Serikali itangaze elimu ya msingi haitolewi bure tena

Elimu ya msingi hapa Tanzania imeendelea kuwagharimu wazazi na walezi fedha nyingi, licha ya Serikali kutangaza kuwa inatolewa bure (bila malipo yoyote).

Inashangaza kuona na kusikia Serikali inaendelea kutangaza kuwa elimu ya msingi hapa nchini inatolewa bure, kwa maana ya kugharamiwa na Serikali wakati ukweli wa mambo ni kwamba haitolewi bure!

 

Tena suala hili siku hizi si kificho tena, liko wazi. Hata viongozi wa Serikali wakiwamo wa wizara husika wanajua ukweli ulivyo. Kwamba elimu ya msingi haitolewi bure tena hapa Tanzania.


Kama mzazi au mlezi hana fedha, basi ni dhahiri kuwa mtoto wake hana nafasi ya kupata haki yake ya msingi ya kupata elimu ya msingi hapa Tanzania. Nani anapinga?

 

Tanzania ndiyo nchi pekee katika Afrika Mashariki, na pengine duniani, ambayo Serikali yake haijafanikiwa kudhibiti michango lukuki isiyo rasmi katika shule za msingi na sekondari.


Siku hizi, ili mzazi au mlezi aweze kumsajili mtoto wake kuanza darasa la kwanza hapa hapa Tanzania, katika shule hizi hizi za Serikali yetu, lazima awe amejipanga sawasawa kwa kuhakikisha anakuwa na kitita cha fedha mkononi.

 

Kitu cha kwanza, kila mtoto anayeandikishwa kuanza elimu ya msingi hutakiwa kulipiwa kati ya Sh 15,000 na Sh 30,000 za dawati katika shule hizi hizi za Serikali, zinazotangazwa na Serikali hii hii kwamba zinatoa elimu bure kwa watoto wa Kitanzania.

 

Lakini pia mtoto huyo huyo hutakiwa kulipiwa na mzazi au mlezi wake kati ya Sh 3,000 na 5,000 za nembo ya shule husika. Pia hudaiwa kati ya Sh 5,000 na 10,000 kuchangia ujenzi wa majengo ya shule kila baada ya miezi sita au mwaka.

 

Huko shuleni wanafunzi ni mithili ya mtaji wa ama walimu, au shule husika. Wanaandamwa na mlolongo wa michango holela ya fedha. Wanachangishwa fedha za kugharimia uchapishaji wa mitihani yao kati ya Sh 1,000 na 3,000 kila wiki. Lakini pia, kila mwanafunzi hulipiwa na mzazi au mlezi wake kati ya Sh 1,000 na 2,000 kuchangia mshahara wa mlizi wa shule kila mwezi.

 

Suala la twisheni nalo limeendelea kushamiri kwa kasi ya ajabu katika shule hizi hizi za Serikali. Walimu walioajiriwa na Serikali ndiyo hao hao wanaochangisha wanafunzi fedha za twisheni. Kwenye vipindi vya twisheni wanafundisha masomo yale yale kwa kutumia majengo yale yale ya shule za Serikali.


Gharama za twisheni zinatofautiana. Baadhi ya shule zinatoza Sh 7,000 na nyingine zinatoza Sh 10,000 kwa kila mwanafunzi kwa mwezi.

 

Ikumbukwe kwamba gharama zote hizo na nyingine nyingi, ambazo sikuzitaja ziko nje ya zaidi ya Sh 50,000 zinazotumika kumnunulia mwanafunzi sare za shule, madaftari, vitabu na kadhalika.

 

Sasa katika hali kama hiyo, katika mazingira kama hayo, makabwela wataendelea kumudu gharama za elimu ya msingi kwa watoto wao? Jibu ni kwamba hawawezi, itafika wakati watashindwa kabisa.

 

Je, kuna uhalali wa Serikali kuendelea kuutangazia umma wa Watanzania na dunia kwa jumla kwamba elimu ya msingi hutolewa bure hapa Tanzania? Kwamba Serikali yetu inagharamia elimu ya msingi kwa watoto wa Kitanzania? Jibu ni hapana.

 

Basi, niseme tu kwamba ingependeza kusikia na kuona Serikali yetu inasema ukweli; inatangaza kuwa elimu ya msingi haitolewi bure tena hapa Tanzania kama ilivyokuwa enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Serikali ya Awamu ya Kwanza) na Ali Hassan Mwinyi (Serikali ya Awamu ya Pili).

 

Mungu ibariki Serikali yetu iweze kusimamia matamko yake kwa vitendo badala ya maneno matupu yasiyovunja mfupa. Amina.

By Jamhuri