Kindumbwendumbwe cha uchaguzi kwa ajili ya kuwapata wenyeviti wa serikali za mitaa na wenyeviti wa vitongoji ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) umemalizika hivi karibuni. Naam, kuna walioshinda na walioshindwa.

Utaratibu huo wa kuwapata wagombea katika nafasi hiyo ndiyo dira pekee ya hali ya Uchaguzi Mkuu wa kuwapata madiwani, wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kadhalika, mashekha na wawakilishi kwa upande wa visiwani.

Utaratibu huo ni tata. Hii ni kwa sababu ya kuleta mgawanyiko kwa wanachama na wagombea ambao hawakushinda.

Katika kufuatilia baadhi ya vituo mbalimbali vya upigaji kura pamoja na jinsi mchakato wa kuwapata wagombea ulivyofanyika katika mchakato uliomalizika hivi karibuni, baadhi ya uongozi katika serikali za mitaa na vitongoji wamewachagua baadhi ya wagombea ambao hawakubaliki.

Wagombea ambao hawakubaliki wamekuwa wakitumiwa na baadhi ya makada wenye nguvu katika chama hicho, ikiwa ni pamoja na kutoa ufadhili wa fedha kwa ajili ya kushawishi wasimamizi wa mchakato huo ndani ya chama.

Mfano mzuri ni namna alivyopatikana mgombea wa CCM katika Mtaa wa Kuzenza, Kata ya Butimba A, wilayani Nyamagana, ambapo wagombea wengi katika nafasi hiyo hawakupewa ratiba ya kufanya kampeni. Ni mmoja tu aliyefanikiwa, naye anaelezwa kuwa hakubaliki.

Hakubaliki kwa sababu elimu yake ni ya chini. Ni darasa la nne. Kuwaacha wasomi wenye upeo wa hali ya juu katika masuala ya kiutawala, ni kuwapa nafasi wagombea wengine kutoka vyama vya siasa ikiwa ni pamoja na Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF kuchukua mtaa hiyo.

Kwa mfano, mgombea aliyepata nafasi ya pili katika uchaguzi huo ni mstaafu katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambaye kutokana na elimu yake ni mtaalamu wa masuala ya utawala na siasa, na taaluma yake angeweza kushirikiana na baadhi ya viongozi wengine.

Anayeshika nafasi ya tatu ni Mhadhiri katika Chuo cha Mtakatifu Augustino (SAUT) ambaye kitaaluma ni mtaalamu wa uhusiano wa kitaifa na kimataifa na masuala ya habari. Hakuweza kupata nafasi ya kupiga kampeni kutokana kwamba wasimamizi wa mchakato huo walimficha muda wa kuanza kampeni.

Kada wa CCM, Deo Bugarama, aliyeratibu shughuli hiyo anakiri kutokea dosari hiyo na kusababisha wagombea hao wawili ambao walikuwa katika kinyang’anyiro hicho kutopata nafasi ya kupiga kampeni, jambo lililosababisha kushindwa kujiandaa na uchaguzi.

Matokeo yake, sasa endapo mambo yatakuwa hivyo kama ilivyo la kumuweka mgombea ambaye hana sifa na wala ‘hakubaliki’ kwa wananchi isipokuwa kwa vinara wa CCM ndani ya chama hicho, wananchi huenda wakapigia kura wapinzani.

Tatizo hilo pia limejitokeza katika Kijiji cha Kadashi, Kitongoji cha Maligisu, wilayani Kwimba wakati wanapiga kura hawakuweza kumshangilia mshindi katika kinyang’anyiro hicho kutokana na baadhi ya wapigakura wapatao 350 kutoka katika vitongoji vingine kwa ajili ya kumpigia mgombea ambaye pia ‘hakubaliki’.

Baada ya msimamizi wa uchaguzi kutangaza matokeo hayo, hakuna mwananchi yeyote aliyefurahia, kadhalika mgombea mwenyewe hakushangilia ushindi huo. Hii ni kwa sababu walitangaziwa mshindi wasiyempenda. Ushindi huo wenye utata utaweza kuisababishia CCM kuwa na wakati mgumu katika uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa kijiji hicho pamoja na ule wa kumpata diwani na mbunge wa Jimbo la Busega.

Baadhi ya wanachama wamesikika wakisema kuwa kitongoji hicho kinachotawaliwa na CUF kitaendelea kushikiliwa na wapinzani na Jimbo hilo la Kwimba huenda likachukuliwa na wapinzani.

Katika Kitongoji cha Nyamikoma Centre wilayani Busega, nako chama hiki tawala kimeendeleza mchezo mchafu wa kuwakatia wapigakura kutoka CCM ambao walionekana kumuunga mkono mgombea anayekubalika. Baadhi ya wapiga kura wapatao 70 walizuiliwa kupiga kura licha ya kuwa na kadi.

Wanasema kwamba mgombea ambaye amepitishwa kwa ajili ya kushika nafasi ya mwenyekiti hakubaliki na wananchi na kudai kuwa kura hizo 70 pamoja na nyingine ambazo ni zile za kutoka kwa wananchi wenye shahada za kupiga kura, zinaangukia upinzani.

Pengine utaratibu huu ni miongoni mwa miongozo iliyowekwa na Kamati Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake, Rais Dk Jakaya Kikwete. Hakika mfumo huu unalenga kung’atua CCM madarakani wakati yeye anapomaliza muda wake mwakani.

Kwake Dk Kikwete kwa upande mwingine, nchi kuiacha mikononi mwa wapinzani (UKAWA) atakuwa imempatia heshima kubwa ndani ya nchi na upande wa kimataifa. Atakuwa ameonesha kwamba Tanzania chini ya uongozi wake, ameonesha demokrasia ya kweli kuiacha nchi ikiwa mikononi mwa mojawapo ya vyama vya upinzani.

Umaarufu wake utakuja kwa sababu amekuwa mstari wa mbele kukaa na kufanya majadiliano na vyama vya upinzani vinavyounda UKAWA, kukemea wazi wazi vitendo vya ufisadi na kupiga vita dawa za kulevya.

Nchi nyingine barani Afrika kama vile Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda, Burundi na nchi nyingine, bado viongozi wake wanataka kupindisha katiba za nchi ili waendelee na utawala, jambo ambalo haliko kwa Rais Kikwete.

Kutokana na mfumo huo wa sasa, ambao CCM umejijengea kulindana na kuwapo na utitiri wa wagombea nafasi za wenyeviti wa mitaa na vitongoji, udiwani, ubunge na rais, ni kujenga makundi ndani ya vyama hivyo na kuwapa mwanya mafisadi kujichagulia viongozi watakaowabeba katika uchaguzi huku ikiwa ni ashiria tosha la anguko la CCM katika uchaguzi wa mwaka 2015.

1222 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!