Wengine waige Vodacom kuwajali wafanyakazi

Kampuni ya Vodacom Tanzania ni mfano mzuri wa kuigwa, katika uwasilishaji wa makato ya fedha za wafanyakazi wake kwenye Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Hicho ndicho kilichoiwezesha Vodacom kuibuka mshindi wa Tuzo ya Kampuni Bora ya Mawasiliano nchini inayowasilisha ipasavyo michango hiyo ya wafanyakazi wake katika mfuko huo. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, alikabidhi tuzo hiyo kwa Mkuu wa Vodacom Kanda ya Kaskazini, Philemon Chacha, katika hafla ya ufunguzi wa mkutano wa wadau wa NSSF jijini Arusha, wiki iliyopita.

 

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Crescentius Magori, amesema asilimia 95 ya wafanyakazi wa Vodacom wamekuwa wakilipiwa makato hayo kikamilifu na kwa wakati katika NSSF.


Ofisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Vodacom, Dk. Fred Mwita, ameielezea tuzo hiyo kuwa ni matokeo ya dhana iliyojengwa na kampuni hiyo ya kujali maslahi ya wafanyakazi wake yakiwamo mafao yao.


“Pamoja na kwamba tunatekeleza wajibu huo kwa mujibu wa sheria, ushindi huu ni kielelezo cha udhati na umakini wetu katika kutimiza kila wajibu unaotuhusu kwa wafanyakazi wetu,” amesema Dk. Mwita.

 

Vodacom imeweka kipaumbele cha upekee katika maslahi ya wafanyakazi wake, kwa kuwa inaamini kwamba mafanikio ya kampuni hiyo yako mikononi mwao kwa kujibidiisha kutekeleza majukumu yao.

 

Utamaduni huo wa Vodacom ni mfano mzuri unaopaswa kuigwa na kampuni nyingine, hususan ambazo viongozi wake hawathamini wafanyakazi na maslahi yao.

 

Kuna kampuni nyingi katika nchi hii zilizokaliwa na viongozi miungu-watu, wanaodhulumu na wanaowanyanyasa wafanyakazi wao katika suala la maslahi kwa kiwango kisichomithilika.

 

Viongozi wa baadhi ya kampuni wamekuwa mstari wa mbele kukata fedha za mishahara ya wafanyakazi wao, lakini hawaziwasilishi kwenye mifuko ya hifadhi ya mafao ya jamii. Hii ni dhuluma, uonevu na unyanyasaji mkubwa!

 

Kwa bahati mbaya hata mamlaka zenye jukumu la kutetea maslahi ya wafanyakazi ni kama zimejiweka kando, hazijaonesha dhamira ya kweli ya kushughulikia kampuni zinazowanyong’onyeza wafanyakazi kiasi hicho.

 

Wafanyakazi wengi Tanzania ni hohehahe kutokana na kuendelea ‘kulizwa’ na kampuni wanazozifanyia kazi, wanashindwa kumudu mahitaji muhimu ya familia zao. Serikali haijaonesha dhamira ya dhati ya kuwasaidia wapate stahili zao. Lakini kwa upande mwingine, NSSF nayo imeonesha mfano mzuri wa kuigwa, kwa kuanzisha tuzo kwa kampuni zinazowasilisha ipasavyo makato ya fedha za wafanyakazi wake.

 

Ni vizuri mpango huo wa NSSF uigwe na mifuko mingine ya mafao ya jamii, ukiwamo Mfuko wa Pensheni za Mashirika ya Umma (PPF).

Mifuko ya hifadhi ya mafao ya jamii pia inapaswa kusimama imara kwa kuhakikisha viongozi wa kampuni zote wanawasilisha kikamilifu na kwa wakati michango ya fedha za wafanyakazi wao.

 

Vinginevyo kampuni nyingi zitaendelea kuwanyanyasa, kuwadhulumu na kuwapunja wafanyakazi mafao yao. Katika hilo, viongozi wa mifuko ya hifadhi ya mafao ya jamii na Serikali hawatakwepa lawama za kuchangia kudhoofisha hali ya maisha ya wafanyakazi na familia zao.


1016 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!