Hapatoshi Wydad vs Esperance

Hatimaye timu ya Esperance de Tunis ya Tunisia na Wydad Casablanca ya Morocco zimefanikiwa kufuzu katika hatua ya fainali ya Klabu Bingwa barani Afrika (CAF Champions League).

Esperance wameingia fainali baada ya kuwafunga TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo goli 1-0 katika mechi ya raundi ya kwanza wakiwa uwanja wa nyumbani. Katika mchezo wa raundi ya pili wakiwa ugenini wakatoka sare ya bila kufungana.

Wydad Casablanca nao wamefuzu kuingia fainali baada ya kuwabwaga Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa jumla ya magoli 2-1, ambapo katika mchezo wa kwanza walishinda nyumbani magoli 2-1 na katika mchezo wa marudiano walitoka suluhu.

Kwa kawaida katika fainali ya Klabu Bingwa barani Afrika, timu zinazofanikiwa kufuzu hatua ya fainali hucheza michezo miwili, yaani nyumbani na ugenini, ndipo bingwa wa mashindano hayo huweza kupatikana.

Mchezo wa kwanza wa fainali sasa utafanyika Mei 24, takriban siku 17 zijazo, ambapo Timu ya Esperance de Tunis itakuwa katika Uwanja wa nyumbani wa  Olympic Stadium of Rades uliopo kusini – mashariki mwa Jiji la Tunis, nchini Tunisia, ikitarajiwa kuwa Esperance watakuwa mbele ya mashabiki wao 65,000 watakaoshuhudia mchezo huo.

Mchezo wa kuhitimisha fainali ya mwisho utafanyika nyumbani kwa Wydad Casablanca nchini Morocco katika dimba la Mohamed V, uwanja unaomudu kuchukua mashabiki 120,000.

Endapo timu ya Esparance itanyakua kombe kwenye michezo ya fainali, itakuwa miongoni mwa timu zilizofanikiwa kubeba ubingwa huo mara mbili mfululizo, baada ya msimu uliopita kuwafunga miamba ya Misri, Al-Ahly kwa jumla ya magoli 4-3.

Esperance de Tunis imekwisha kufanikiwa kutwaa taji la michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika mara tatu. Vilevile katika msimu huu timu hiyo imekuwa na rekodi za kutisha, kwani katika michezo kumi waliyocheza hadi kufika hatua ya  fainali walishinda michezo saba na wametoka sare michezo mitatu, hawajapoteza hata mchezo mmoja.

Rekodi hiyo ni tofauti na ile ya msimu wa mwaka 2017/2018. Katika msimu huo walipoteza michezo mitatu hadi walipotwaa taji la klabu bingwa barani Afrika.

Wydad Casablanca mwaka 2017 walitwaa taji la klabu bingwa kwa mara ya mwisho, baada ya kuwafunga miamba ya Misri, Al Ahly kwa jumla ya magoli 3-2.

Katika mchezo wa kwanza walianzia nyumbani na kushinda magoli 2-1 na katika mchezo wa marudiano walitoka sare ya 1-1.

Endapo Wydad Casablanca watafanikiwa kutwaa taji la klabu bingwa msimu huu, itakuwa mara yao ya tatu kutwaa taji hilo.

Kocha wa Wydad Casablanca, Fawzi Benzarti, anashikilia rekodi ya kuzipeleka timu anazozifundisha katika fainali za CAF, akiwa ameziingiza timu hizo mara saba tangu mwaka 1990.

Club Africain ya Tunisia aliingiza fainali mwaka 1990 na mwaka 2011, lakini hakufanikiwa kutwaa taji lolote katika michezo ya fainali hizo za Kombe la Shirikisho barani Afrika.  Timu nyingine alizowahi kuzipeleka fainali ni Esperance de Tunis mara mbili, mwaka 1994 na mwaka 2010, alishinda taji moja mwaka 1994.

Akiwa Etoile du Sahel alifanikwa kubeba makombe mawili ya shirikisho katika fainali za mwaka 2006 na 2015.

Katika michuano ya sasa, utumbukizaji mabao wa washambuliaji wa timu ya Wydad Casablanca umekuwa wa utata kwa kuwa anayeongoza katika kutikisa nyavu si kutoka safu ya washambuliaji wa timu hiyo, bali ni mlinzi wa kushoto, Mohamed Nahiri.

Nahiri, kwa mujibu wa mtandao wa taarifa za michezo wa www.supersport.com, amefunga mabao manne akifuatiwa na Walid El Karti mwenye magoli matatu, ambaye ni kiungo wa katikati (central midfielder) na Badi Aouk mwenye mabao mawili ni mshambuliaji wa pembeni (right winger).

Wachezaji wengine hatari katika timu ya Wydad Casablanca ni  Walid El Karti, ambaye ameifungia timu yake magoli hayo matatu katika michuano hii ya CAF. Wachezaji wengine hatari katika timu hiyo ni pamoja na washambuliaji Michael Babatunde, Salahedinne Saidi na Mohammad Ounajemi.

Esperance de Tunis si timu ya kupuuza, miongoni mwa wachezaji wake wa ‘kuchungwa’ ni pamoja na Taha Khenissi, huyu ni mshambuliaji, akiwa amefunga magoli 10 katika Ligi Kuu ya Tunisia na anaongoza kwa magoli kwenye ligi hiyo. Wengine ni winga wa kushoto, Anice Badri, ambaye ameifungia magoli matano timu hiyo kwenye Ligi Kuu ya Tunisia msimu huu.

Makocha wote wa timu hizo hupenda kutumia mifumo inayofanana uwanjani. Wote hupendelea mfumo wa 4-2-3-1.