Zabikha lawamani ada darasa la saba 

DAR ES SALAAM

Na Aziza Nangwa

Baadhi ya wazazi wenye watoto wa darasa la saba katika shule binafsi kadhaa wamelalamika kulipishwa ada kinyume cha mapatano.

Wazazi wanalalamika kutozwa ada kubwa huku wakilazimishwa kumaliza malipo sawa na ya mwaka mzima kwa wanafunzi wanaotarajiwa kumaliza shule Septemba mwaka huu, wakiwa wamesoma mihula mitatu tu. 

Bakari Hamidu ambaye mtoto wake anasoma Shule ya Msingi Zabikha, ameliambia JAMHURI kuwa kwa miaka saba aliyosoma shuleni hapo hakukuwa na matatizo katika kulipa ada.

“Nilikuwa mlipaji mzuri wa ada lakini mwaka huu mtoto alipoingia darasa la saba, uongozi wa shule ukatushangaza wazazi kwa kututaka tulipe fedha zote kabla ya Julai.

“Mwongozo tuliokuwa nao tangu awali ni kulipa kwa awamu nne. Sasa kwa darasa la saba, hilo limebadilika bila kuzingatia kipato cha watu kuwa kinatofautiana. Hawaelewi!” anasema Hamidu.

Anasema maelekezo ya uongozi wa Zabikha kutaka ada yote kwa muda mfupi yalimchanganya kutokana na udogo wa kipato chake.

Bahati nzuri Mungu akamsaidia, akapata fedha lakini akapungukiwa Sh 50,000 na kumpeleka shule mwanaye.

“Hakupokewa! Mwalimu akasema hadi ada yote iwe imekamilika. Inasikitisha na kukera sana. Mtoto nimemsomesha hapa miaka saba leo ninaonekana si mwaminifu?

“Na hiki ni kilio cha wazazi wengi. Kwamba watoto wakifika darasa la saba, walimu wanabadilika na kukiuka utaratibu tuliokubaliana.

“Unaambiwa kama hautaki nenda na mwanao hatafanya mtihani wa taifa,” anasema Hamidu.

Mzazi mwingine wa mtoto wa darasa la saba katika shule nyingine binafsi iliyopo Mbezi Luis, anakubaliana na hoja ya Hamidu, akisema shule hiyo imehakikisha wazazi wanalipa ada ya mwaka mzima kwa watoto wa darasa la saba.

“Ni kama uhuni tu. Mtoto anasoma miezi tisa, unapigiwa hesabu za uongo na kweli ili ulipe ada ya mwaka mzima na ukipungukiwa hata Sh 10,000 mtoto haingii kwenye geti la shule,” anasema mzazi huyo.

Anaiomba serikali kuangalia kwa undani kama shule hizo zinafuata miongozo ya elimu inayotolewa na wizara husika akiamini kuwapo ukiukwaji wa aina fulani wa haki ama za wanafunzi au walezi wao. 

Mwalimu Mkuu wa Zabhika, Adamu Ibrahim, anasema wazazi wenye watoto shuleni hapo hupewa sheria na miongozo kabla ya kufanya usajili.

“Mlezi anaamua mwenyewe kwa kuwa hii ni biashara. Ni kweli kabisa, inawezekana kuna watoto waliorudishwa nyumbani kutokana na kutotimiza ada. Sikatai. 

“Wahudumu waliowapokea walikuwa wanafuata sheria. Shule yetu kama kuna mtoto hajamaliza ada bila taarifa, tutamrudisha nyumbani kwa sababu ndio utaratibu tuliojiwekea,” anasema Mwalimu Ibrahim.

Kuhusu wazazi kulalamika kulipishwa ada ya mwaka mzima wakati watoto wanasoma miezi tisa, anasema: 

“Si kweli kwa sababu shule inafuata mitaala na miongozo yote kutoka serikalini. Kuna kufidia kwani darasa la saba huanza masomo Desemba na hawana likizo hadi mtihani wa mwisho. Fedha inayolipwa hufidia miezi hiyo.

“Hebu rejea katika mwongozo wa serikali kipindi cha ugonjwa wa corona (mwaka jana). Watoto waliporejea shuleni walisema hata kama wamekaa nyumbani, watatakiwa kulipa ada ya mwaka mzima kufidia siku za masomo.”

Anasema wasichojua wazazi ni kwamba shule binafsi hufanya biashara tofauti na za serikali, kwa hiyo hutakiwa kulipa kulingana na shule inavyotaka.

“Kama hawezi kulipa kutokana na changamoto za maisha, atoe taarifa kwa barua kabla ya kumleta mtoto ili akija asibugudhiwe. Sivyo, amhamishe shule, japokuwa hatushauri hivyo,” anasema mwalimu huyo.

Anasema shule hiyo ni ya watu wema, hawawezi kumbugudhi mzazi kwani wanjali utu.

“Hawa ni wateja wetu ndiyo maana hata ikitokea mzazi amefariki dunia na alikuwa anamsomesha mtoto kwetu, tunamchukua mtoto na kumsomesha bure hadi amalize masomo.

“Kila mwaka shule tunakwenda vituo vya watoto yatima kuchukua baadhi yao na kuja kuwasomesha bure, si kazi ndogo! Kila mwaka!

“Kwa hiyo tunajali sana watoto wasome na si kuhama kwani kuna baadhi ya wazazi hawana shida ila wana tabia ya kuhamishahamisha tu shule watoto kukwepa ada. Akiona anadaiwa, anahama mpaka mwaka unakwisha,” anasema Mwalimu Ibrahim.

Mwongozo wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia unazitaka shule binafsi nchini kuwapokea wanafunzi wote na kuwaruhusu kuendelea na masomo pasipo ubaguzi wowote.

Agizo hilo limetolewa kufuatia kuwapo malalamiko kutoka kwa baadhi ya wazazi juu ya ongezeko la ada linalofanywa na baadhi ya shule kwa kigezo cha janga la corona.

Taarifa iliyotolewa na kusainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo, Sylvia Lupembe, imewataka wazazi pamoja na uongozi wa shule husika kuheshimu makubaliano ya ulipaji ada yaliyokuwapo hapo awali kabla ya janga la corona na kuzingatia pia mwongozo uliotolewa na wizara mara baada ya Rais Magufuli kutangaza kuwa shule zote nchini zifunguliwe ifikapo Juni 29, mwaka huu.

Taarifa hiyo ya wizara inasema haitakuwa busara kwa shule kutoza gharama ya usafiri iliyokuwa ilipwe wakati shule zimefungwa na badala yake watoze gharama kama vile ankara za maji, umeme pamoja na mishahara ya walimu na watumishi wengine, gharama ambazo kimsingi hazikusimama wakati wa janga la corona.

Aidha, taarifa hiyo imewataka wazazi nao kuwa waungwana kwa kuhakikisha wanalipa ada na gharama zote stahiki kwa wakati ili kuziwezesha shule nazo kuendelea kutoa elimu pasipo kikwazo chochote.