Chupuchupu kwa Mkapa

Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Dakika 90 za mchezo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa miamba ya soka Tanzania Bara, Simba na Yanga, zimemalizika kila upande ukisema wenzao wameponea chupuchupu.

Mechi hiyo iliyofanyika jioni ya Jumamosi iliyopita imemalizika kwa sare ya bila kufungana, hivyo kuwaacha Yanga wakiendelea kuongoza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa pointi 20; pointi mbili mbele ya mabingwa watetezi, Simba wanaokamata nafasi ya pili wakiwa wamejikusanyia pointi 18 katika michezo minane ya raundi ya kwanza ya Ligi Kuu inayodhaminiwa na Benki ya NBC.

Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa, wanasoka wa kila upande wakionyesha umahiri wao katika kusakata soka, lakini hadi mapumziko, hakuna aliyeweza kuona lango la mwenzake.

Kwa kiasi fulani, viungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Khalid Aucho walionekana kulimiliki eneo la katikati ya uwanja, lakini utulivu wa hali ya juu wa beki wa kati wa Simba, Joash Onyango, uliliweka salama lango lake lililokuwa likilindwa na kipa namba moja wa Tanzania, Aishi Manula.

Ngome ya Simba iliyoongozwa na Onyango ambaye baadaye alionyeshwa kadi ya njano, iliimarishwa pia na Mohamed Hussein aliyefanya kazi kubwa kumlinda Manula.

Kwa muda mrefu kazi ya Onyango akisaidiwa na Henock Inonga ilikuwa ni kula sahani moja na Piston Mayele.

Hadi mwamuzi wa mchezo huo Herry Sasii anapuliza kipenga kuashiria mwisho wa dakika 90, hakuna bao lililopatikana, hivyo kuifanya Yanga kuendeleza rekodi ya kucheza mechi nane bila kufungwa.

Rekodi hiyo inayowapa kiburi mashabiki wake, ilitarajiwa kuvunjwa na Simba katika mchezo wa wiki iliyopita, lakini ikashindikana, na sasa mashabiki wa Yanga wanaamini timu yao itamaliza Ligi Kuu Tanzania Bara 2021/22 bila kufungwa.

Miongoni mwa vituko vilivyotokea katika mchezo huo ni kuzuiwa kuingia uwanjani kwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzale.

Kwa zaidi ya wiki moja Barbara aliongoza kile kilichoonekana kama mapambano dhidi ya TFF kupitia Bodi ya Ligi Kuu kutaka kuingiza ‘mdhamini mpya’ (GSM) katika Ligi Kuu.

Hata hiyo, kuzuiwa kwa Barbara, kwa mujibu wa TFF, hakukutokana na mapambano hayo yaliyosababisha kuondolewa kwa matangazo ya GSM katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizosambaa mitandaoni, Barbara anadai kuwa alifika uwanjani hapo akiongozana na familia yake kwa ajili ya kushuhudia mechi hiyo muhimu, lakini akazuiwa na maofisa wa TFF.

Inadaiwa kuwa Barbara alifika uwanjani hapo akiwa na ‘kila kitu’ kinachomruhusu kuingia.

“Asante sana Tanzania Premier League Board (TPLB – wasimamizi wakuu wa Ligi Kuu Bara) kwa kunizuia kuingia kwenye mechi na familia yangu. 

“God Bless Tanzania (Mungu ibariki Tanzania), God Bless Simba (Mungu ibariki Simba),” anaandika kiongozi huyo mwanamama wa moja kati ya klabu kubwa Afrika, Simba.

Lakini TFF sasa wanasema: “Tumesikitishwa na vitendo vya vurugu vilivyofanywa na baadhi ya viongozi wa Simba kwenye eneo la kuingilia Jukwaa la Watu Maalumu (VVIP) Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya mchezo wa Simba na Yanga.

“Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alifika eneo hilo akiwa na watoto watatu ambao hawaruhusiwi kuingia VVIP.

“Watoto hao walioongozana naye walikuwa na kadi za watu wengine walioalikwa kinyume cha utaratibu unavyotakiwa.

“Barbara ambaye aliruhusiwa kuingia, alianza kutoa lugha isiyofaa kwa ofisa wa TFF huku akirekodi video na baadaye kutupa kadi na kuondoka.

“Katika hatua nyingine, viongozi wa Simba walifanya vurugu kwenye eneo la kuingilia baada ya kutaka kulazimisha mmoja wa viongozi kuingia bila kadi ya mwaliko.

“Tukio hilo limeripotiwa kwenye mamlaka husika zinazosimamia mchezo.”

Akizungumza na mtandao wa Saleh Jembe, Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema kuwa wachezaji wake hawakutumia nafasi walizozitengeneza kwenye mchezo wao dhidi ya Simba.

Nabi anasema hakukuwa na timu iliyokuwa na uhakika wa kupata ushindi kwenye mchezo huo uliotawaliwa sawasawa na kila upande.

“Awali niliweka wazi kwamba uwezekano wa kupata ushindi ni nusu kwa nusu na ndivyo imetokea, hivyo hakuna wa kumlaumu.

“Naweza kusema kwamba Yanga hatukutumia nafasi tulizozitengeneza na hilo limetufanya tushindwe kupata ushindi, lakini wachezaji walicheza vizuri,” amesema.