Na Joe Beda Rupia

Gesi ya kupikia imepanda bei. Hili unaweza kudhani ni suala dogo tu. Lakini kwa hakika lina ukubwa wake na limenifikirisha sana.

Sisi ambao wazazi wetu ni wazee na sasa wanaishi peke yao vijijini, tukaamua kuwapunguzia ‘msalaba’ wa kutumia kuni na mkaa wakati wa kupika.

Naam! Wazee hawa wameitumia nishati hii kwa muda mrefu sana hadi sasa sisi tunazeeka, kwanini waendelee kuhangaika nayo uzeeni?

Tukadhani kwa kuwanunulia gesi ya kupikia tutawasaidia sana. Ni kweli. Walifurahi na wanaendelea kufurahi hata leo.

Bahati mbaya sasa hali inakuwa mbaya huku Dar es Salaam. Gesi imepanda bei. Maana yake hadi Mpanda itapanda bei. 

Mbaya zaidi tozo ya uzalendo haina dalili ya kuondolewa. Tunayo. Tutaishi nayo. Tuizoee. Maana yake hata fedha ya kununulia gesi mama akiishiwa kule nyumbani Makanyagio, Mpanda, itabidi nijibane sana kuituma kwa kuwa gesi imepanda bei, na tozo inaongeza gharama.

Kwa hakika kifo tu ndio ukomo wa kuchacharika na maisha. Dar es Salaam tunachacharika, Mpanda wazee wetu bado wanachacharika hata kama ni kwa kusubiri kununuliwa gesi na kutumiwa fedha zenye tozo ya kizalendo.

Vyote hivi vinanipigia kengele kunieleza kuwa muda na maandalizi ya kina ndilo jawabu la kustaafu vizuri. Sidhani kama nipo sahihi kwa asilimia 100! Si rahisi.

Mipango mizuri inaingiliwa na maisha (gesi imepanda, tozo la kizalendo) mwishowe kuna hatari ya kustaafu kwa huzuni! 

Uzoefu unaonyesha kuwa watu wengi wanapostaafu badala ya kufurahia kwenda kupumzika, husikitika.

Ipo haja ya kuandaa tabasamu la kustaafu ukiwa bado kazini na kama ninavyoandika mara kwa mara, siri ipo katika kuanza kujiwekezea sasa. 

Siku ya kwanza ya ajira inapaswa kuwa ya kwanza kujiandaa kwa kuwekeza kwa ajili ya siku za baada ukomo wa ajira. 

Kuchelewa kuanza kuwekeza ni kupishana na faida jumuishi zinazopatikana kwenye mifuko ya UTT AMIS; eneo ambalo nina uzoefu nalo kuliko biashara nyingine.

Kuna msomaji mmoja alinipigia simu akidai kuwa mfumo wa uwekezaji ninaoupigia debe ni wa watu wenye kipato kikubwa pekee.

Hii inatokana na mifano inayotolewa kuhusisha fedha nyingi sana. Ukiambiwa kuwekeza kiwango cha awali cha Sh milioni 5 na kuendelea kuongeza Sh 200,000 kila mwezi kwa miaka 10 utakuwa na Sh milioni 29 kutegemea makubaliano ya riba, kulimkwaza msomaji wangu.

Nikalazimika kumwelekeza kwa wataalamu ambao wamemwelewesha namna ambavyo hata mtu wa kipato cha kawaida anavyoweza kunufaika.

Ninatumaini ameelewa na tayari amejiunga nasi kwa kuwa maisha ni mapambano na kifo tu ndiyo suluhu ya mapambano haya. 

Naam! Maajabu kwa mfanyakazi wa kada ya kati au ya chini kujikuta akiwa na mamilioni baada ya miaka 20 ya kazi; mbali na fedha za NSSF au PSSSF, yanastahili muda kuyatafakari lakini yanawezekana. Muhimu tu ni kukaa na wataalamu. 

Wakati maishani tunapambana na misukosuko ya kupanda kwa bei ya bidhaa, kama nilivyoanza kwa kuelezea gesi ya kupikia, katika uwekezaji kwa malengo ya baadaye nako kuna kupanda na kushuka kwa thamani ya hisa au kipande chako.

Ni tabia ya uwekezaji wowote, hata ungekuwa na duka au genge kuna siku unapata zaidi na siku nyingine unapata kidogo katika eneo lako hilo hilo hata kama umeongeza mtaji!

Wataalamu wanasema wakati wa kustaafu ni wakati wa kuziba nyufa za nyumba uliyojenga; si wakati wa kujenga nyumba!

Inakuwaje kwa ambao hatukuweza kujenga tukiwa kazini kwa sababu mbalimbali? Basi, sisi sasa tusijenge nyumba za kifahari (ghorofa) baada ya ukomo wa ajira.

Kanyumba kadogo na kazuri katika eneo stahiki kwa ‘mzee’ kanatosha kukufariji baada ya hekaheka za maisha na huku ukimudu gharama za kukatunza. 

Majumba makubwa wakati mwingine hugeuka mizigo baada ya kustaafu. Kumbuka kuhudumia jumba kubwa ni gharama! Umeme, maji, ulinzi na hakuna unaoishi nao maana familia imeshapungua! Hatari.

Lazima nyumba itunzwe huku gharamu muhimu kama matibabu, zikiendelea kama kawaida. Badala ya kusubiri muamala usome kutoka kwa wanao ili ununue gesi, jiandae kuwa na uwezo wa kununua gesi inapokwisha, na wala kabia kamoja jioni za wikiendi jamani!

Huo sasa unakuwa ndio uzee wenye raha mustarehe! Hii yote ni kama umefanikiwa kujiwekea akiba ya kutosha.

Usipokuwa na akiba ya namna hiyo ni majuto, kwani hata baadhi ya vitu vya gharama ambavyo umekuwa ukivimiliki kwa miaka, hugeuka kuwa visivyo na maana tena baada ya kustaafu.

Wakati wa ajira kuna vitu vyake. Je, utapaswa kuwa navyo baadaye? Kama hapana, achana navyo sasa na badala yake kiasi ambacho kingetumika kuvinunua, kiwekezwe, kitengwe kwa baadaye. 

Madeni nayo ni shughuli nyingine, madeni yakiwa mengi na makubwa yanatoa tafsri ya uchache wa akiba au uwekezaji kwa ajili ya kustaafu. 

Usipoangalia utaingia kwenye kustaafu na madeni mengi, huu ni mzigo tena mkubwa ambao utaubeba huku nguvu zikiwa zinafifia.

Watoa ushauri mara kwa mara wanataka kila mmoja awe na bajeti inayoeleweka. Siyo ukiulizwa hivi mwaka jana ulipata na kutumia kiasi gani cha fedha, unabaki mdomo wazi.

Zaka kanisani au msikitini haujatoa wala wazee wako haujawanunulia gesi na hata akiba yako mwenyewe haujaweka; vipi wewe?

Bajeti ni pamoja na kuchagua nini kifanyike na kipi kisifanyike kwa wakati husika na hapo katika kujiwekea akiba ni muhimu kupunguza uwezekano wa kupata hasara kwa kila namna.

Tawanya uwekezaji wako kwa kuchagua maeneo yenye unafuu wa kodi kama katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

Ukiweka kwenye mfuko mmoja uliouchagua unakuwa kama umewekeza sehemu nyingi. Bila wewe kutambua, tayari unakuwa umewekeza kwenye hisa za kampuni mbalimbali, kwenye hati fungani za serikali na hata benki!

Kifo hakiepukiki na kama mwenza wako ndiye alikuwa kichwa, fahamu anaweza kutangulia mbele ya haki kabla yako. Ni muhimu kujiandaa kwa mshituko kama huo, kwani mengi hubadilika.

Ada ulikuwa hauna habari nazo, sasa ni juu yako; kodi mbalimbali, ni wewe; chakula pia unatafuta mwenyewe. 

 Uwe kazini au umestaafu, bima ya afya ni kitu muhimu sana na kuna kila sababu ya kutenga fedha kwa ajili ya bima hii, kwani ni vigumu kulipa gharama za matibabu kutoka mfukoni mwako hasa kwa magonjwa kadhaa makubwa.

Mjadala wa fao la kujitoa NSSF au PSSSF huwa ni mgumu sana, wengi wakitaka kuchukua fedha mara wanapoacha kazi. Huo ni uchoyo na ukosefu wa upendo.

Washauri siku zote wanasema ni vizuri kuchukua kiunua mgongo ukifika wakati wa kustaafu kwa sababu watu wengi hatuna mipango mizuri ya fedha.

Wengi si wafanyabiashara au wawekezaji stadi. Hivyo basi ni vizuri kusubiri fainali uzeeni.

Kama nilivyosema, kuchacharika kunaisha pale tu Mungu atakapoichukua roho yako. Kwa hiyo hata baada ya kustaafu, unapaswa kuwa na shughuli nyingine ya kufanya. Maisha ni mapambano! 

Anzisha jambo jipya kupata uzoefu tofauti na muhimu ni kuwa makini usipoteze mtaji ulionao.

Nimewahi kusema neno ‘kustaafu’ ni tatizo kubwa. Tubadili na kuacha kulitumikia mara moja. Badala yake tusema kuanza maisha mapya kwa kuendeleza yale ambayo tumeshaanza au kubuni mapya.

Ukistaafu sema; kazi iendelee! Kisha rejea kwenye akiba ulizowekeza UTT AMIS, na uanze maisha mapya, kwani huko utakuwa ukipewa mafao kadiri ya mfuko uliojichagulia. Pesa zako zinaendelea kukufanyia kazi!

Tumia uzee wako kujifunza mambo mengine darasani kwa kuwa elimu haina mwisho. Pesa zipo kwenye mfuko salama, una hofu gani?

Kuna mstaafu mmoja wa ualimu mjini Moshi sasa hivi ana kitalu cha maua kinachomwingizia fedha nyingi hata kuliko alizokuwa akipata kazini.

Mbali na kipato, amekuwa mwenye furaha huku akiupa mwili mazoezi ya kutosha kila siku.

Hakuna tafsiri kamili kuhusu uzee, wengine kuanzia miaka 40 tu wanaitwa wazee! Uzee ni umri usio na mpaka, tutakapoanza kusema ‘sasa basi tumezeeka’ inaweza kuwa chanzo cha matatizo ya ufukara na kukosa furaha. Mwisho wa kuchacharika uwe ni kifo chako.

By Jamhuri