Amani iendelee kutamalaki Uchaguzi Mkuu

Tumeanza wiki ya pili ya kampeni za Uchaguzi Mkuu. Tunawapongeza Watanzania kwa kuvuka wiki ya kwanza tukiwa na kampeni zilizotawaliwa zaidi na hoja badala ya vurugu.

Wajibu wetu kama vyombo vya habari ni kuendelea kulisisitiza suala la amani kwa kipindi chote cha kampeni na hata baada ya kutangazwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu.

Pamoja na hali kuendelea kuwa nzuri, zipo dalili za hapa na pale kutoka kwa baadhi ya wanasiasa kuanza kujisahau na kuyageuza majukwaa ya kampeni kuwa ya mipasho, vijembe na kashfa.

Tayari mwelekeo wa haya umeanza kuonekana. Vyama vyenye wagombea urais, hasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema wanaowakilisha Ukawa, wameshaanza kurushiana maneno ambayo kwa mtazamo wa wengi si mazuri, na kwa kweli yanapaswa kuepukwa.

Tunaendelea kuwasisitiza wagombea na wanasiasa wote kujikita zaidi katika kuelezea sera za vyama vyao ili Watanzania wawe kwenye hatua nzuri ya kuamua kuchagua viongozi kadri ya utashi wao.

Kauli za vitisho za kwamba akichaguliwe yule au asipochaguliw yule amani itatoweka, tunaamini hazifai hata kidogo.

Watanzania kwa umoja wetu ni watu wanaopendana baada ya kuishi pamoja kwa miaka mingi bila kujali tofauti zetu za kiitikadi, dini, rangi, kabila, jinsi, hali au namna nyingine yoyote.

Mifarakano katika mataifa mengi imesababishwa na wanasiasa kwa uchu wao wa madaraka. Hili tunaliona sasa katika Sudan Kusini. Hatutaki tufike huko; na kwa pamoja Watanzania tuwe radhi kusimama kidete kuwapinga wote wanaothubutu kuhubiri shari.

Tumeona namna maelfu kwa maelfu walivyoshiriki mikutano ya uzinduzi wa kampeni za CCM pale Jangwani, na pia tumeshuhudia maelfu ya watu walivyoshiriki mkutano wa aina hiyo wa vyama vinavyounda Ukawa. Jambo la faraja ni kuona kuwa wananchi wamekuwa wakienda kushiriki mikutano hiyo wakiwa wenye furaha na hakuna mahali ambako kumeripotiwa matukio ya uvunjifu wa amani.

Baada ya mikutano kumalizika, wananchi hao walirejea makwao wakiwa katika makundi na huko walikopita hawakuanzisha vurugu kwa namna yoyote ile.

Aina hii ya staha na uvumilivu miongoni mwa wafuasi wa vyama inapaswa kwenda hadi kwa viongozi na wagombea wa nafasi mbalimbali za kisiasa katika Uchaguzi Mkuu.

Mara zote tumesema tuna wajibu wa kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kuendelea kuidumisha amani yetu ambayo ni matunda tuliyoachiwa na wasasisi wa Taifa letu. Tunatoa wito kwa wananchi wote kutokubali kujengewa uhasama kwa misingi ya kiitikadi, hasa wakati huu ambao joto la kisiasa liko juu.

Kampeni na uchaguzi ulio huru na wa amani ndiyo nguzo muhimu ya kuiona Tanzania mpya ambayo wengi wanataka kuiona chini ya uongozi ujao wa Awamu ya Tano.

Mungu Ibariki Tanzania.