Wiki iliyopita, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliandaa mikutano mbalimbali na wadau wake wakiwamo wamiliki wa vyombo vya habari na wahariri.

Katika mikutano hiyo, mengi yamezungumzwa lakini kubwa ni kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini kuagizwa kufuata maadili ya taaluma sambamba na sheria za uchaguzi, ili kuepuka kupitisha habari kutoka vyanzo visivyo rasmi.

Mwenyekiti wa Tume, Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu, Damian Lubuva, amewaambia wahariri kwamba wana dhamana kubwa ya amani ya Tanzania sasa, wakati wa Uchaguzi Mkuu na baada ya mchakato huo.

Katika wito wake, Jaji Lubuva anasema, “Ndugu zangu, muda uliobaki kuelekea Uchaguzi Mkuu ni mfupi mno. Dhamana ya amani ipo kwenu na kwetu.”

Sisi tunakubaliana na Jaji Lubuva juu ya kudumisha amani katika nchi kwa sababu uchaguzi ambao mwenyekiti huyo anauongoza ni wa kupita tu na kwamba Tanzania na wananchi watabaki palepale.

Kwa kumnukuu, Jaji Lubuva anasema: “Hatuna budi kuitikia wito wa kukwepa kuandika habari za upendeleo na kuwa “uandishi wa namna hii hauusaidii umma.”

Lakini pia tunaungana na Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri, Neville Meena, ambaye naye pia aliomba Tume ifanye kazi kwa karibu ili kuepuka hayo aliyoyasema.

Hakuna ubishi kwamba hiki ni kipindi cha mawimbi mazito ya kisiasa na siasa za Tanzania zimebadilika sana. Tufanye kazi kwa ushirikiano kama alivyosema Mhariri huyo Mtendaji wa Kampuni ya Free Media inayochapisha magazeti ya Tanzania Daima na Sayari.

Kwa mazingira ya sasa, tunaamini kwamba uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti na miaka 20 iliyopita kwa kuwa umejaa ushindani wa hali ya juu na tunasema ni bora NEC wamekutana na wadau kuweka mambo sawasawa.

Tunachoweza kusema ni kwamba hakuna sababu ya kushutumiana baina ya wadau, badala yake tushirikiane.

Ni vyema wananchi wakafahamishwa kuwa baada ya kumaliza kupiga kura kituo hicho kinabadilika na kuwa kituo cha kujumlishia kura, na mawakala wote wa vyama wanasaini fomu ya matokeo na baadaye yanabandikwa kituoni.

Hivyo, hakuna haja ya wananchi kubaki vituoni baada ya kupiga kura na badala yake warudi nyumbani kusubiri matokeo kupitia vyombo vya habari.

Tunatoa wito kwa wagombea wa vyama vyote vya siasa kunadi sera zao jukwaani na iwapo wameishiwa na sera wakae kimya kusubiri siku ya kupiga kura badala ya kutoa lugha za kejeli, kukashifiana na matusi pamoja kukoma kuhamasisha wananchi kulinda kura zao.

2070 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!