Vyama vya upinzani ni vichanga? -2

sehemu ya kwanza ya makala haya, wiki iliyopita nilizungumzia chimbuko la vyama vingi vya siasa kabla na baada ya Tanzania  kuwa huru. Leo tunaendelea na sehemu ya pili.

 

Baada ya vyama vya TANU na ASP kuwa imara katika harakati za kudai uhuru, vyama vingine vingi vilianzishwa vikiwa na malengo ama vya kudai uhuru au kupinga harakati za kupigania uhuru na kuendeleza maslahi ya wakoloni kwa mfano, Kule Zanzibar vyama kama Zanzibar and Pemba People Party ZPPP, Umma Party vilianzishwa.

Hapa Tanganyika vyama vya African National  Congress (ANC), All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT), People Democratic Party (PDP), Masasi African Democratic Union (MADU), All African Tanganyika Federal Independence cha mini Tanga kilichokuwa na msimamo wa Serikali ya majimbo au mkoa kilianzishwa pia.

 

Kama  wataalamu wa mambo ya kale wasemayo kuwa historia hujirudia, ni kweli vuguvugu la mageuzi ya kisiasa yaliyoanzia mnamo miaka ya 1980 yalifikia kilele chake katika miaka 1990 hasa pale kambi ya Mashariki ya kisoshalisti iliyokuwa chini ya Urusi kuparaganyika na hatimaye kufa.

 

Ukweli kumefanya nchi nyingi duniani kuyumba na hasa za Afrika na za kusini mwa dunia na zingine kujitoa katika kambi hii na kujiunga na kambi la Magharibi ya kibepari inayoongozwa na Marekani, iliyotopea kwenye ubeberu na kuzaa huu mfumo wa ujanja ujanja wa utandawazi.

 

Tanzania haikuwa na njia ya kufanya, ilibidi lazima ikubali mfumo wa vyama vingi duniani. Suala la kuridhia mfumo huo haukuwa na mjadala. Naweza kusema vyama vingi vya siasa awamu ya pili hapa nchini vilianza 1992. Leo vyama vingi vya siasa ambavyo tunaviita vyama vya upinzani vina umri wa miaka 21 na CCM, chama tawala kina umri wa miaka 36.

 

Historia inatufahamisha kuwa wakati wa vuguvugu la ujio wa vyama vingi katika awamu ya pili mnamo miaka ya 90, Watanzania wengi hawakupenda kuweko kwa vyama hivyo,  kwa madai vingeleta ghasia. Watu kufarakana, kuuana hata kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe  nchini.

 

Dhana hizo zilijengwa na watu ambao walizoea taratibu za uongozi wa chama kimoja cha siasa na walipata kusikia au kuona nchi, zenye vyama vingi watu kugombana mara kwa mara kutokana na tofauti zao za kisiasa.

 

Watu waliotaka vyama vingi vya siasa waliamini kwamba kuweko kwa vyama hivyo ni kuweka demokrasia ya kweli, yenye kutoa uhuru wa mawazo, uhuru wa kuchagua kiongozi amtakaye, kusimamia haki, usawa, kuondoa dhuluma, uonevu na kadhalika. Misimamo miwili ya kuweko na kutokuweko mfumo wa vyama vingi uliibua mjadala mzito uliojaa hoja mbalimbali yakinifu.

 

Asilimia 80 ya Watanzania walitaka mfumo wa chama kimoja na asilimia 20 walitaka mfumo wa vyama vingi. Busara ilitumika kupitisha asilimia 20, na nchi kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Hii ina maana wengi wape na wachache wasikilizwe.

 

Katika uchaguzi wa mwaka 1995, Watanzania wamevieleza vyama vya upinzani ni vichanga kwa maana ya kuwa na umri wa miaka mitatu vikiliganishwa na CCM kilichofikisha umri wa miaka 18. Aidha vilihesabika kukosa viongozi bora na weledi wa kuendesha vyama na kushiriki katika chaguzi.

 

Pamoja na uchanga wao na kukosa viongozi weledi na wenye tajiriba, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 1995 vyama visivyopungua 10 vilishiriki uchaguzi huo, vikiwemo NCCR-Mageuzi, CUF na UDP pamoja na CCM, chama tawala vikisimamisha wagombea urais ubunge na udiwani.

 

Katika uchaguzi huo Mwalimu Nyerere alishiriki kikamilifu katika kampeni za kukinadi chama chake CCM na mgombea urais kwa tikiti ya chama hicho, Benjamin William Mkapa. Katika kampeni hizo, Mwalimu Nyerere mara kwa mara alisikika akisema kuwa vyama vya upinzani havina sifa na uwezo wa kushika Dola katika uchaguzi huu (1995) hata wa 2000 na 2005. Labda labda uchaguzi wa 2015.

 

Hiyo ni kauli nzito na yenye welevu mkubwa. Inahitaji tafakuri makini. Ni kweli tangu uchaguzi wa 1995 hadi 2010 hakuna chama chochote cha upinzani kilichoshinda.

 

 

1631 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!