Katika Gazeti letu la JAMHURI, toleo la wiki iliyopita na wiki hii tumeripoti kwa kina habari ya uchunguzi kuhusu mwekezaji wa kampuni ya utafutaji wa mafuta na gesi, kusini mwa Ziwa Tanganyika, kutoa chanjo kwa wafanyakazi wake isiyotumika nchini.
Chanjo hiyo ya Typhoid ilitolewa na Kampuni ya Beach Petroleum  inayomilikiwa na mwekezaji kutoka nchini Australia kwa nyakati tofauti Novemba na Desemba 2014, kwa wafanyakazi wake waliopo mikoa ya Rukwa na Kigoma.
Kabla ya kutolewa kwa chanjo hiyo na uongozi wa Beach Petroleum, wafanyakazi walipewa vitisho vya kufukuzwa kazi  iwapo wangekataa kupewa chanjo hiyo. Kwa hofu ya kufukuzwa kazi walilazimika kukubali kupewa chanjo.
Baada ya kushindwa kuhimili vitisho vya mwekezaji huyo, Watanzania hao, Novemba 18, 2014 walianza kupewa chanjo hiyo iliyotolewa bila kibali cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), pia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC ) na taasisi nyingine muhimu za Serikali nazo hazifahamu kinachoendelea.
James na mkewe, Katherine Ann (raia wa kigeni), walianza kutoa chanjo kwa wafanyakazi 39 wa kampuni ya BGP ya Wachina katika mikoa ya Rukwa na Katavi na baada ya miezi miwili wafanyakazi 190 walikuwa tayari wameshapewa chanjo na kuanza kupata madhara ya kiafya kutokana na chanjo hiyo.
Pamoja na mwekezaji huyo kutoa chanjo hiyo, baadhi ya watendaji wa Wizara ya Afya, wanaeleza kushtushwa na chanjo hiyo iliyotolewa bila kuhusishwa wizara hiyo.
Sisi JAMHURI tunasema kwamba kama Watanzania tumefikishwa hapa na kudharaulika kwa kiasi hiki na watu wa mataifa mengine wanaopewa majina ya wawekezaji ambao wako tayari kufanya lolote watakalo ndani ya nchi yetu hii, haikubaliki kabisa.
Hali hii imechangiwa kwa kiwango kikubwa na udhaifu wa Serikali yetu ambayo imeamua kujivunia umaskini na wakati mwingine kutembeza kopo la ombaomba tu hata kwa mambo mengine ambayo Watanzania wenyewe tunaweza kuyafanya.
Mgeni anaweza kufanya lolote atakalo ndani ya Tanzania. Ni ruhusa kuvunja sheria na kufanya jambo lolote lile bila hata kuihusisha Serikali, kama uhuni huu uliofanywa na mwekezaji huyu aliyeamua kutoa chanjo kwa Watanzania ambayo haitumiki nchini kwa zaidi ya miaka minane.
Tumewaacha viongozi, mawakala wa wanyonyaji na ambao kwa makusudi wameamua kuudhalilisha utu wa Watanzania kwa kuwaacha wageni kufanya watakalo hata ikibidi Watanzania wafe kwa sababu hakuna anayejali.
Jambo la kujiuliza; ni raia yupi wa Tanzania anayevunja sheria anapokuwa ndani ya nchi nyingine bila kuchukuliwa hatua za kisheria? Tusikubali kugeuzwa shamba la bibi na kijiji cha wagonjwa wa akili na kuchezewa na kila mnyonyaji anayekaribishwa kwa kivuli cha uwekezaji wa namna hii.

 

 
2549 Total Views 4 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!