Mchuano wa kuwania uwakilishi wa kwenye uchaguzi wa rais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) unazidi kushika kasi.
Wagombea zaidi ya 30; kila mmoja anajitahidi kutumia mbinu, ama halali, au haramu, kutafuta kuungwa mkono.


Kwenye mpambano huu kumeonekana mambo ambayo tunaamini tunapaswa kuwa sehemu ya wanaoyapinga.
Baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya jamii vimechapisha picha zisizofaa za Makongoro Nyerere. Kwa maelezo yaliyopo ni kwamba picha hizo zimeandaliwa mahsusi kwa ajili ya kumpunguza kasi ya kukubalika kwake miongoni mwa wana CCM na Watanzania.
Hatujakabidhiwa dhima ya kumtetea Makongoro wala mgombea yeyote awaye, lakini tumeshawishika kulisema tukio hili kwa sababu linaelekea kwenda nje ya mada halisi ya kugombea urais.


Kuna habari kwamba wapo vijana maalum waliopewa kazi ya kutengeneza picha chafu za aina hiyo kwa malipo mazuri na kuzisambaza kwenye mitandao.
Mbinu hiyo ndiyo inayotutia shaka kwa sababu kama kila mgombea ataamua kutumia muda na fedha kuwachafua wagombea wenzake kwa namna hiyo, waathiriwa watakuwa ni wana CCM na Watanzania wenye kiu ya kupata viongozi wanaowataka.
Itakumbukwa kuwa mchezo huu mbaya ulishafanywa hadi kwa kiongozi mkuu wa nchi, yaani Rais Jakaya Kikwete; katika hatua ambayo ilionekana kuvuka mipaka.


Aidha, Mbunge wa Arusha Mjini naye yameshampata ya aina hiyo. Walioumizwa ni wengi. Hata kama mambo haya yanakuwa ni ya kutungwa kwa kutumia teknolojia hii ya kisasa, bado yamekuwa na athari kwa walengwa na watu walio karibu nao. Yamewaumiza wengi kisaikolojia.
Imani yetu ni kwamba wagombea wote bado hawajaishiwa hoja za kuwashawishi wajumbe au wanachama wenzao kuweza kuwakubali.


Bado wana hazina kubwa ya hoja ambazo kama watatumia muda wao mrefu kusiwasilisha kwa wanaowapitisha, ni wazi kwamba watapata fursa ya kusonga mbele.
Siasa za kistaarabu zina manufaa makubwa kwa wagombea wenyewe na kwa ustawi wa nchi yetu. Tukianza kukubaliana na utamaduni huu wa kusambaza picha chafu za kutungwa, maana yake ni kuwa endapo mpango huo utafeli, zitatumika mbinu nyingine mbaya.
Mbinu hizo si nyingine, isipokuwa ni za kufanya ushawishi kwa misingi ya kidini, kikanda, kikabila, kijinsi, kihali au rangi. Wote wanaotumia mbinu chafu za aina hiyo ni wanasiasa mufilisi.


Tunaomba tukio hili alilofanyiwa Makongoro Nyerere liwe la mwisho kwa wagombea waliokwishaonyesha nia ya kuwania urais. Pia lisifanywe kwa wagombea wa ngazi zote zinazoshindaniwa. Staha ni silaha muhimu itakayolinda na kudumisha heshima ya Tanzania na Watanzania.

 
2619 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!