*Nusu ya mapato yake yanatumika makao makuu

*Walimu wanaendelea kukamuliwa asilimia mbili

 

Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa, katika Mkutano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni alichangia Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kuhoji matumizi ya mabilioni ya shilingi yanayofanywa Makao Makuu ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT). Ifuatayo ni sehemu ya hotuba ya mbunge huyo.

Mheshimiwa Spika, kidogo naomba niwapongeze sana, siyo kidogo… niwapongeze sana walimu wote nchini wale ambao hawakugoma. Lakini sisemi niwalaani, lakini nawasikitikia sana sana walimu waliogoma. Kwa sababu kwa kitendo hicho hawakuwatendea haki watoto wetu na watoto wao.

 

Katiba za vyama na Sheria za Ajira na Uhusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004 zimeainisha namna ya fedha za chama zitakavyotumika na zitakavyonufaisha wanachama wake.

 

Mheshimiwa Spika, mimi hoja yangu ya msingi hapa nataka niwaulize hasa Waziri, hii michango ya asilimia mbili kwa kila mshahara wa mwalimu Tanzania nzima ni ya hiari au ni ya lazima? Lakini na matumizi yake nani anayaangalia.

 

Lakini niulize Mheshimiwa, hivi yule mwalimu aliyeko Sumve, aliyeko Njombe, aliyeko Peramiho ananufaika vipi na hizi hela?

 

Mheshimwa Spika, kwa sababu kwa taarifa ambazo ninazo ni kwamba fedha hizo zinaishia Makao Makuu. Mfano mwaka 2010 Chama Cha Walimu Tanzania kilikusanya Sh bilioni 16.491 kikatumia Sh bilioni 13.2. Kati ya hizo, Sh bilioni 7.8 zilitumika Makao Makuu peke yake.

 

Lakini mikoani ambako ndiko kwenye walimu wengi kwenye ofisi za mikoa za walimu zikapelekwa Sh milioni 944 tu, ukigawa kwa mikoa iliyokuwapo wakati huo kwa wale wanaojua hesabu zaidi sitaki niwarahisishie.

 

Lakini Maige yupo pale anaweza kugawa. Lakini wilayani kati ya Sh bilioni 13 Ofisi za Wilaya wakati ule zipo 104 walipeka Sh bilioni 2.6. Gawa kwa wilaya 104 utajua walipeleka ngapi? Lakini najiuliza hivi bilioni zote hizi ni kwa nini zitumike Makao Makuu peke yake… Sh bilioni 7.8 kuna nini? Kama siyo watu hawa wanajilipa posho wao wenyewe na kuna masilahi mengine?

 

Mheshimiwa Spika, lakini tukijiuliza lile jengo la Mwalimu House lipo pale Ilala, kuna benki imepanga pale, Wachina wamepanga pale hizo fedha zake nani anaziratibu? Nani anazitumia? Hivi tukiulizana humu ndani waheshimiwa wabunge kwenye wilaya zetu ni wapi ambapo pana SACCOs kupitia hii michamgo ya asilimia mbili ya walimu ambapo zinawanufaisha walimu wetu?

 

Mheshimiwa Spika, kazi yao ni kusema Serikali iongeze mishahara ili wapate fedha nyingi zaidi baadaye fedha ziwe nyingi zaidi, ili waweze kuzitumia wao wenyewe.

 

Mheshimiwa Spika, lakini mwaka 2011 makusanyo yalikuwa Sh bilioni 20.2 na matumizi yalikuwa ni Sh bilioni 15.7. Kati ya hizo fedha Makao Makuu yaliyopo Dar es Salaam yalitumia Sh bilioni 8.4 kwa kazi gani? Sijui. Lakini kwenye ofisi za mikoa wakapeleka Sh bilioni 1.2 tu, kwenye ofisi za wilaya wakapeleka Sh bilioni 3, tugawane kwenye wilaya hizo.

Lakini kipo kichekesho kingine ambacho itabidi tumwombe CAG labda aende akasaidie kukagua. Kwa sababu idadi ya walimu na kwa sababu wanaingizwa bila utaratibu mfuko huu nao ni vizuri kukaguliwa. Isije ikawa sehemu ya kichaka cha watu kujifichia kujipatia fedha na kunufaika, lakini ukienda kule ukimuuliza mwalimu, hebu niambie mwalimu katika huu mchango wa asilimia mbili unaouchanga hivi wewe unanufaika nini?

 

Mheshimiwa Spika, tofauti na mifuko mingine, ukichanga kwenye mifuko baada ya muda fulani miaka 60 unapata mafao yao. Lakini mfuko huu hivi kweli unamnufaisha namna gani mwalimu?

 

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana walimu wanatumika sana tu, walimu wetu wanatumika, watu wamekaa wamejirundika kule wanajilipa posho, wanajilipa marupurupu ‘kibao’. Nendeni mkahangaike halafu fedha sisi tuchukue tule! Kwa sababu ukiangalia Sh bilioni 7 Makao Makuu, Sh bilioni 8 Makao Makuu zinafanya nini? Kama siyo za kula?

 

Mheshimiwa Spika, lakini tukijiuliza lile jengo la Mwalimu House mapato yake yote yanatokana na wapangaji waliopo humu ndani yanakwenda wapi? Tujiulize, ndiyo maana nimesema ipo haja kubwa ukimchunguza mwenzako basi wewe uchunguzwe. Kwa sababu hawa kila siku Serikali wanaisema ni mbaya kumbe wapo watu wanaotaka kujinufaisha wao wenyewe.

 

Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri hili hebu alisimamie kwa sababu sioni sababu na ninajua na bahati nzuri nimetokea JUWATA, baada ya JUWATA ikaja OTTU na baadaye ikaja TUCTA.

 

Mheshimiwa Spika, taratibu za migomo zinajulikana. Lakini Serikali ina utaratibu wake – anakaa mwajiri hapa, TUCTA inakaa hapa, ATE inakaa hapa wanakaa wanazungumza kwa pamoja wanakubaliana. Wakishindana wanarudi wanakaa tena wanakwenda kuzungumza mpaka wanafikia muafaka. Lakini leo ukiwauliza hata huu mgomo wa walimu sina uhakika kama TUCTA walishirikishwa kama chama shirikishi ambacho ndiyo Chama Kikuu cha Vyama vingine hivi 14.

 

Nawaomba sana, Mheshimiwa Waziri vyama hivi havijaanza leo vina historia yake, na migomo hii haijaanza leo ina historia yake. Lakini migomo siyo suluhusho la ufumbuzi wa matatizoyetu.

 

Mheshimiwa Spika, namsihi sana Mheshimiwa Waziri vyombo vitatu hivi viwe na utaratibu wa kukaa kama ambavyo vilikuwa vinakaa zamani. Ulikuwa unaitwa utatu – Mwajiri, ATE na TUCTA.

 

1639 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!