Ujanja ujanja kwenye mfumo wa mishahara ya watumishi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) ya jijini Arusha, unatajwa kuwa chanzo cha Serikali kupoteza fedha nyingi.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa mfumo wa ‘Lawson’ unaotumika kuandaa mishahara, umeingizwa taarifa potofu zinazosababisha upotevu wa fedha na watumishi kadhaa kupandishwa ngazi tatu za mishahara kwa mwaka mmoja, jambo ambalo si la kawaida.

“Mfumo huu hufanya kazi vizuri pale unapokuwa umepewa data sahihi; unapolishwa data potofu katika hatua ya awali na ikazikubali, huendelea nazo.

“Mbinu hii imetumika kinyume cha kanuni, miongozo na sheria za utumishi wa umma, ili kikundi kidogo cha wafanyakazi wanaotetea maslahi binafsi ya mkuu wa taasisi wapate mishahara mikubwa wasiyostahili,” kimesema chanzo chetu.

Waraka wa Serikali Na. CAC.45/257/01/E/83 unataka mtumishi atumikie si chini ya miaka mitatu, kwa wale walio katika utumishi wa umma; au miaka minne, kwa wale ambao itawapasa wapitie kipindi cha majaribio kwa wale ambao hawajawahi kuwa katika utumishi wa umma.

Kifungu cha 22 cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003 kinataka kuwe na tathmini ya utendaji ya mfanyakazi ya miaka mitatu mfululizo inayompa sifa za kupanda ngazi.

Lakini pia inatakiwa kuwe na kibali cha upandishaji cheo kutoka mamlaka ya juu kwa mujibu wa Kifungu cha 5-12 cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka huo.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kukiukwa kwa kanuni hizo kwa kuwapa mishahara mikubwa baadhi ya watumishi katika chuo hicho.

Mathalani, imebainika kuwa mtumishi mmoja (jina tunalihifadhi kwa sasa) ambaye ni Mkaguzi wa Ndani Mwandamizi aliandika barua ya maombi ya kazi mwaka 2010, kutokana na tangazo lililotoka kwenye Gazeti la Daily News la Mei 3, 2010 nafasi ya Mkaguzi wa Ndani. Februari 11, 2011 alikubali ajira na kuingia kwa mara ya kwanza katika utumishi wa umma kama Mkaguzi Mwandamizi II, ngazi ya PGSS 15-16 kwa mshahara Sh 1,399,100 kwa mwezi. Hii ilitokana na ofa ya ajira aliyopewa kwa barua ya Desemba 12, 2010 iliyosainiwa na Profesa Dubi.

Mwaka 2012 akawa PGSS 16 kwa mshahara wa Sh 1,539,000.  Mwaka 2013 akawa Mkaguzi wa Ndani Mwandamizi I kwa ngazi ya mshahara ya PGSS 18/1. Kuanzi mwaka 2014 amekuwa akilipwa kwa ngazi ya PGSS 18/3 ikionesha kuwa kwa mwaka mmoja amepanda ngazi tatu na kulipwa mshahara wa Sh 2,962,000 kwa mwezi.

“Ameruka ngazi nyingi, jambo ambalo katika Lawson isingekuwa hivyo kwa sababu isingekubali,” kimesema chanzo chetu. Inakisiwa kuwa tangu mtumishi huyo aajiriwe hadi mwanzoni mwa mwaka huu, ameingizia hasara Sh milioni 68.

“Mbali na wizi wa fedha za umma, udanganyifu huu unazalisha maafisa wa ngazi za juu wasiokuwa na uzoefu, ujuzi na uwezo sahihi wa kufanya kazi, vitu ambavyo angevipata kama angepanda ngazi hatua kwa hatua.

“Baraza la Uongozi la Chuo na Kamati ya Ajira na Maendeleo ya Watumishi walipewa taarifa, hawakubariki wizi huo. Mkuu wa chuo hajataka kurekebisha na kuwapa mshahara wanaoustahili,” uchunguzi umebaini.

Mtumishi mwingine ambaye naye JAMHURI inahifadhi jina lake kwa sasa kwa kuwa hajapatikana kuzungumza, aliandika barua Mei 6, 2010 akiomba nafasi ya Ofisa Rasilimali Watu. Alikubali ofa Januari 2, 2011 kwa nafasi hiyo daraja la kwanza kwa ngazi ya PGSS 13-14 ambayo mshahara wake ulikuwa Sh 1,023,100. Ofa yake ilipitia barua ya Desemba 12, 2010 iliyosainiwa na Profesa Dubi. Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa ajira hii ilikuwa ya kwanza kwake katika utumishi wa umma.

Miezi sita baadaye, yaani Juni 3, 2011, kinyume cha sheria na kanuni, akaruka hadi kufika ngazi ya PGSS 15-16 ya mshahara wa Sh 1,230,100.

Miezi michache baadaye akapanda ngazi na kuwa PGSS 15 kwa mshahara wa Sh 1,353,100; ikiwa ni kwa mujibu wa hati ya malipo ya mshahara ya Februari 2012.

Ilipofika mwaka 2013 akapewa SHRO – 1 kwa ngazi ya PGSS 17/3 na hivyo kumfanya akunje kitita cha mshahara cha Sh 2,352,000. Katika malipo ya mwaka 2014 amekuwa katika ngazi ya PGSS 17/3 Senior HRMO – I akilipwa mshahara wa Sh 2,586,000 kwa mwezi.

Uchunguzi unaonesha kuwa mtumishi huyo, kama asingepandishwa ngazi na mishara kwa kasi hiyo, Serikali ingeliokoa Sh 44,384,400.

Idadi ya watumishi katika idara hizo na nyingine wanaolipwa kwa mtindo huo ni wengi mno, na JAMHURI itachapisha majina yao watakapokuwa wameulizwa.

 

Ajira kwa wageni

Imebainika kuwapo kwa idadi ya raia wa kigeni wanaolipwa na chuo wakiwa hawafanyi kazi katika taasisi hiyo.

Miongoni mwao amebainika kuwa ni Profesa Morris Agaba. Kulingana na hundi namba 110560924; PUTS.6.1, amekuwa akilipwa Sh 5,470,000. Analipwa mshahara na Serikali ya Tanzania, amepewa nyumba ilhali aliondoka muda mrefu na akaajiriwa na taasisi ya utafiti ya BecA – ILRI ya Kenya.

“Mkuu wa taasisi kaisababishia Serikali hasara ya shilingi zaidi ya 65,640,000 kwa mwaka, mbali ya gharama ya nyumba aliyokuwa anatumia kipindi chote hicho.

“Kwa muda mrefu ameendelea kuwalipa mshahara raia wa Ethiopia – Profesa Amare Gessesse hundi Na. 110780003, PUTS 5.1, Sh 5,045,000 kwa mwezi (malipo ya mwaka 2014);  na Dk. Tileye Feyisa, Sh 4,755,000 kwa mwezi.

“Waliondoka nchini kwa kutopewa kibali na Uhamiaji na kufanya kazi nchini, alishauriwa katika Baraza la Chuo mishahara yao isitishwe, akakataa.

“Hazina waangalie hawa watu waliendelea kulipwa hadi lini. Serikali imepata hasara ya Sh 60,540,000 kwa mwaka kupitia kwa Amare Gessessa na Sh 57,060,000 kwa mwaka kupitia kwa Tileye Feyisa. Tileye ndiyo kwanza amerudi nchi kufanya kazi,” kimesema chanzo chetu.

Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Burton Mwamila, anatetea ajira za wageni hao na kusema wengine walishaondoka.

Katika majibu yake kwa JAMHURI anasema: “Profesa Amare na Dkt. Tileye waliondoka nchini Desemba 2014 na malipo yalisimamishwa mara tu ilipoonekana kuwa mikataba yao ya ajira na vibali vya makazi vingechelewa kutolewa na Serikali.

“Dkt. Tileye sasa amerudi baada ya kukamilika mikataba ya ajira na vibali vya makazi kutolewa na Serikali. Prof. Amare bado hajarudi kwa vile taratibu hazijakamilika. Si kweli kwamba Tileye aliendelea kulipwa mshahara wakati hakuwa nchini.”

Pia taasisi ilimwajiri raia wa Marekani, Revocatus Kalege, kama Meneja Majengo kwa ngazi ya PGSS 21 ya mshahara wa Sh 3,400,000 mwaka 2013.

Baadaye ilibainika kuwa Kalege ana uraia wa Marekani na Tanzania na ana hati mbili za kusafiria za mataifa hayo. Kwa muda alioajiriwa, Kelege alilipwa Sh milioni 142.8

Profesa Mwamila anajibu: “Wakati Revocatus Kalege anaomba kazi hapa chuoni alitoa taarifa ya kwamba yeye ni raia wa Tanzania, na alionesha paspoti ya kusafiria ya Tanzania.

“Chuo kilimwajiri Revocatus Kalege kwa kuzingatia taarifa alizozitoa kwetu zikionesha kuwa yeye ni Mtanzania. Hadi wakati wa kumaliza mkataba wa utumishi wake katika chuo hiki, mamlaka za chuo hazikuwa zinafahamu kwamba Kalege si raia wa Tanzania. Aidha, chuo kilipata taarifa juu ya uraia wake wa Marekani kupitia mamlaka nyingine za Serikali ikiwamo Mahakama, miezi mitatu baada ya kumaliza mkataba wa kazi na Taasisi ya Nelson Mandela.”

Raia wa Kenya, Calorine Ndemaki, naye aliajiriwa kwa ngazi ya PUSS 7.8 kwa mshahara wa Sh 3,530,000 kwa mwezi kwa mujibu wa nyaraka za malipo za mwaka 2014.

Ameajiriwa kama Ofisa Mkutubi Mwandamizi; kazi ambazo baadhi ya watumishi katika chuo hicho wanasema zingeweza kufanywa na Watanzania.

Profesa Mwamila anatetea ajira ya Mkenya huyo kwa kusema: “Ajira ya Caroline Ndemaki ilifanywa kwa mujibu wa taratibu za ajira katika Utumishi wa Umma nchini Tanzania.

“Aidha, wakati nafasi ya ukutubi ilipotangazwa, hakujitokeza mtaalamu wa Kitanzania aliyekuwa na sifa ambazo zilikuwa zinahitajika kwa nafasi ile na ambaye angeiwezesha Taasisi ya NM-AIST kuanzisha maktaba yenye ubora wa kimataifa na yenye viwango vinavyohitajika kwa ajili ya ufundishaji na

ujifunzaji, utafiti na ubunifu katika sayansi, uhandisi na teknolojia.

“Kibali cha ajira ya Ndemaki kilitolewa na Serikali kwa mujibu wa taratibu za ajira za watumishi wanaotoka nje ya nchi hususani Afrika Mashariki.

“Aidha, uongozi wa chuo unamwandaa mrithi wa nafasi ya Caroline, Neema Mosha, ambaye anategemewa kumaliza masomo ya Shahada ya Uzamivu Oktoba 2017 katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini.”

Mwingine aliyeajiriwa ni Dkt. Anael Sam kwa ngazi ya PUTS 7/1 ya mshahara wa Sh 4,009,000 kwa mwezi kwa hati ya malipo ya mwaka 2013 akiwa kama Mhadhiri Mwandamizi.

Katika mlolongo huo, imebainika kuwapo kwa baadhi ya watumishi walioajiriwa bila kibali cha ajira kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma; na wengine bila kufanyiwa usaili.

Baadhi ya watumishi ambao ajira zao zitatajwa kuwamo kwenye kundi la kuchunguzwa ni Eva Grace Maro aliyeajiriwa mwaka 2012 na Happy Mtungakoa.

“Mkuu wa chuo aseme ni lini tangazo la ajira lilitolewa, walifanyiwa usaili lini na nani waliohusika. Yupo aliyeajiriwa bila usaili lakini kwenye makaratasi inaonekana alipata alama 87, ajibu ni lini alifanyiwa usaili? Mbona taarifa zilizopo zinaonesha siku inayodaiwa kuwa alifanyiwa usaili, yeye alikuwa amelazwa hospitalini?

“Haki ya Watanzania walioomba kazi, wakawa ‘shortlisted’ wakasafiri kutoka mikoa mbalimbali hadi Arusha, wakafanya usaili awamu ya kwanza kwa maandishi (mtihani), wakachujwa, wangine wakaingia hatua ya pili na kufanya usaili wa mdomo – ana kwa ana – haki yao imekwenda wapi?” Kimehoji chanzo chetu cha habari.

Kwenye orodha hiyo, yumo Ofisa Mkuu wa Mawasiliano (jina tunalihifadhi) ambaye naye inadaiwa ameajiriwa bila kuwapo kibali kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Wengine ni Wakutubi Wasaidizi II (2), na Msaidizi wa Makamu Mkuu wa Chuo, na Mtaalamu wa Tehama walioajiriwa bila kibali kutoka Ofisi ya Rais. Majina yao tunayahifadhi kwa sasa.

 

>>INAENDELEA

2425 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!