelezo ya kutosha ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.

Meneja Mkuu wa Kampuni Easy Payment Ltd, Hillary John, naye pia hakuweza kupatikana, lakini alipotafutwa kiongozi mwingine wa kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Musa, alikwepa kuzungumzia chochote kuhusu eneo hilo na kuwatupia mpira viongozi wa Manispaa ya Ilala kuwa wao ndiyo wasemaji na kukata simu.

By Jamhuri