Watanzania na walimwengu wiki hii wanafanya kumbukizi ya miaka 16 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Ni muda mrefu tangu alipofariki dunia, lakini bado wapenda amani na maendeleo wanaendelea kumkumbuka na kumuenzi.

Kumbukizi ya mwaka huu, kama ilivyokuwa ile ya miaka ya 2000, 2005 na mwaka 2010 ni ya kipekee. Huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu wa nne Tanzania ikiwa haina Mwalimu.

Ingawa ni miaka 16 sasa, ukweli ni kwamba bado Mwalimu Nyerere anaendelea kuishi miongoni mwa Watanzania, Waafrika na walimwengu wengi.

Hotuba pamoja na maandishi yake, ni vitu vinavyomfanya Mwalimu aendelee kuwa hai miongoni mwa wanadamu wengi, hasa wapenda amani na maendeleo.

Wakati wa uhai wake Mwalimu kama kiongozi shupavu, aliainisha mambo mengi na ya msingi aliyoyatumia kama dira ya kuijenga Tanzania, Afrika na dunia yenye usawa.

Bado Watanzania wanakumbuka namna alivyosimama imara kutetea mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa mwaka 1992 licha ya maoni ya wananchi zaidi ya asilimia 80 kupendekeza mfumo wa chama kimoja. Mwalimu alitetea mfumo wa vyama vingi kwa kuamini kuwa hilo lilikuwa hitaji muhimu la kijamii katika ulimwengu tulionao.

Katika kipindi chote cha maisha yake, Mwalimu hakuchoka kusisitiza masuala ya amani, usawa na maendeleo. Kwa namna ya pekee, bila kujali umaskini wa nchi na wananchi wake, alituongoza kwenye mapambano ya ukombozi wa nchi zilizokuwa zikitawaliwa kwa mabavu. Aliamini Uhuru wa Tanzania usingekuwa na maana kama mataifa mengine ya Afrika yangekuwa yakiendelea kukandamizwa na wakoloni.

Moyo huo wa upendo wa Mwalimu umeleta neema kubwa kwa mataifa ya Msumbiji, Angola, Zimbabwe, Namibia, Afrika Kusini na kadhalika. Duniani kote Mwalimu alikuwa alama ya mtetezi mkuu wa wanyonge. Ndiyo maana haishangazi kuona hata Palestina, jina la Mwalimu lipo hadi kwenye mitaa.

Watanzania wanajivunia mambo mengi mazuri waliyoyapata kutoka kwa Mwalimu. Umoja, mshikamano na upendo miongoni mwao si mambo yaliyokuja yenyewe, isipokuwa yamewezekana chini ya uongozi wake na waasisi wengine kama Mzee Abeid Amani Karume.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unachukuliwa na walimwengu kama kilelezo halisi cha namna Watanzania wanavyomuenzi Mwalimu. Ili kuendelea kuilinda sifa hii njema, Watanzania, kila mmoja kwa nafasi yake, tuna wajibu wa kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unakuwa huru, wa haki na unatawaliwa na amani. Hiyo ndiyo njia nzuri ya kwanza kabisa ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Yeyote anayehubiri vurugu miongoni mwa wananchi, hasa wakati huu na baada ya Uchaguzi Mkuu, kila Mtanzania mpenda amani na maendeleo ana haki na wajibu wa kumsema, na ikibidi kumuumbua. Uchaguzi huu uwe wa kumuenzi Mwalimu.

 

MUNGU MPUMZISHE KWA AMANI MTUMISHI WAKO JULIUS KAMBARAGE NYERERE

By Jamhuri