Vyama vya upinzani bado ni vichanga? (1)

Mara kwa mara Watanzania huzungumzia juu ya vyama vya siasa, hasa vyama wanavyoviita vyama vya upinzani au vya ukingani. Mazungumzo hayo ni kuhusu sababu za kuanzishwa, shughuli zinazofanywa na malengo ya vyama hivyo.

Ukweli, chama cha upinzani ni chama cha siasa chenye malengo na madhumuni ya kushika dola. Kuongoza, kutawala kitakapopata ridhaa ya wananchi wengi wanaokubali na kupokea sera za chama hicho.

Asili ya vyama hivyo hapa Tanzania ni wakoloni. Ndiyo walioleta kitu hiki — chama cha upinzani — wakiwa na malengo ya kupinga vyama vya siasa vya wananchi vinavyojishughulisha na harakati za ukombozi, kupigania Uhuru na kuondoa Serikali ya kikoloni madarakani. Mtindo huo haukufanyika hapa nchini kwetu tu, bali ulimwenguni kote.

Kwa mfano, huku Tanganyika baada ya wananchi kuanzisha Tanganyika African National Union (TANU) Julai 7, 1954, Chama cha Ukombozi kitaifa; aliyekuwa Gavana wa kikoloni, Sir Edward Twining, alihamasisha na kuwatumia baadhi ya watumishi wa  Serikali, viongozi wa dini na wananchi kuanzisha United Tanganyika Party (UTP) – chama cha kupinga harakati za TANU na kuendeleza kulinda maslahi ya wakoloni. Gavana huyo alisimamia kikamilifu kuandikishwa rasmi kwa UTP Machi 27, 1956.

Kule Zanzibar, baada ya wananchi kugundua hila na njama za Waarabu kuanzisha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) – chama kilichotokana na Arab Association mwaka 1955, waliunganisha vyama vyao vya African Association na Shirazi Association na kuunda Afro-Shirazi Union (ASU), Februari 5, 1957. Baadaye katika harakati za ukombozi walibadili jina na kuwa  Afro-Shirazi Party (ASP).

Kuzaliwa kwa ASP kulimfanya sultani wa Zanzibar na Waarabu wenzake pamoja na mdhamini wao, Mwingereza, kubadili madhumuni ya ZNP ya mwanzo na kuweka mapya ya kudai Uhuru, kuendeleza maslahi ya wakoloni na kukipinga chama cha ukombozi kitaifa cha ASP.

Baada ya vyama vya TANU na ASP kuwa imara katika harakati za kudai Uhuru, vyama vingine vingi vilianzishwa vikiwa na malengo, ama ya kudai uhuru au kupinga harakati za kupigania Uhuru na kuendeleza maslahi ya wakoloni. Kwa mfano, kule Zanzibar vyama kama Zanzibar and Pemba Peoples Party (ZPPP), Umma Party vilianzishwa.

Hapa Tanganyika vyama vya African National Congress (ANC), All Muslim African Democratic Union (MADU), All African Tanganyika Federal Independence cha mjini Tanga kilichokuwa na msimamo wa Serikali ya majimbo au mikoa kilianzishwa.

Ukweli, baada ya TANU kushinda harakati za ukombozi na kuipatia Tanganyika Uhuru Desemba 9, 1961 chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na ASP kuamua kufanya mapinduzi Januari 12, 1964, chini ya uongozi wa Sheikh Abeid Amani Karume, kupinga na kondoa Uhuru bandia wa wananchi wa Zanzibar uliopatikana Desemba 10, 1963 chini ya Serikali ya Sultan ikiongozwa na Waziri Mkuu, Sheikh Mohamed Shamte, na Rais wa ZPPP pamoja na Ali Muhsin wa ZNP.

Mapinduzi hayo ya Zanzibar yaliwezesha Zanzibar huru  kuungana na Tanganyika huru kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aprili 26, 1964.

Tanzania ilikumbwa na mfumo wa utawala wa chama kimoja cha siasa uliopiganiwa duniani, na huku ndani Tanzania kupata msukumo wa Wananchi kupuuza vyama vingi vya siasa. Baadhi ya vyama vilikufa vyenyewe na vingine kuondolewa na wananchi.

Tanzania ikiwa inatawaliwa na Serikali iliyoendeshwa na vyama viwili vya siasa vyenye msimamo mmoja, TANU na ASP, hadi vilipoamua kuungana na kuwa chama kimoja cha siasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Februari 5, 1977.

Kama wataalamu wa mambo ya kale wasemavyo kuwa historia hujirudia, ni kweli vuguvugu la mageuzi ya kisiasa yaliyoanzia miaka ya 1980 yalifikia kilele chake katika miaka 1990, hasa pale kambi ya kimashariki ya kisoshalisti iliyokuwa chini ya Urusi kuparaganyika na hatimaye kufa.

Ukweli, kumefanya nchi nyingi duniani kuyumba na hasa za Afrika na za kusini mwa dunia na nyingine kujitoa katika kambi hii na kujiunga na kambi ya Magharibi ya kibepari inayoongozwa na Marekani, iliyotopea kwenye ubeberu na kuzaa huu mfumo wa ujanja wa utandawazi.

By Jamhuri