Aliyekuwa Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mushengezi Nyambele, ameweka hadharani namna aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah, alivyokula njama kuzuia makontena kadhaa yenye shehena yasilipiwe ushuru.

Nyambele, ambaye pia alikuwa Mshauri wa Sheria wa TRA wa kwanza, anaeleza jinsi Dk. Hoseah alivyodiriki kumchongea kwa Rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa, baada ya kutofurahishwa na msimamo wake wa kutaka kodi stahiki za Serikali zilipwe.

Anasema: “Desemba 1996 nilijikuta ninakaimu kama Kamishna Mkuu. Desemba 24, 1996 nililetewa taarifa kwamba kuna makontena mawili ya nguo yalikuwa yatolewe kwenye bohari ya forodha Dar es Salaam kinyemela na wakala wa forodha, ambaye baadaye tuligundua kuwa ni rafiki wa karibu wa Edward Hoseah.

“Mpango wa kuyaondoa makontena hayo siku hiyo mchana ulizingatia ukweli kwamba wakati kama huo watu wengi wanakuwa katika pilikapilika za sikukuu, hivyo mzigo ungetoka ‘kilaini’.

 

“Wakala huyo alipanga kuuza nguo zilizokuwa kwenye makontena kama ujira wa kazi aliyokuwa amefanya kuyaondoa bandarini ili yasafirishwe kwenda kwa mwagizaji aliyekuwa anaishi Malawi.”

Anasema alitoa amri ya kuzuia kuondolewa kwa makontena hayo na mara baada ya Sikukuu ya Krismasi aliagiza maofisa wawili wa upelelezi wachunguze na watoe taarifa kamili juu ya mzigo huo tangu ulipowasili bandarini na sababu za kutosafirishwa kwenda Malawi ulikotakiwa kwenda.

“Kama sehemu ya uchunguzi wao, maofisa wale walikwenda kufungua makontena yale ili kuhakiki aina na kiasi cha bidhaa zilizokuwamo. Wakati wanajiandaa kuyafungua makontena yale, walizuiliwa na watumishi wa PCCB waliokuwa wametumwa na Edward Hoseah.

“Baada ya hapo Edward Hoseah alitumia ushawishi na hata vitisho kutaka makontena yale yaachiliwe na kukabidhiwa kwa wakala huyo, bila mafanikio.

 

“Baada ya kuona ameshindwa, aliandika barua kwa TRA akiagiza ikusanye kiasi cha Sh milioni 131.3 kama ushuru na kodi mbalimbali; jambo ambalo lisingewezekana kwa kuwa mali hiyo haikulengwa kutumiwa nchini mwetu,” anasema Nyambele.

Anasema wakati huo huo, iligundulika kwamba mwagizaji wa Malawi alikuwa amehama nchi na kwa vile alikuwa hakumlipa aliyetuma bidhaa zile, TRA ilipelekewa maombi ya kuruhusu  mzigo urejeshwe Thailand ulikotoka.

“Wakati tunajiandaa kutoa kibali cha kurejesha mzigo ulikotoka, Edward Hoseah alipeleka taarifa kwa Rais Mkapa ambaye aliagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kumpelekea taarifa haraka.

“Tangu mwanzo, mimi nilikuwa na msimamo kwamba hakuna kodi iliyostahili kulipwa hapa nchini iwapo mzigo ungepelekwa Malawi au kurejeshwa ulikotoka, na huo msimamo niliuweka kwa maandishi.

 

“Nilipohojiwa na hao waliotumwa kufanya uchunguzi, nilisisitiza msimamo huo. Bahati mbaya Edward Hoseah alikuwa miongoni mwa timu iliyoundwa kuchunguza utata juu ya mzigo huo. Kwa hiyo, haikuwa ajabu kwa timu ile kuwasilisha taarifa ambayo iliegemea kukandamiza uongozi wa TRA,” anasema.

Anaongeza kusema: “Kwa bahati nzuri nilipata tetesi mapema na nilihakikisha kwamba Rais anapata ukweli wa sakata lile. Hatimaye alikubaliana na msimamo wa TRA na kuagiza watumishi wa PCCB waliokuwa wameingilia kazi isiyowahusu wapewe onyo.

“Malipo yangu kwa kazi ile ya kuzuia makontena yasichukuliwe na swahiba wake Edward Hoseah hayakuchelewa. Uamuzi wa Rais ulitoka mwisho wa Februari, 1998. Juni 3, 1998 nililetewa ilani ya kujieleza chini ya kifungu cha 8(1) cha sheria ya kuzuia rushwa, ilani hiyo ilitumwa “Kwa Bwana Nyambele, Mamlaka ya Mapato”. Haikuwa kwenye karatasi rasmi ya taasisi hiyo na inaelekea kwamba mwandishi alikuwa hana au hajui hata majina yangu yote.

 

“Inawezekana pia kuwa mwandishi alikuwa na haraka sana, hivyo hakujali kutumia karatasi rasmi au kuandika majina yangu yote. Ilani ilinitaka niorodheshe mali zangu zote ikiwa ni pamoja na fedha taslimu, fedha katika akaunti n.k na ‘nijieleze kiukweli na kiusahihi’ jinsi nilivyopata fedha kuniwezesha kupata mali hizo. Nilitakiwa kuwasilisha maelezo hayo katika muda wa siku 3 tangu nikabidhiwe ilani hiyo. Niliwasilisha majibu ya ilani hiyo katika muda niliopewa.”

Jitihada za kumpata Dk. Edward Hoseah ili kupata maelezo yake dhidi ya tuhuma hizi hazikuweza kufanikiwa. Gazeti la JAMHURI linaendelea kumtafuta.

By Jamhuri