Uamuzi wa Uingereza kupiga kura ya maoni kuwa ndani au nje ya Umoja wa Ulaya (EU) unaogopesha. Watu wanaweza kuona ni kitu kidogo hapa au hapo nyumbani, lakini ukizama kwa kina unaona kwamba tayari kuna mtetemeko kwenye sekta mbalimbali za jamiii.

Ile tu Waziri Mkuu, David Cameron kuahidi kura hiyo, kumejenga mazingira kwamba kuna uwezekano mkubwa wa wakubwa hawa wa uchumi kuondoka EU.

 

Ndani ya chama chake watu wamefurahia kwamba demokrasia na uhuru vinakua, kwenye chama cha upinzani – Labour wanafikiria wamseme vipi, na wachumi wanaendeleza utafiti wao.

 

Kwa ufupi tu katika siku mbili tatu hizi, habari hizo hazijapokewa vizuri kwenye masoko ya fedha na hisa ya kimataifa, maana haitakuwa afya kuikosa Uingereza ndani ya EU.

Yote kwa yote, hata Waingereza wanaoangalia mbali wanaona sio siha njema kwenda huko, maana ni kukaribisha mvunjiko.

 

Kwa kifupi huu ni uchuro kama wa bundi anapolia, hata kama Cameron na matori wanasema kwamba kura hiyo itapigwa mwaka 2017 au baada ya hapo.

Kuna vigezo kadhaa kabla ya hiyo kura kupigwa, na itategemea iwapo wanachama wengine 26 wa Umoja wa Ulaya watakwenda na matakwa ya wakati huo ya Uingereza.

 

Nchi za EU zina rekodi dhaifu kihistoria, kuhusiana na kuchukua uamuzi kwa kauli moja juu ya suala lolote. Katika mazingira haya, hili linabaki kuonekana kama karata ya Cameron na chama chake, tena yenye malengo mawili.


La kwanza ni kuwatenganisha matori na Liberal Democrats waliooana kisiasa na kuunda serikali ya pamoja (chini ya Cameron na Nick Clegg).


Pia hii ni karata inayolenga kuwanyima pumzi jamaa wa mrengo wa kulia – Chama cha UKIP ili washindwe kuendeleza mashambulizi dhidi yake, chama chake na serikali yao.


Cameron amefikiria sana kabla ya kufanya uamuzi huu, na ni kwa vile vyombo vya habari vimegawanyika, kisiasa walau, basi unaonekana kwamba ni uamuzi mzuri na muhimu.


Swali kubwa la kujiuliza hapa ni iwapo kiukweli, tukiachana na siasa zake, uamuzi huo utasaidia na unajenga kitu kizuri au unaharibu umoja na kuongeza mipasuko?


Masoko nayo hayawezi kudanganywa kirahisi namna hii, ndiyo maana mpaka mwisho wa wiki iliyopita hapakuwa na habari njema sana kuhusu uchumi wa Uingereza kukua wala sarafu yake (Sterling Pound) kuimarika.


Pauni tayari ipo chini ya shinikizo kubwa na mpaka Alhamisi ya wiki iliyopita, pauni ilikuwa kwenye 1.18 ikilinganishwa na sarafu ya Euro – kiwango ambacho ni kidogo zaidi katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.


Labda tusubiri kuona walau wiki au mwezi mmoja baada ya uamuzi wa Cameron mambo yatakuwaje kwenye uchumi, moja ya mihimili mikubwa ya EU. Je, hatima ya Uingereza ipo ndani au nje ya Umoja wa Ulaya? Tafakari, tuwasiliane.


By Jamhuri