Tanzania, Tanzania, Nakupenda kwa moyo wote,

Nchi yangu Tanzania, Jina lako ni tamu sana,

Nilalapo nakuota wewe, Niamkapo ni heri mama wee,

Tanzania, Tanzania, Nakupenda kwa moyo wote.

Tanzania, Tanzania, Ninapokwenda safarini,

Kutazama maajabu, Biashara nayo makazi,

Sitaweza kusahau mimi, mambo mema ya kwetu kabisa,

Tanzania, Tanzania, Nakupenda kwa moyo wote.

 

Tanzania, Tanzania, Watu wengi wanakusifu,

Siasa yako na desturi, Ilikuletea uhuru,

Hatuwezi kusahau sisi, Mambo mema ya kwetu hakika,

Tanzania, Tanzania, Nakupenda kwa moyo wote

 

Huu ni wimbo wa uzalendo wa wananchi wa Tanzania. Kila Mtanzania mpenda amani ana wajibu wa kuuimba na kuzingatia maudhui yaliyomo.

Tumejaliwa amani, utulivu na mshikamano. Mwaka huu wa 2015, hasa mwezi huu, walimwengu wanaimulika Tanzania kuona kama ile sifa yetu njema duniani kote, ya amani na utulivu-itaendelea kuvuma.

Tupo kwenye kipindi muhimu cha kuuthibitishia ulimwengu kuwa pamoja na uchanga wetu kama Taifa, bado tuko imara katika kuulinda umoja na mshikamano wetu.

Taifa letu linaingia kwenye Uchaguzi Mkuu unaotajwa kuwa wenye msisimko usiokuwa wa kawaida tangu kurejeshwa kwa mfumo wa siasa ya vyama vingi nchini mwetu mwaka 1992.

Tayari jumuiya ya kimataifa imeshakaa mkao wa kuona nini kitatokea Tanzania kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu. Mashirika ya kimataifa yameshatoa hadhari kwa watumishi wake waliopo nchini mwetu. Balozi mbalimbali, hasa za Ulaya zimefanya hivyo.

Kwao, Tanzania haina tofauti na mataifa mengine ya Afrika yaliyotopea kwenye vurugu na uvunjifu wa amani.

Sasa Watanzania tuna kazi moja. Kazi iliyo mbele yetu ni kuwasuta wale wote wanaojitahidi kuleta uchuro wakiamini kuwa Watanzania tunaweza kufarakana kutokana na tofauti zetu za kiitikadi. Tusiruhusu mwanya wowote wa kuwafanya walimwengu watuweke kwenye kundi la mataifa yaliyofeli.

Tuuthibitishie ulimwengu kuwa matunda ya amani, umoja na mshikamano tuliyoachiwa na waasisi wetu tukingali nayo, na kwamba tutayalinda milele kwa nguvu na hekima zote alizotujalia Mwenyezi Mungu.

Lakini ili hayo yafanikiwe, vyombo vya usimamizi na utoaji haki havina budi kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa kila upande. Ni muhimu kutambua kuwa bila haki, hakuna amani.

Wananchi wote tuna wajibu wa kuhubiri amani na kuisimamia kwa vitendo. Yeyote awaye, awe mmoja mmoja au kundi la watu; anayethubutu kuleta vurugu au kuwagawa Watanzania, tuna wajibu wa kuungana pamoja kumkataa kwa vitendo.

Watanzania wote tuweke nadhili ya kuiona Tanzania ikiendelea kuwa moja na Watanzania wakiwa wamoja kabla na hata baada ya Uchaguzi Mkuu.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

1557 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!