Wiki iliyopita, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF) vilionesha ukomavu wa kisiasa.

CHADEMA na CUF viliombana radhi siku moja baada ya kutokea mtafaruku mkubwa bungeni mjini Dodoma baina ya wabunge wa vyama hivyo, na kusababisha Naibu Spika, Job Ndugai, kuahirisha kikao cha Bunge.

 

Itakumbukwa kuwa chanzo cha mtafaruku huo ni hotuba ya Kambi ya Upinzani iliyosomwa na Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ezekiel Wenje, na kuihusisha CUF na vyama vinavyoshabikia ndoa za jinsia moja, ushoga na usagaji.

 

Matamshi hayo yalisababisha wabunge wote wa CUF kusimama na kuanza kumtusi Wenje bungeni, wakimtaka atengue kauli hiyo bila mafanikio.

 

Hata hivyo, siku iliyofuata, baada ya ushauri wa kiti cha Spika na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe na Mnidhamu wa CUF, Rashidi Ali Abdallah, waliviwakilisha vyama vyao kuombana radhi bungeni.

 

Tunapenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza CHADEMA na CUF kwa hatua hiyo ya kuombana radhi kwani vimeonesha ukomavu wa kisiasa.

 

Kitendo cha vyama hivyo kuombana radhi ni mfano mzuri wa kuigwa, na hasa ikizingatiwa kuwa hakuna binadamu asiye na upungufu. Tunaamini kuwa Wenje aliteleza kuzungumza maneno hayo na hata wabunge wa CUF nao waliteleza kumtusi mbunge huyo wa CHADEMA.

 

Ni kwa msingi huo sisi JAMHURI  tunaona kwamba kitendo cha vyama hivyo kuombana radhi kitaondoa chuki na uhasama, ambavyo vingejengwa na wabunge husika, hivyo kuchafua hali ya hewa ya kisiasa hapa nchini.

 

Katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa wa kisiasa, Watanzania tungependa kuona na kusikia busara na hekima vikitawala maneno na vitendo vya wanasiasa wetu wakiwamo wabunge.

 

Ni vizuri wanasiasa wetu wakiwamo wabunge wakatawaliwa na dhana ya kupingana kwa nguvu ya hoja, ili kuepuka mitafaruku isiyo na tija kwa jamii katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, mwaka 2015. Mungu wabariki wanasiasa Tanzania.

 

By Jamhuri