Hii ni sehemu ya maoni ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Tundu Lissu kuhusu Mpango wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013. Endelea

 

Katika maoni yetu kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilionyesha jinsi ambavyo “tafsiri hii mpya ya Makubaliano ya Muungano na Katiba ya Jamhuri ya Muungano imetiliwa nguvu kubwa na Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo imeipa Zanzibar nafasi na ushawishi mkubwa katika utungaji wa Katiba Mpya.”

 

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilionyesha kwamba, kwa mujibu wa Sheria hiyo, “Rais wa Zanzibar siyo tu kwamba ana mamlaka karibu sawa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, bali pia ana kura ya turufu katika mchakato mzima wa Katiba Mpya.”

 

Aidha, tulithibitisha jinsi ambavyo “… ushawishi mkubwa wa Zanzibar hauishii katika kura ya turufu aliyo nayo Rais wa Zanzibar pekee yake (bali) Zanzibar ina ushawishi mkubwa vile vile kutokana na nafasi kubwa iliyo nayo katika vyombo vingine vinavyoundwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba….”

 

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia tena tahadhari iliyoitoa wakati huo kwamba: “Masharti haya ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yana athari kubwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu yanakiuka Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano na hata Katiba ya sasa ya Zanzibar ….” Na kama tulivyosema wakati huo, “… tafsiri hii mpya ya Makubaliano ya Muungano na ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inarudisha mezani mjadala juu ya muundo wa Muungano wetu na nafasi ya iliyokuwa Tanganyika katika Muungano huo.”

 

Kama ilivyo kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba katika mazingira ambayo upande mmoja wa Muungano umejitangazia uhuru kama ambavyo tumeonyesha hapa, huu ni wakati muafaka kuanzishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika .

 

Katika mazingira ambayo upande mmoja wa Muungano siyo tu una Serikali kamili, Bunge kamili, Mahakama kamili, wimbo wa taifa, bendera ya taifa, na sasa una nchi kamili yenye mipaka na eneo la bahari linalojulikana, una majeshi yake na Amiri Jeshi Mkuu wake, huu ni muda mzuri kwa Serikali ya Tanganyika kuzaliwa upya.

 

Katika mazingira kama haya, Mheshimiwa Spika, upande wa pili wa Muungano unatakiwa kuwa na vitu vyote hivyo pia ili uweze kujadiliana na upande wa kwanza katika hali ya usawa.

 

Huu ni wakati wa kurudishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika kama ilivyopendekezwa na Tume ya Rais ya Chama Kimoja au Vyama vingi mwaka 1991 na Tume ya Kissanga mwaka 1998, na kama ilivyopendekezwa na Kundi la Wabunge 55 wa Bunge hili tukufu na kuungwa mkono na Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi kabla ya hoja hiyo kutunguliwa na Baba wa Taifa mwaka 1993!

 

KURA YA MAONI JUU YA MUUNGANO

 

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaielekeza Tume ya Katiba kuongozwa na misingi mikuu ya kitaifa ya kuhifadhi na kudumisha ‘kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano.’ Hata hivyo, baada ya kujitokeza kwa wananchi wanaopinga kuendelea kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba amesema kwamba wale wanaopinga Muungano nao wajitokeze kutoa maoni yao kwa Tume. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu ni namna gani maoni ya wale wanaotaka kiini macho hiki cha Muungano kiishe yatashughulikiwa na Tume ambayo imepewa jukumu kisheria la kukihifadhi na kukidumisha kiini macho hicho? Ni kipi kitakachoizuia Tume ya Warioba kupuuza maoni ya watu hao kwa hoja kwamba Sheria inaielekeza Tume kuratibu na kukusanya maoni na kutoa mapendekezo ya kuhifadhi na kudumisha Muungano?

 

Katika miezi ya karibuni kumejitokeza makundi ya wananchi, hasa kwa upande wa Zanzibar , ambayo yamedai kwamba iitishwe kura ya maoni ya wananchi ili kuamua kama bado kuna haja ya kuendelea na Muungano. Makundi haya, yakiongozwa na kundi la Uamsho, yameshambuliwa sana hadharani kwa kudaiwa kwamba yanataka kuvunja Muungano. Na watu ambao wameongoza mashambulizi dhidi ya wana-Uamsho ni viongozi waandamizi wa CCM, wakiwamo viongozi wakuu wastaafu wa chama hicho.

 

Katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tulisema kwamba “… hofu … ya kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ndiyo imesababisha kimya kikuu – ndani ya CCM na ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano – juu ya ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano uliofanywa na Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar, 2010.” Naomba nikiri kwamba tulikosea kusema hivyo.

 

Tulichotakiwa kusema wakati ule, na tunachokisema sasa, ni kwamba kimya kikuu ndani ya CCM na ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya ukiukwaji mkubwa wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano pamoja na Katiba kinatokana siyo tu na ‘hofu’ ya kuwaudhi Wazanzibari, bali pia kinatokana na ukweli kwamba viongozi waandamizi wa CCM pamoja na wa Serikali yake walishiriki katika ukiukwaji huo! Wao ndiyo wanaoongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ndiyo walioandaa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar .

 

Na wao ndiyo wanaoongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano waliokula kiapo cha kuihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Na kwa hiyo wao ndiyo walioiruhusu Zanzibar kutangaza uhuru kwa Mabadiliko haya ya Katiba yake.

 

Kwa viongozi hawa na chama chao kuibuka sasa na kuwatuhumu wana-Uamsho na makundi mengine kwamba wanataka kuvunja Muungano kwa kudai kura ya maoni ya wananchi wakati wao wenyewe wamekaa na kupitisha marekebisho ya Katiba ambayo tayari yamevunja Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano ni kilele cha juu cha unafiki wa kisiasa.

 

Mashabiki hawa wa Muungano waeleze walikuwa wapi wakati Zanzibar inatangaza uhuru wake kwa kuchanachana Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano.

 

Kwa wale wanaodai kwamba wana-Uamsho wanataka kuvunja Muungano kwa sababu tu ya kudai kura ya maoni, tunaomba tuwakumbushe yafuatayo.

 

Kwanza, kwa mujibu wa Baba wa Taifa katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania : “Huko nyuma baadhi ya viongozi wa Zanzibar wapinzani wa Muungano wamewahi kudai tufanye referendum kwa Zanzibar kuhusu Muungano.

 

Tukakataa kwa sababu safi kabisa.” Hapa Mwalimu alikuwa anamzungumzia aliyekuwa Rais wa Zanzibar Alhaj Aboud Jumbe, Waziri Kiongozi Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Bashir Ebassuah Kwaw Swanzy waliong’olewa madarakani mwaka 1984 baada ya ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa.’

 

Aidha, Mheshimiwa Spika, katika kitabu hicho hicho Mwalimu Nyerere anasema yafuatayo juu ya kilichotokea kwenye Bunge hili hili wakati wa Bunge la bajeti la mwaka 1993: “Tarehe 30 Julai, 1993 wakati wa mkutano wa Bunge la bajeti ukiendelea, zaidi ya wabunge 50 kwa pamoja walitoa taarifa ya kusudio la kuwasilisha hoja bungeni ambayo inadai (kwamba) kuendelea na mfumo huu wa Muungano usiowaridhisha wananchi wengi wa upande mmoja ni kuhatarisha kuendelea kudumu kwa Muungano…. Hivyo basi, wabunge hawa wanaliomba Bunge … liazimie kwamba Serikali … ilete muswada bungeni kabla ya Februari 1994, kurekebisha katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kuwezesha uundaji wa ‘Serikali ya Tanganyika ’ ndani ya Muungano…. Tarehe 20 Agosti, 1993 wabunge wahusika waliwasilisha taarifa nyingine … iliyokuwa inalitaka Bunge … liazimie kwamba Serikali … iandae kura ya maoni ambayo itafanyika kabla ya 31 Desemba, 1994 ili kupata maoni ya wananchi wa Tanzania juu ya kuundwa kwa “Serikali ya Tanganyika ” ndani ya Muundo wa Muungano….”

 

Pili, Katiba ya sasa ya Zanzibar ambayo mashabiki wa Muungano wameileta kwa kupitia Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba tayari imewapa wananchi wa Zanzibar haki ya kuamua, kwa kura ya maoni, mambo mbalimbali yanayoihusu nchi hiyo na namna itakavyoongozwa.

 

Mashabiki hawa wa Muungano wakubali kuvuna walichopanda, wasibeze wale wote wanaotaka kutumia haki ya kura ya maoni kuamua hatma ya Muungano na nafasi ya Zanzibar ndani au nje yake.

 

Ni wazi, kwa kuzingatia ushahidi huu, kwamba madai ya kuwa na kura ya maoni ya wananchi ili kuamua masuala makubwa yanayohusu Muungano wetu ni ya siku nyingi na yametolewa na watu na taasisi mbalimbali.

 

Madai haya hayajaanzishwa na wana-Uamsho wala CHADEMA. Ni wazi vile vile kwamba kura ya maoni inaruhusiwa kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar .

 

Kwa sababu hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaungana na wale wote ambao wamedai, na wanaendelea kudai kuitishwa kura ya maoni ya wananchi ili waweze kuamua mustakbala wa nchi yetu.

 

Kuendelea na kiini macho cha Muungano wakati Serikali zote mbili na chama tawala cha CCM wanauvunja kivitendo kutaipeleka nchi yetu kwenye njia ya Ethiopia na Eritrea , au Sudan na Sudan Kusini au Yugoslavia ya zamani.

 

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Watanzania waamue, kwa kura ya maoni, kama bado wanataka kuendelea na Muungano na kama jibu lao ni “ndiyo”, ni muundo gani wa Muungano wanautaka.

 

Kama, kwa busara zao, wataamua kwamba nusu karne ya Muungano inatosha, basi itakuwa afadhali kwenda njia ya Czechoslovakia ya zamani kuliko kwenda njia ya Yugoslavia ya zamani, au Ethiopia na Eritrea au Sudan na Sudan Kusini.

 

Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwaeleze Watanzania juu ya hatua, kama zipo, ilizozichukua kuzuia ukiukwaji huu wa Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba. Na mwisho, Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu kama – kwa ukiukwaji huu wa Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano – Bunge hili tukufu litakuwa ndani ya mamlaka yake kuchukua hatua za kumshtaki Rais kwa mujibu wa ibara ya 46A ya Katiba kwa kushindwa kuihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Muungano kama kiapo cha kazi yake kinavyomtaka.

  

1314 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!