* Sh mil 763.8 zakwapuliwa kifisadi

* Mwenyekiti CCM Mkoa ahusishwa

* Waandishi wa habari wapata mgawo

Siku chache baada ya gazeti hili kuchapisha taarifa za nyaraka zinazoonesha Halmashauri ya Wilaya ya Geita ilipokea Sh bilioni 11.1 za kununua madawati lakini fedha hizo hazijulikani zilivyotumika, taarifa nyingine zimepatikana zikionesha ubadhirifu wa Sh zaidi ya milioni 763 katika halmashauri.

Taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu wa Ndani katika halmashauri hiyo, iliyotolewa mwaka 2011 inaonesha kuwa mwaka 2010 Sh milioni 763.8 zilitumika katika mazingira ya ubadhirifu, licha ya mkaguzi huyo kutahadharisha kuwa ni wizi wa fedha za umma.

 

“Chini ya kanuni ya 18 ya fedha za umma ya 2001 na tangazo la Serikali namba 132 la 06.04.2001 huu ni upotevu wa fedha,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

 

Wakati mkaguzi huyo akionesha kile alichokiita wizi wa fedha za umma, Diwani wa Kata ya Kasamwa, Fabian Mahenge, amemrushia tuhuma mzito Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Geita, Joseph Musukuma, kuwa alihusika kuwalinda wezi wa fedha hizo.

 

Amefafanua kuwa madiwani wa upinzani walipeleka hoja kwenye Baraza la Madiwani kutaka iundwe tume maalum ya madiwani kuchunguza tuhuma za wizi huo, lakini Musukuma pia aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita alishirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo kukataa hoja hiyo.

 

“Sisi tulipata taarifa hiyo mapema na tulifuata utaratibu wa kikanuni, tukapeleka hoja kwenye Baraza la Madiwani ili iundwe tume maalum kuchunguza wizi huo na wahusika wafikishwe mahakamani, lakini Musukuma alikula njama na mkurugenzi wakaficha hoja yetu na kukataa kujadiliwa.

 

“Huyu Musukuma kuna kila dalili kuwa alikuwa anakula nao ndiyo maana alikuwa anawatetea sana na kuwalinda, lakini alikuwa wa kwanza kwenda kwenye vyombo vya habari na kuutangazia umma eti anapambana na wala rushwa wakati ndiye anayewakingia kifua kwenye Baraza,” alidai Mahenge.

 

Ripoti hiyo yenye Kumb. Namba GDC/CF.10/12/VOL.VI/25 Desemba 31, 2010 iliyoandikwa kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo na kusainiwa na Marwa Wankyo kwa niaba ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani,  iliweka hadharani upotevu wa mamilioni hayo ya shilingi.

 

Taarifa hiyo inabainisha kuwa upotevu huo ulifanyika katika maeneo mbalimbali, ambapo Sh 252,218,234  zinaonesha ni malipo yaliyofanyika bila hati. Mkaguzi huyo anabainisha kuwa hati za malipo zinapaswa kuwapo kwenye sefu ya mtunza fedha wa halmashauri lakini matumizi hayo hayakuandikiwa hati.

 

Kuhusu malipo ya fedha bila kutolewa kwa taarifa za mafunzo na utekelezaji, Sh 55,102,800, mkaguzi anasema fedha hizo zinaonekana kulipwa kwa watumishi mbalimbali wa halmashauri hiyo kwa kazi tofauti, lakini hazionekani kwenye mafaili na hakuna hati ya malipo (payment vouchers).

 

“Hakuna viambatanisho muhimu kama barua za kuitwa kwenye semina, mafunzo, wahusika wangapi na zana za kufundishia. Uhalali wa kufanyika kwa kazi hizo unakosekana, hivyo yawezekana fedha hizo hazikutumika kwa shughuli za halmashauri,”  anasema mkaguzi huyo.

 

Masurufu yaliyolipwa kwa watumishi lakini hayajarejeshwa ni Sh 74,375,175. Mkaguzi alibaini kulipwa kwa masurufu hayo kwa watumishi wa halmashauri hiyo lakini  hayakurekodiwa kwenye hati za malipo na vitabu vya masurufu.

 

“Inaashiria kukosekana kwa usahihi wa matumizi ya fedha za umma,”  anasisitiza mkaguzi huyo kwenye ripoti yake.

 

Malipo yenye nyaraka pungufu ni Sh 115,996,999. Mkaguzi alibainisha kuwapo malipo hayo bila nyaraka za kuthibitisha usahihi wake. Malipo mengine yalibainika kufanyika Desemba 7, 2012 kupitia namba hundi 125821. Halmashauri ililipa Sh 25,180,000 kwa ajili ya miradi na usambazaji wa miongozo ya MMAM.

 

Mkaguzi alibaini kutokuwapo kwa saini za wahusika waliopokea fedha hizo, lakini Sh 18,000,000 zilitumika kudurufu nakala 180,000 za miongozo ya MMAM na alithibitisha kwamba hakuna ushahidi wa nakala hata moja ya mwongozo wa MMAM.

 

Mkaguzi anahoji kwanini nakala moja ilitolewa kwa watu binafsi 100 wakati kuna wazabuni wa Serikali walioshinda kupitia Wakala wa Huduma ya Ununuzi wa Vifaa na seiikalini (GPSA).

 

kuhusu malipo ya posho ya vikao vya timu ya  uongozi wa hospitali Sh 2,466,000, mkaguzi alibaini ulipwaji wa posho kubwa tofauti na kiwango cha kawaida. Wajumbe sita walilipwa Sh 60,000 kila mmoja na wajumbe wengine 21 walilipwa Sh 100,000 kila mmoja, ingawa walistahili walipwe Sh 20,000 kila mmoja. Pesa hizo zililipwa kwa hundi namba 125835 ya Desemba 13, 2010.

 

Desemba 12, 2010 kupitia cheki namba 123803 akaunti ya maendeleo, halmashauri hiyo ililipa Sh 3,600,000 kwa M/S  Suitable Pace Systems kwa ajili ya kudurufu nakala 35,000 na kutengeneza vitabu nakala 20 lakini mkaguzi alibaini kuwa nakala hizo hazikuwapo.

 

Novemba 15, 2010 kupitia hundi  namba 126044, halmashauri ilimlipa  M/S Sood Garage Sh 2,880,000 kwa ajili ya matengenezo ya gari namba  SM 5264 lakini mkaguzi alibaini kuwa hapakuwapo na mkataba wa kazi, maombi ya matengenezo ya gari hilo kutoka idara husika ya afya, taarifa ya kukagua gari kabla na baada ya matengenezo wala hati ya madai (invoice) lakini malipo yamefanyika.

 

Ununuzi wa vifaa na huduma mbalimbali kwa njia ya masurufu unaonekana uligharimu Sh 85,200. Mkaguzi alisema halmashauri iliidhinisha ununuzi na  ujenzi kwa njia ya masurufu kinyume cha kanuni ya 63 na 78 za ununuzi wa umma za mwaka 2005 na tangazo la Serikali namba 97 la Aprili 15, 2005.

 

Ununuzi wa mafuta na vilainishi bila kupokewa kwenye vitabu na matumizi hayakutolewa, unaonekana kugharimu Sh 89,192,760. Akaunti zilizokaguliwa na kukutwa na upungufu ni za afya na uchaguzi.

 

Mkaguzi alibaini utata wa malipo yaliyofanyika kwa ankara kifani (proforma invoice) kutoka  M/S Hamdy Hassan Filling Station, yaani malipo kwanza kabla ya kupatiwa huduma.

 

Mafuta na vifaa havikupokewa  kwenye daftari la vifaa (stores ledger). Ununuzi wa mafuta kwa kiasi kikubwa kwa wakati mmoja na haijulikani mafuta yalikabidhiwa kwa nani kwani hakuna hati ya kukabidhi vifaa (Delivery note) iliyosainiwa.

 

Mapunjo ya posho za usumbufu Sh 1,316,597.20 zililipwa kinyume cha kanuni za kudumu za utumishi wa umma toleo la mwaka 2009 liloanza kutumika mwaka 2010 kifungu cha L.13. Halmashauri ilipunja watumishi mbalimbali, kwa mfano, ilimlipa  Francis P. Kaghoma Sh 90,000 kupitia cheki namba 126903  badala ya Sh 225,000.

 

Mafuta yaliyochukuliwa bila kuonekana kwenye daftari za magari husika yanaonekana kugharimu Sh 4,830,780. Mkaguzi alibaini kuwapo kwa lita 2,466 za mafuta zilizochukuliwa lakini hazionekani kwenye madaftari ya magari husika.

 

Inaonekana Sh 6,915,000 zilitumika kulipa vifaa bila kukaguliwa na kamati ya ukaguzi wa vifaa. Kupitia hundi namba 125818 ya Desemba 6, 2010 halmashauri ilimlipa Frank Maganga kiasi hicho cha pesa kwa ajili ya kununua vifaa vya kompyuta na shajara.

 

Malipo yenye mashaka kiasi cha Sh 68,899,000, mkaguzi alibaini matumizi ya kiasi hicho cha pesa kwa  mchanganuo kuwa Oktoba 29, 2010 kupiti hundi namba 1320625 mlipwaji ni Hamdy Hassan Filling Station  kwa ununuzi ya lita 7,000 za dizeli zenye thamani ya Sh 13,300,000. Hakuna maelezo kuhusu mafuta yalivyotumika.

 

Oktoba 19, 2010 kupitia hundi namba 120613 mlipwaji DED kwa ununuzi wa lita 700 za dizeli kwa thamani ya Sh 1,300,000 na hakuna maelezo ya matumizi yake.

 

Agosti 18, 2010 hundi namba 120608 mlipwaji DED kwa ununuzi wa lita 700 za dizeli zenye thamani ya Sh 1,260,000 na Novemba 10, 2010  kupitia hundi namba 115777 mlipwaji akiwa ni Kamena General Traders kwa kazi ya kudurufu nakala 112,500 na kutengeneza vitabu 225, lakini nakala hizo hazikuonekana na hakuna taarifa ya ukaguzi wa vifaa (Goods inspection report).

 

Mtoa taarifa wetu ameendelea kuieleza JAMHURI kuwa watumishi wa halmashauri hiyo walifanikiwa kuwaweka “mateka” kifedha, baadhi ya waandishi wa habari {majina yanahifadhiwa kwa sasa}  kwa kuwalipa fedha ili wasifichue wizi huo.

 

“Baadhi ya waandishi wa habari waliyoonekana kufuatilia walikuwa wanaitwa, wanaandikiwa hundi kwamba wamefanya kazi maalum lakini kazi hizo hazikuwapo; kumbe ni ruswa ili wasifichue wizi huo,” kimesema chanzo chetu cha habari.

 

Wakati waandishi wa habari wakituhumiwa, ripoti hiyo ya mkaguzi inaonesha kuwa Oktoba 12, 2010 halmashauri ililipa Sh 1,020,000 kupitia hundi namba 123722 kwa waandishi wa habari kwa ajili ya posho ya kutangaza miradi ya maendeleo, lakini mkaguzi alibaini hakuna mkataba wa kazi hiyo na hakuna nakala ya matangazo hayo wala risiti.

 

Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina historia ya kupata hati za mashaka kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo, ambapo mwaka wa fedha 2009/2010 na mwaka 2010/2011 ilipata hati yenye mashaka, na matumizi ya Sh 230,494,054 yalitiliwa shaka na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

By Jamhuri