Dini zote kuu hutaja siku moja ambayo maisha ya binadamu na matukio ya dunia yatafikia kikomo. Zinaonekana dalili kama tunakaribia huko.

Nimekumbuka hili niliposikia tetemeko la ardhi likitikisa Butiama. Dini za chimbuko la Abrahamu zinafundisha kuwa mwisho wa kila kitu utatanguliwa na matukio kadhaa: matetemeko ya ardhi, uvamizi wa nzige, magonjwa ya maangamizi, vita, na majanga mengine ya kila aina.          

Si jambo geni kuwapo matatemeko ya ardhi Butiama. Tupo jirani na mkondo wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki, linaloanzia kwenye Ghuba ya Aden na kushuka kusini mpaka Malawi. Ni kipande kikubwa cha Bara la Afrika chenye urefu wa kilomita 3,000 kinachomeguka kutoka Bara la Afrika kwa wastani wa milimita 6 – 7 kila mwaka. Baadhi ya matetemeko yanasababishwa na hatua hiyo ya kujimega.

Hiyo ni sayansi ya miamba, lakini kama ni mfuasi wa hizi dini na umeshuhudia ardhi inatetemeka unaweza kutoa tafsiri kuwa matetemeko ni ishara ya mwanzo wa mwisho wa yote.

Kutokea kwa makundi ya nzige ni ishara nyingine. Wimbi la sasa la nzige limesababisha hasara kubwa kwa wakulima na kuhatarisha uhakika wa kupatikana chakula kwa mamilioni ya watu katika mataifa ya Ethiopia, Somalia, Uganda, Sudan Kusini, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, na hata Pakistan.

Umoja wa Mataifa (UN) umetahadharisha kuwa kama hatua za haraka hazitachukuliwa, nzige hawa watasababisha baa la njaa ambao halijawahi kushuhudiwa katika nchi zilizoathirika. Tunaoishi kaskazini mwa Tanzania jirani na nchi ambazo tayari zimevamiwa tuna hofu kuwa si muda mrefu tutafikiwa na baa hili.

Lakini haihitaji kuamini maandiko ya dini kuhisi kuwa mwisho umewadia. Kwa mkulima ambaye anategemea mavuno ya ka-shamba kake kadogo kupata chakula na kugharimia mahitaji yake muhimu; kuteketezwa mazao yake na nzige hakuna tofauti na kiama.

Ishara zipo nyingi. Nyingine ni magonjwa ya maangamizi. Leo tunalazimika kupeana salamu za miguu kuepuka kuambukizwa homa ya Corona iliyoanzia China. Kufikia wakati wa kuandika makala hii homa hii ilikuwa imesababisha vifo vya watu zaidi ya 3,000 na kuambukiza zaidi ya watu 100,000 ulimwenguni.

Katika historia yapo magonjwa ambayo yameua watu wengi zaidi kuliko homa ya Corona, lakini inawezekana kabisa kuwa hofu inayoambatana na mlipuko huu wa sasa inachochewa zaidi na hisia kuliko hali halisi. Teknolojia imesaidia kusambaza taarifa za homa ya Corona – za uongo na za kweli – kwa kasi kubwa zaidi.

Kwa sasa tumempuuza mbu ambaye anaweza kuwa hatari zaidi kuliko virusi vya Corona. Kwa takwimu za mwaka 2018 mbu waliambukiza binadamu milioni 228 malaria na kusababisha vifo vya watu 400,000. Katika muktadha huu wa magonjwa ya maangamizi labda mbu angetajwa kuwa kiumbe hatari zaidi kuliko magonjwa ya mlipuko kama homa ya Corona, ambayo baadhi wanaamini kuthibitisha maandiko ya dini ya ishara za mwisho wa uhai na nyakati.

Siyo dini zote zinazohubiri kuwapo kwa mwanzo na mwisho wa uhai na matukio. Zipo dini zinazohubiri kuwa uhai na matukio ni mzunguko usiokuwa na mwisho. Viumbe vinazaliwa, vinakufa, halafu vinazaliwa tena. Hii ni imani ya baadhi ya dini za Kihindi. Kinachoonekana kufanana kwenye dini karibu zote ni kuwapo mzunguko wa maisha ya neema na vipindi vya majanga na maafa.

Na bila shaka binadamu wanakubaliana kwa jambo moja, kuwa vita si suala la neema. Vita katika dini nyingi huashiria mwisho wa dunia. Tukumbuke kuwa dini nyingi zimekuwapo kabla ya uvumbuzi wa karne ya 20 wa silaha za maangamizi; silaha ambazo zikitumika zitafyeka viumbe wote duniani, na bila kubagua kama ni waumini wa dini au la!

Makubaliano ya nchi zinazomiliki silaha za maangamizi yametuepusha na balaa hilo hadi sasa, lakini tishio la kuangamiza ulimwengu kwa silaha hizo bado halijatoweka; ingawa kila mara wababe wa nyuklia wakianza kukosana tishio hilo linapanda.

Sasa hivi tunashudia kuwa mataifa yenye silaha za nyuklia yametumbukia kwenye vita nchini Syria. Upande mmoja ni Urusi ambayo inaunga mkono serikali ya Syria; na upande mwingine ni makundi ya wapiganaji yanayoungwa mkono na Marekani na washirika wake.

Isitoshe, Uturuki, inayopakana na Syria kwa Kaskazini, imeivamia Syria ikipigana dhidi ya Wakurdi ambao wamekuwa wanaendesha mapambano ya muda mrefu dhidi ya Uturuki ili kuunda taifa lao huru. Zipo Iran na Saudi Arabia, nazo zikiunga mkono pande kinzani huko Syria. Nchi ya Qatar nayo inaunga mkono makundi yanayopigana dhidi ya serikali. Uingereza na Ufaransa zimetoa msaada kwa baadhi ya makundi hayo. Kikundi cha wapiganaji cha Hezbollah nacho kimeingiza wapiganaji kwenye vita hiyo kikiunga mkono majeshi ya serikali ya Syria. Kwa ufupi, vita ya Syria imevutia mataifa na makundi mengi.

Baadhi ya makundi ya wapiganaji wanaopinga serikali ya Syria wanaamini kuwa mji wa Dabiq au mji wa Amaq nchini Syria ndiyo itakuwa miji ambako vita kubwa itapiganwa kati ya majeshi ya uvamizi ya Wakristu dhidi ya majeshi ya kujihami ya Waislamu na kwamba itaisha kwa ushindi wa majeshi ya Waislamu na ushindi huo utakuwa mwanzo wa nyakati za mwisho.

Kuna hoja nzuri ya kuamini kuwa yanayotabiriwa, hasa kwa Syria, hayatatokea kwenye vita ya sasa, labda baadaye. Vitabu vinasema vita itakuwa kati ya Waislamu na Wakristu, lakini kinachotokea ni tofauti. Tunachoshuhudia ni Waislamu na Wakristu wanaungana upande mmoja kupigana dhidi ya Waislamu na Wakristu walioungana upande mwingine; upande mmoja ukiongozwa na Urusi na upande mwingine ukiongozwa na Marekani.

Zipo sababu nyingi za kuhoji kama kweli nyakati za mwisho zimewadia, kama inavyotabiriwa kwenye vitabu vya dini. Lakini haihitaji kuwa muumini wa dini yoyote kutambua kuwa tunaishi ndani ya nyakati ambazo binadamu hayuko salama hata kidogo.

Barua pepe:  [email protected]

Please follow and like us:
Pin Share