Mara nyingi nimeandika kuhusu ardhi, hususan viwanja na nyumba. Katika kufanya hivyo, mara kadhaa nimejaribu kuwatahadharisha watu namna mbalimbali ya kisheria ya kuepuka kuingia katika migogoro ya viwanja na nyumba, hasa wakati wa kununua (wanunuzi). 

Nimewahi kueleza vitu vya msingi ambavyo mnunuzi anatakiwa kuvizingatia na kuhakikisha vipo katika mkataba wa ununuzi. Nikaeleza umuhimu wa kila kimoja na nikasisitiza kuwa atayekuwa amenunua ardhi na mkataba wake ukajaliwa kuwa na vitu hivyo, basi si tu atakuwa amefanya manunuzi bora, lakini pia atakuwa amefanya manunuzi yanayokubalika kisheria.

Ifike hatua watu waelewe kuwa migogoro mingi ya ardhi huanzia na kutokuwa makini kwenye manunuzi. Kutokupata ushauri wa kisheria, ikiwa ni pamoja na kutopitia hatua za msingi za kisheria kabla ya manunuzi, kuandikiwa mikataba ya manunuzi isiyokidhi vigezo vya kisheria, ikiwemo ile ya Serikali za Mitaa, ambayo hairuhusiwi kabisa kisheria ni kati ya sababu chache kati ya nyingi zitakazosababisha mtu aingie katika mgogoro. Leo nitaeleza hatua kadhaa za msingi sana ambazo mtu anayenunua ardhi anapaswa kuzipitia.

1.  Hatua tano za kufuata ununuapo nyumba/kiwanja 

Ziko hatua tano muhimu za kupitia pale unapokuwa katika mchakato wa kununua ardhi. Ukizipitia hatua hizi kwa umakini ni vigumu sana kujikuta katika mgogoro kuhusu kiwanja hicho siku za usoni.

Pia, hata kama utatokea mgogoro, kama umepitia hatua hizi kwa ukamilifu, ni rahisi kwako kushinda katika mgogoro huo. Hatua ya kwanza huitwa hatua kabla ya mkataba (pre contractual stage). 

Hatua hii ina mambo yake ya msingi na ya kisheri ambayo kuyafuata kwako kwaweza kukuweka mbali na hatari ya kununua ardhi yenye mgogoro au itakayokuingiza katika mgogoro. Hatua hii ndiyo nitakayoeleza kama msingi wa makala ya leo kama tutakavyoona. 

Kabla ya kueleza hatua hiyo ni vema pia nikazitaja hatua nyingine japo kwa ufupi. Hatua ya pili huitwa hatua ya mkataba (contractual stage). Hii ni hatua ya kupitia na kujiridhisha na mkataba wa manunuzi ikiwa ni pamoja na kuusaini.

Hatua ya tatu huitwa “pre completion stage”,  hatua ya nne huitwa hatua ya kumalizia (completion stage) na hatua ya tano na ya mwisho huitwa hatua baada ya kumalizia (post  completion  stage).

2. Usinunue nyumba/kiwanja bila kupitia hatua hii

Kama nilivyoeleza hapo juu, hatua nitakayojadili hapa huitwa hatua kabla ya mkataba au “pre contractual stage”.  Jambo kubwa ambalo huhusishwa katika hatua hii ni kufanya utafiti  wa kitaalamu uitwao “official search”.

Katika hatua hii mlengwa anayetaka kununua ardhi kupitia ofisi ya mwanasheria ataandika barua kwenda kwa Msajili wa Ardhi kumuuliza taarifa kamili za nyumba  au kiwanja anachotaka kununua. Msajili wa Ardhi atapekua katika kumbukumbu zake rasmi na kutoa majibu sawa na kile kilicho katika kumbukumbu zake.

3. Mambo  muhimu utakayouliza kwenye barua ya msajili

Kwanza, katika barua yako utahitaji kujua jina la mmiliki wa kiwanja/nyumba linalosomeka katika nyaraka za serikali. Hii itakusaidia kulinganisha jina la anayekuuzia na lile linalosomeka katika kumbukumbu za serikali. Kwa kujua jina tu utaepuka kununua ardhi kutoka kwa mtu ambaye si mmiliki halisi.

Pili, utahitaji kujua iwapo ardhi hiyo imewekwa kama dhamana popote katika taasisi za fedha. Kama imewekwa dhamana, basi taarifa zitaonyesha. Hii ni kwa sababu taasisi za fedha hutuma taarifa kwa Msajili wa Ardhi katika kila ardhi inayowekwa kwao kama dhamana.  

Tatizo la kununua ardhi iliyowekwa dhamana bila kujua ni aidha ukubali  kuingia hasara kulipa deni ili nyumba ubaki nayo au uwe mpole nyumba uliyonunua iuzwe upate hasara, iwapo itatokea deni halitalipwa.

Tatu, utaweza kujua iwapo ardhi hiyo ni ya wanandoa hasa iwapo wanandoa hao wana mgogoro. Hii  ni kwa sababu sheria humpa haki mwanandoa kuweka zuio katika ardhi ya familia iwapo mmoja wao ana wasiwasi mwenzake anaweza kuuza ardhi hiyo. 

Kwa hiyo, ikiwa taarifa kama hizo tayari zimepelekwa ardhi, basi utakapopitia hatua hii kabla ya kununua utaonyeshwa taarifa hizo, na hivyo kuepuka kununua mali ya familia, kitu ambacho ni kama kupoteza.

Nisisitize kuwa hatua hii ni muhimu sana, kwa kuwa ni hatua pekee ya kujiridhisha na uhalali wa ardhi unayotaka kununua. Nathubutu kusema kuwa usinunue  kiwanja/nyumba bila kupitia hatua hii.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG. 

By Jamhuri