4.+Nape+akihamasisha+kwenye+mkutano+huo,+Kushoto+ni+Mlezi+wa+mkoa+wa+Dar,+Abdulrahman+Kinana2015 ni mwaka ambao macho na masikio ya Watanzania yanaelekezwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kuwa katika kipindi cha changamoto ya wanachama wake ambao wanasaka nafasi ya ukubwa wa nchi.
CCM inakumbana na changamoto ya wanachama wake kupigana vikumbo kutokana na baadhi ya vigogo ndani ya chama hicho kutangaza nia ya kugombea urais katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Watanzania wanaitazama CCM katika maono ya kipekee, jicho la tahadhari huku wakitoa tahadhari kwa chama hicho ambacho iwapo hakitokuwa makini katika kipindi hiki basi tutashuhudia chama hicho kikiparaganyika na kuwa vipande vipande.
CCM na viongozi wake wanapaswa kujiuliza nini wananchi wanataka katika kipindi hiki cha karne ya 21, vipaumbele na matarajio ya Watanzania katika kipindi cha miaka mitano ijayo.


Watanzania wana maono, ndoto na mahitaji ya lazima, hawahitaji tena viongozi wapiga porojo wasio na uthubutu, wasio na maamuzi na kuruhusu mambo ya hovyo kufanyika katika ardhi ya nchi yao.
Kila mwananchi kipindi hiki anatamani kuiona nchi ikipiga hatua za kimaendeleo ambayo yanasukumwa na viongozi wao kuanzia ngazi ya rais, wabunge na hata madiwani.
CCM inatakiwa kujitafakari katika kufanya maamuzi yake iwapo kitataka kuendelea kushika dola kama ilivyo malengo ya chama cha siasa.


Ijitafakari kwa kuhakikisha kinampa nafasi mtu atakayeuzika kwa wapigakura, anayeaminiwa na mwenye uthubutu vinginevyo itakuwa ni sawa na kuchezea shilingi chooni.
Ni matarajio yangu na Watanzania wenzangu kuona CCM na viongozi wake wakuu wakikaa na kufanya maamuzi stahiki kwa kuteua jina la mgombea mmoja anayekubalika ndani ya chama na nje ya chama kuwania nafasi ya urais.
Pamoja na nafasi hiyo nyeti, zipo nafasi za ubunge na udiwani ambazo CCm wamekuwa wakifanya makosa kwa kuweka wagombea wanaopendwa na chama sio wapigakura.Kipindi hiki iwapo kosa hilo litafanyika basi natarajia kuona chama hiki kikibwagwa mchana kweupe na kubaki wakilaumiana.
Nayasema haya kutokana na mnyukano uliopo ndani ya chama huku watangaza nia wakipigana vikumbo na kebehi za hapa na pale zikianza kutikisa kutoka kwa wapambe wao ambao wengi wao ni wachumia tumbo.


Sitarajii kuona CCM ikipatwa na kigugumizi kwa watangaza nia wake na kushindwa kutizama na kuenenda na upepo wa kisiasa unaotikisa ardhi ya Tanzania na watu wake.
Nchi sasa inatikiswa, inatikiswa na kutikisika kutokana na mchakato huu wa kutangaza nia kisha kutafuta wadhamini, nchi inatikishwa na vishindo vya kisiasa vinavyoendelea kushindiliwa na nguvu ya mabadiliko ya kweli inayosukumwa kuelekea uchaguzi mkuu.
Tumeweza kusikia jinsi watangaza nia wanavyojinadi, tumeshuhudia jinsi watu wanavyojitokeza kusikia kauli zao, na tutaendelea kusikia na kuona jinsi watakavyoongezeka idadi yao. Ni jukumu sasa la CCM kuangali na kukubaliana na ukweli uliopo kwa mustakabali wa nchi yetu.
Pamoja na kuwepo kwa makundi yanayosigana ndani ya chama, ni vyema chama hiki kikawa makini katika uteuzi wa wagombea wake hasa nafasi ya urais na sio kuishia kumegwa na makundi haya ambayo yamekuwa yakiishi kwa kuwindana na kumalizana kila iitwayo leo.


Sitarajii kuona chama hiki kikifanya makosa ambayo yatakuja kukigharimu miaka kadhaa ijayo, makosa ya kusimamisha mtu ambaye sio kipenzi cha watu, mtu ambaye hatoweza kuuzika na asiye na maono wala utayari wa kuwatumikia Watanzania. Mtu ambaye hatoweza kupigania maslahi ya nchi na watu wake.
Tunahitaji mtu atakayekuwa tayari kukataa wizi na ubinafsi uliotengenezwa na kupandikizwa katika akili za walio wengi, asiyependa kusifiwa zaidi ya kutimiza wajibu wake ipasavyo bila woga wala unafiki.


Mtu atakayekuwa tayari kupambana na udokozi unaofanywa na baadhi ya wawekezaji uchwara wanaosifika kwa kuhamisha raslimali za nchi bila kubughudhiwa, mtu atakayekuwa tayari kuhakikisha raslimali za nchi zinatumika kwa maslahi ya wote sio wachache kama ilivyo hivi sasa.
CCM wanatakiwa kuangalia na kupima nchi iko wapi na inaelekea wapi katika kipindi cha zaidi ya nusu karne ya uhuru. Ni lazima chama hiki kikakumbuka ya kuwa Watanzania katika zama hizi chama sio kipaumbele katika chaguzi bali mtu husika.
Watanzania wameamka, wameamka katika usingizi wa fikra za chama waliokuwa wameulala kwa muda mrefu, wanahitaji mageuzi ya kweli, mageuzi ambayo iwapo hawatoyapata ndani ya chama basi watayafuata nje ya chama.

 
1519 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!