Jumamosi ya Agosti 29, mwaka huu Gazeti la JAMHURI lilifanya mahojiano na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Damian Lubuva aliyezungumzia mambo mbalimbali likiwamo la namna ya kuhesabu kura.

Mahojiano hayo yalizaa habari ndefu tuliyoichapisha Septemba mosi, mwaka huu na msomi huyo anayetumia hekima na busara kutoa haki kwa watu na mali zao, alitamka kwa mara kwanza kwamba kura zote zitahesabiwa vituoni na matokeo kubandikwa.

Jaji Lubuva alikuwa anajibu swali kwamba kuna dhana kwamba kura za urais zingekusanywa tu vituoni na kupelekwa kwa mkurugenzi ama wa manispaa au halmshauri ya mji kwenda kuhesabiwa.

Jambo hilo lilianza kulalamikiwa na baadhi ya vyama vya siasa hususani vile vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Lakini Jaji Lubuva alielezea jambo hili vema kama alivyofanya wiki iliyopita alipozungumza na viongozi wa dini jijini Dar es Salaam, akisema kitakachofanyika kwenye vituo hivyo ni kuhesabu na kubandikwa vituoni.

Akaongeza kusema utangazaji wa matokeo utafanyika kama kawaida katika kila ngazi, udiwani kwenye kata, ubunge wilayani na urais Tume makao makuu ambako kwa mujibu wa sheria ni yeye.

Lengo la Lubuva ambaye leo tunamsifu kuongeza uwazi na kupunguza malalamiko ya wizi wa kura kama ambavyo vyama vya ushindani (upinzani) vilianza kupiga yowe.

Jaji Lubuva pia alipata kueleza haya kwenye magazeti akisema, “Hakuna haja ya kuwa na shaka wala kuandaa vijana wa kulinda vituo. Hakutakuwa na nafasi hiyo kwa sababu kura zote zitahesabiwa na kubandikwa huko.”

Ukweli ni kwamba hii itakuwa ni tofauti na zamani ambapo zilikuwa zinasafirishwa na kuhesabiwa wilayani ambako watu wengine walidhani yanabadilishwa hivyo kuzusha hofu.

Sisi JAMHURI tunachukua nafasi hii kumpongeza Jaji Lubuva kwa kufanya kazi zake kwa weledi na kisasa. Amekuwa mwepesi kusikiliza maoni ya upande mwingine na kushauri.

Mara nyingi amekuwa akihasa vyombo vya habari kuandika habari za ukweli badala ya kuchochea watu wanaoweza kutuondolea tunu ya amani hasa wakati huu nchi inakwenda kufanya mabadiliko ya uongozi wa juu katika utawala.

Bila shaka umri, uzoefu wa kazi na kushika nyadhifa kadhaa kubwa, zimemsukuma Jaji Lubuva kutangaza hayo ambayo tathmini inaonyesha kwamba wananchi wameipokea kauli yake kwa mikono miwili.

Kwa uwazi anaoutangaza Jaji Lubuva ni imani yetu kuwa itaondoa dhana ya upendeleo kwa chama fulani au mtu katika Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Kuonyesha kwamba Lubuva ametosha katika nafasi yake, mara kwa mara amekuwa akiwaasa wanasiasa, wagombea, wafuasi na wanaowanadi kuacha lugha za matusi, vitisho, kejeli na kukashifiana ili kuepuka kuchochea fujo na uvunjifu wa amani badala yake wajikite katika kunadi sera za vyama vyao.

By Jamhuri