Vyama vya siasa vilivyokamilisha vigezo vilivyowe kwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kupata kibali rasmi cha kuanza kampeni za kunadi sera za vyama vyao ili kuwashawishi wapiga kura kuwachagua viongozi na vyama wavipendavyo katika uchaguzi mkuu unaotajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu visijikite kueneza chuki na kutafuta kuwagawa watanzania.

Kuthubutu kunadi matusi, kejeli, kashfa, ubabe na kuzua kila namna ya ghasia kama njia ya kukubalika na wananchi ambao ndio waajiri wa viongozi hao ni kuwakatisha tamaa na kusababisha baadhi yao kushindwa kuitumia haki yao ya msingi ya kupiga kura.

katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 2010 wagombea waliweza kujinadi kwa sera za vyama vyao bila kuruhusu ndimi zao kunadi matusi, japo baadhi yao kwa uchache wao na kutojifunza kuishi maisha ya kistaarabu kwa kukosa hoja za msingi walitumia lugha chafu kama mtaji wao wa kisiasa.

Ni wazi kwamba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kumejitokeza mwamko mkubwa wa kisiasa kwa wananchi kwa kufuatilia kwa ukaribu sera pamoja na mitazamo na mapendekezo ya wagombea na vyama vyao, na kuwapima kama wanaweza kutekeleza ahadi zao kwa manufaa na maendeleo yao na taifa zima kwa ujumla wake.

Katika uchaguzi wa mwaka huu wagombea wa nafasi tatu za urais, ubunge na udiwani watakuwa na fursa ya kuuza sera, miongozo na dira za vyama vyao kwa wapiga kura ambazo zitapimwa na wananchi kama zinafaa kuwatoa hapa walipokwama katika lindi la umaskini kwa zaidi ya nusu karne sasa.

Kama waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao watakuwa na majibu sahihi mbele ya wapiga kura kwa kueleza bila ubabaishaji ni kwa nini nchi yetu bado ni maskini pamoja na kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali ambazo zinawanufaisha wageni na atafanya nini kuondoa utata huo? Hapa tunachotaka ni majibu ya hoja badala ya kuanza kuporomosha matusi.

Tunataka mgombea aeleze kinagaubaga kama ndio anawania kwa mara nyingine nafasi ya ubunge au udiwani kwa nini alishindwa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi na apimwe kwa kazi yake aliyofanya katika vipindi vilivyopita badala kutoa kejeli na vijembe ambavyo havitawasaidia watanzania wanaoendelea kuwa maskini huku watu wachache wakijinufaisha kwa kutumia mtaji wa rushwa, ufukara na ujinga wa watanzania walio wengi.

Wakati huu ni muhimu sana kwa mustakabali wa taifa hili kutokana na ukweli kuwa viongozi bora watakaochaguliwa kidemokrasia, watakuwa dira ya kusogeza mbele maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wake.

Tunasema kuwa kipindi hiki cha kampeni, kinakuwa na msisimko wa pekee kwa wengi kutokana na mwamko wa kisiasa ulivyo miongoni mwa wananchi wengi hata hivyo tunachotarajia kampeni ambazo zitahusu masuala ya kijamii zaidi, hatutarajii kusikia wagombea wakishambuliana na kuchafuana wao kwa wao kwa masuala binafsi ambayo hayana msingi kwa watanzania wanaomtaka mtu atakayewatoa katika kadhia hii ya umaskini.

1375 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!