Golikipa wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya Ujerumani, Nadine Angerer, ameshinda tuzo ya mwanamke bora mcheza soka barani Ulaya.

Angerer anayetarajia kuanza kucheza soka la kulipwa nchini Marekani mwaka kesho, aliwashinda wachezaji wengine wa timu hiyo, Lena Goessling na mshambuliaji Lotta Schelin kutoka Sweden.

 

Mwanamke huyo alishinda tuzo hiyo ya UEFA kutokana na kura zilizopigwa na waandishi wa habari za michezo zilizopendekezwa na wakufunzi wa timu za wanawake zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa.

 

Wafuatiliaji wa matukio ya soka watakumbuka jinsi Angerer alivyoweza kuzuia mikwaju ya penalti mara mbili katika fainali ya Ulaya mwaka 2013 na hivyo kuisaidia Ujerumani kuishinda Norway kwa goli 1-0.

 

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34, atacheza soka lake nchini Australia akichezea klabu ya Brisbane Roar kabla ya kujiunga na klabu inayoshiriki Ligi ya Soka kwa wanawake.

 

Hata hivyo, Angerer anasema kuwa bado hatua hiyo haijathibitishwa lakini kwa vyovyote mipango hiyo itaanza mwaka 2014.

By Jamhuri