DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi

Mataifa mbalimbali duniani yamo kwenye vita kali dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 unaotokana na virusi vya corona tangu kugundulika kwa ugonjwa huo wa homa kali ya mapafu katika Jiji la Wuhan, China, Desemba 2019.

 Ugonjwa huo ulianza kusambaa kwa kasi katika mataifa mbalimbali duniani yakiwamo mataifa ya Afrika. Baada ya mwezi mmoja ugonjwa huo uliripotiwa kuingia Afrika huku tahadhari dhidi ya ugonjwa huo zikionekana kusuasua kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ugonjwa huo unawaathiri zaidi watu weupe.

Baada ya ugonjwa huo kusambaa na kushamiri Afrika tofauti na matarajio ya wengi, madhara yake kwa afya, uchumi na maisha ya kijamii yamekuwa na funzo muhimu.

 Pamoja na vita hii kuonekana kupiganwa kwa mbinu na silaha tofauti kwa kila bara na kila taifa kutegemeana na mazingira na uwezo wa kiuchumi wa mataifa husika, changamoto kubwa inayozikumba nchi nyingi za Afrika ni uchumi tegemezi na sekta ya afya kutopewa kipaumbele vya kutosha katika bara hili.

Katika mapambano dhidi ya COVID-19 wimbi la kwanza na la pili baadhi ya nchi za Afrika zilijaribu kuwafungia wananchi ndani (lockdown) huku nyingine zikitumia tiba za asili.

Afrika baada ya kufanikiwa kwenye vita ya ukombozi wa kisiasa na kijamii bado kuna tatizo katika ukombozi wa kiuchumi pamoja na kuwa na utajiri wa rasilimali ikilinganishwa na mataifa mengine duniani.

Katika mapambano dhidi ya COVID-19 nchi nyingi zimedhihirisha wazi kuwa Afrika imeshindwa kutumia nguvu yake pekee inayoweza kuipa nafasi katika uamuzi wa utekelezaji wa majukumu yake katika kuwahudumia wananchi wake. 

Kama alivyowahi kuonya na kushauri Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuhusu Afrika kutoungana, akiwa Accra, Ghana kwenye maadhimisho ya miaka 40 ya uhuru wa taifa hilo Machi 6, 1997. 

Alisema baada ya kufanikiwa kujikomboa, sasa Afrika ina mataifa 53 (54 baada ya Sudan Kusini kuongezeka mwaka 2011) huru. Mataifa 21 zaidi ya yale yaliyokutana Addis Ababa Mei 1963, wakati Kwame Nkrumah alipotaka iundwe serikali moja ya Afrika.

Kama idadi ingekuwa na uwezo, Afrika leo ingekuwa juu sana; ingekuwa ni bara lenye nguvu kuliko yote duniani, kwa sababu ina viti vingi kwenye Umoja wa Mataifa kuliko bara  jingine lolote.

Lakini ukweli ni kwamba bara letu ndilo maskini na dhaifu zaidi duniani. Na udhaifu wetu unatia huruma. Umoja hauwezi kumaliza udhaifu wetu lakini mpaka tutakapoungana, hatuwezi hata kuanza kukomesha udhaifu wetu.

Huu ni wito wangu kizazi kipya cha viongozi wa Afrika na watu wa Afrika fanyeni kazi pamoja kwa dhamira ya dhati kwamba bila umoja Afrika haina mustakabali mwema. 

Hata hivyo, ni kama bado tunahitaji kuwa na sehemu yetu chini ya jua, alieleza Mwalimu Nyerere.

Katika wimbi la kwanza la COVID-19 nchi nyingi za Afrika zilikuwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya kupimia virusi vya corona, wataalamu na taasisi nyingi za afya Afrika zimekuwa na mashine za kupima wagonjwa wa corona, hali iliyoleta taharuki katika baadhi ya nchi.

Mei mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli, alibainisha kuwa kuna shaka kwenye vipimo vinavyotumika kupimia virusi vya corona baada ya kupima sampuli za papai na mbuzi kubainika kuwa na maambukizi ya virusi hivyo.

Baada ya kauli hiyo, Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa barani Afrika, John Mkengason, alikanusha taarifa hizo na kueleza imani yake kwa vifaa hivyo vinavyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kwa upande wake Mkuu wa WHO Afrika, Matshidiso Moeti, aliwaambia waandishi wa habari kwamba: “Tuna uhakika vifaa vya upimaji corona vilivyonunuliwa kupitia WHO na vilivyotoka Jack Ma Foundation havikuwa na maambukizi ya virusi.”

Bila shaka msigano huo usingetokea kama kungekuwa na taasisi imara ambayo ipo kwa  masilahi mapana ya Afrika, badala ya kila upande kutetea nafasi yake na wananchi kuachwa njia panda.

Katika harakati za mapambano dhidi ya COVID-19 mataifa yaliyoendelea yamefanikiwa kupata chanjo ya ugonjwa huo na kushauri mataifa ya Afrika kutumia chanjo hiyo, hali iliyoleta wasiwasi na hofu kwa baadhi ya nchi za Afrika.

Baadhi ya nchi za Afrika zimetilia shaka chanjo hiyo na kutaka kufanyiwa utafiti wa kina na wataalamu wa ndani kabla ya kuanza kutumika kwa wananchi. Na wengine kushauri kujengwa viwanda vya chanjo ya corona katika nchi za Afrika.

Hatua ambayo bado inakumbana na changamoto nyingi kutokana na dawa hizo kuchukua muda mrefu katika tafiti za kisayansi.

Mwaka jana nchi 40 za Afrika zilishiriki mafunzo yaliyotolewa na WHO kuhusu ujenzi wa viwanda vya kutengeneza chanjo ya corona  katika mataifa mbalimbali duniani ikiwamo Afrika.

Nchi zote 54 za Afrika zimekubali azimio la hivi karibuni la Ethiopia kuhusu Mkutano Mkuu wa 74 wa afya duniani kuhusu viwanda vya dawa vya ndani na teknolojia mpya ya afya ili kuongeza nguvu katika mapambano ya magonjwa mbalimbali tishio ikiwamo COVID-19.

Pamoja na makubaliano  hayo, hatua za utengenezaji chanjo zinaelezwa kuchukua muda wa miaka mitano hadi 10 ikiwa ni sambamba na utafiti, kliniki za majaribio, wanyama wa majaribio na leseni za viwanda za chanjo hizo.

Afrika yenye idadi ya watu bilioni 1.2 ina uwezo wa kutoa chanjo kwa asilimia moja katika chanjo zinazotolewa duniani. Hii ni kwa mujibu wa WHO.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi mpya wa IMF, Kristalina Georgieva, amezitaka nchi tajiri duniani kusaidia mataifa maskini ya Afrika katika mapambano dhidi ya corona.

“Huu ni wakati muhimu sana kwa nchi za G20 kuchukua hatua madhubuti pamoja na watengeneza sera duniani kote kusaidia nchi maskini za Afrika,” amesema  Georgieva.

Januari 27, mwaka huu, Dk. Magufuli aliwataka Watanzania kuwa makini wanapoamua kufuata chanjo ya corona nje ya nchi, akiwahimiza Watanzania kuchukua tahadhari na kumuomba Mungu.

Kama hiyo haitoshi, Aprili 6, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, aliunda kamati maalumu ya kufanya tathmini ya hali ya ugonjwa wa corona nchini na kutoa ushauri wa kitaalamu wa namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Mei 17, mwaka huu, kamati hiyo chini ya Mwenyekiti Profesa Said Aboud, ilikabidhi ripoti ikipendekeza njia ya kupata unafuu kama serikali itajiunga na mpango wa chanjo wa ‘facility’ kwa kuwasilisha andiko la kupatiwa chanjo.

Juni mwaka huu Rais Samia alisema Tanzania iliandaa andiko kwa ajili ya kuomba chanjo za ugonjwa wa COVID-19 kupitia mpango wa chanjo wa Covax Facility.

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa na idadi ya vifo vinavyotokana na corona hapa nchini, hatimaye Tanzania imepokea awamu ya kwanza ya msaada wa dozi 1,058,400 za chanjo dhidi ya virusi vya corona, huku Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, akiwahakikishia Watanzania kuwa chanjo hiyo ni salama kwa ajili ya matumizi.

Katika hatua nyingine, Julai 28 Rais Samia alizindua chanjo rasmi  na kuwashauri Watanzania kupata chanjo hiyo, kwa kuwa imethibitishwa na wataalamu wa Afya.

“Nimechanjwa na nimeingia katika ‘database’ (kanzidata) ya dunia kwamba nimechanjwa,” amesema Rais Samia.

Dk. Hassan Sembogo wa Morogoro anasema wimbi la tatu la COVID-19 ni hatari sana ikilinganishwa na wimbi la kwanza na la pili, hivyo jamii inapaswa kuchukua tahadhari kubwa na kufika hospitalini mara kwa mara kupima afya.

“Sisi wataalamu wa Afya tumeendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaofika kwa matibabu hapa hospitalini na tunashukuru mwitikio wa wananchi ni mzuri na wengi wanachukua tahadhari,” anasema Dk. Sembogo.

0755985966

By Jamhuri