Mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, jana aliwaita waandishi wa habari na kuwapa takwimu za ushindi anaodai kuupata kwenye Uchaguzi Mkuu.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa Hamad anaongoza dhidi ya mpinzani wake mkuu, Rais Dk. Ali Mohamed Shein wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Baada ya taarifa hiyo, wananchi wa Zanzibar ambao ni wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) cha Hamad, waliingia mitaani kushangilia. Hatua hiyo iliwalazimu polisi kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya.

Kisheria, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ndiyo yenye mamlaka kisheria ya kumtangaza mshindi. Tulidhani viongozi na wafuasi wa vyama vya CCM na CUF wangekuwa na subira ili Tume iweze kutekeleza wajibu wake wa kisheria.

Kwa hali ya mambo ilivyo ni kwamba endapo hatua za dharura hazitachukuliwa, Zanzibar inaweza kujikuta kwenye machafuko mengine na kuharibu ladha ya amani ambayo imeshuhudiwa kwa kiwango cha juu wakati wote wa Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania.

Tunawasihi viongozi na wananchi katika Visiwa vya Zanzibar kutulia na kuwa tayari kuyapokea matokeo; lengo kuu likiwa kuendelea kuitunza amani ambayo tayari ilishaonekana kustawi.

Wakati tukiyasema hayo kwa upande wa Zanzibar, hatuna budi pia kuwakumbusha viongozi na wafuasi wa vyama vya siasa upande wa Tanzania Bara nao kuendelea kuyapokea matokeo kwa njia ya amani na utulivu. Kumekuwa na matukio ya kusuasua kutangaza washindi kwenye nafasi za udiwani na ubunge; jambo ambalo linachochea hisia mbaya miongoni mwa wapigakura.

Wasimamizi wa uchaguzi hawana sababu za kuchelewesha kutangaza matokeo hasa pale wanapokuwa wameshajiridhisha na hatua zote zinazotakiwa kabla ya kuyatangaza. Mizengwe na urasimu ni mambo yanayoweza kuleta malalamiko na hatimaye uvunjifu wa amani.

Kwa ujumla tunawapongeza wananchi wote wa Tanzania walioshiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani na kwa utulivu. Tunaomba waendelee na staha hiyo hiyo wakati huu wa kuyasubiri matokeo ya mwisho.

Kama tulivyoomba wiki moja iliyopita kwenye safu hii, Watanzania wamethibitisha kuwa ni wamoja na wanaweza kupita kwenye mitihani migumu bila misuguano. 

Jumuiya ya kimataifa ilidhani Watanzania wangeweza kupigana, hata ikafikia hatua ya kuwaonya wageni kutokuja nchini kwa hofu ya kuzuka kwa vurugu. Watanzania wameonesha ukomavu kwa kumaliza shughuli ya Uchaguzi Mkuu kwa amani. 

Tunaomba hatua hiyo hiyo iendelee wakati huu wa kupokea matokeo ya mwisho kwa Zanzibar na kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

1220 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!