Bakwata ni kifupisho cha Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania, chombo cha kudumu kilichoundwa mwaka 1968 kuratibu, kusimamia na kuongoza shughuli zote za Waislamu nchini Tanzania (Tanzania Bara) kwa lengo la kutekeleza wajibu wa Waislamu wa kuendeleza na kuimarisha itikadi yao ya kidini, kukuza na kuimarisha ushirikiano, umoja na udugu miongoni mwao.

Umma wa Kiislamu popote ulipo una wajibu mkuu wa kuwa na ‘kauli moja’ inayotafsiri umoja na mshikamano baina yao kama Allaah Mtukufu alivyowaamrisha katika Qur’aan Tukufu sura ya 3 (Surat Ali-Imraan), aya ya 103 kuwa: “Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka.”

Kwa namna umma wa Kiislamu ulivyo na mapito yake ya kihistoria kumeshuhudiwa kuwepo kwa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu na uwepo wa wingi wa wafuasi na uchache miongoni mwa Waislamu katika nchi mbalimbali, hali iliyosababisha kuwepo “mamlaka za kidini” zinazozingatia “wengi wape” na “wachache wasikilizwe”.

Hali hii ndiyo iliyosababisha “mamlaka za kidini” zilizoundwa kufuata madhehebu ya Waislamu walio wengi kwa lengo la kuhakikisha umoja na mshikamano unakuwepo miongoni mwao na lengo la uwepo wa “kauli moja” inayotafsiri umoja na mshikamano baina yao linatimia. 

Vyombo mfano wa Bakwata vipo nchi mbalimbali na baadhi yake huwa sehemu ya serikali na sehemu nyingine huwa vyombo visivyo vya kiserikali vinavyotambuliwa na serikali kuwa “mamlaka ya kidini” zenye kuratibu, kusimamia na kuongoza shughuli zote za Waislamu katika nchi husika.

Katika baadhi ya nchi pamoja na uwepo wa vyombo mfano wa Bakwata, uwapo pia wizara za mambo ya Kiislamu na wakfu au wizara za wakfu (Endowment). Mfano wa mamlaka za kiserikali zinazoshughulikia mambo ya Kiislamu kama Bakwata katika Afrika ni pamoja na Baraza Kuu la Mambo ya Kiislamu na Wizara ya Wakfu nchini Misri, Wizara ya Wakfu na Mambo ya Kiislamu nchini Morocco, Wizara ya Mambo ya Kiislamu nchini Comoro, Kamisheni ya Wakfu nchini Kenya na Ofisi za Mufti, Kadhi Mkuu na Kamisheni ya Wakfu na Mali za Amana, Zanzibar.

Mamlaka zisizo za kiserikali zinazotambuliwa kuwakilisha sauti ya Waislamu katika nchi ni pamoja na Mabaraza Makuu ya Waislamu katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika nchi zote hizi, Bakwata ndicho chombo pekee, kwa mujibu wa Katiba yake, kilichotoa fursa kwa Waislamu kushiriki moja kwa moja katika mchakato wa kuchagua asilimia kubwa ya viongozi wake kwa kuwapa Waislamu wote haki ya kushiriki katika uchaguzi wa msingi kabisa wa ngazi ya msikiti kwa masharti mawili tu ya kuwa mkazi wa eneo husika la msikiti na kuswali katika msikiti husika na kuchagua wawakilishi wa kushiriki katika chaguzi za ngazi za kata, wilaya na mkoa. Bakwata imetoa uanachama wa moja kwa moja kwa Waislamu wote wanaoishi katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Ili kuutekeleza vema wajibu wa kuratibu, kusimamia na kuongoza shughuli zote za Waislamu nchini, Katiba ya Bakwata Ibara ya 3 hadi ya 5 zikaonyesha Hadhi ya Chombo hiki kama ifuatavyo:

1. Bakwata litakuwa ndiyo chombo pekee cha kuongoza Waislamu na litakuwa na kauli ya mwisho katika kulinda, kutetea na kueneza Uislamu na nadharia yake nchini kwa mujibu wa Qur-aani na Sunna. 

2. Bakwata litakuwa na uwezo wa kuanzisha au kuidhinisha kuanzishwa matawi na taasisi zake katika misikiti, wilaya, mikoa na taifa kwa lengo la kutekeleza madhumuni yake. 

3. Bakwata litakuwa ndiyo chombo cha kuunganisha Waislamu wa Tanzania na Waislamu wenzao, vyombo vingine vya Kiislamu nchini na nje ya nchi. 

4. Msingi wa maongozi yote ya Baraza Kuu na utekelezaji wake na shughuli zake zote mbalimbali utakuwa wa kitabu cha Mwenyezi Mungu, Qur-aani na Sunna za Mtume Muhammad (S.A.W).  

Kadhalika, Katiba ya Bakwata imeweka madhumuni yanayoakisi masilahi ya Uislamu na Waislamu nchini kama yanavyobainishwa katika Ibara ya 9 (1-17) kuwa:

1. Kusimamia, kufungua, kujenga, na au kusaidia na kuendesha vyuo vya dini na elimu ya dunia kwa Waislamu wa Tanzania, na kutoa uwezo wa elimu ya juu kwa wanafunzi wa Kiislamu. 

2. Kusimamia na kutetea haki za msingi za Waislamu nchini, na kukemea mambo yanayoleta kero kwa Waislamu.

3. Kuanzisha na kuhimiza Tabliigh ya dini na kueneza dini katika lugha ambazo Bakwata limezitaja katika Katiba hii. 

4. Kusimamia malezi na maadili mema kwa vijana wa Kiislamu na Waislamu kwa ujumla. 

5. Kuwahimiza na kuwasaidia Waislamu nchini kuanzisha miradi na shughuli za uchumi na uzalishaji mali kwa lengo la kuupiga vita umaskini. 

6. Kufungua, kujenga, kusimamia, na au kusaidia kuendesha misikiti, mali za wakfu, huduma za afya na matibabu kama Bakwata litakavyoona inafaa. 

7. Kusimamia, kuhimiza, kuimarisha, na au kusaidia kuweka mipango ya ukusanyaji, utunzaji na utumiaji wa Zakka na Sadaka kwa kutimiza amri ya Mwenyezi Mungu, na katika kuinua dini na maendeleo ya Waislamu. 

8. Kusimamia, kuendesha, na au kusaidia kuendesha mipango ya utunzaji na malezi kwa watoto yatima, watu wasiojiweza na maskini. 

9. Kusimamia, kuhimiza, na au kuweka taratibu na mipango ya ‘Hijja na Umra’ na huduma zake. 

10. Kusimamia, kuendesha, na au kusaidia kuweka mipango ya Ndoa, Talaka,  Mirathi na haki ya kurithi mali za Waislamu zilizoachwa bila ya wenyewe. 

11. Kuweka mipango ya kusimamia utekelezaji wa Ibada za Kiislamu na sherehe za sikukuu za kidini, kama siku ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W), sikukuu za Idd, sikukuu ya Mwaka Mpya na inapendekezwa kuwa siku hiyo ya mwaka mpya wa Kiislamu iwe siku ya mapumziko kitaifa. 

12. Kutoa au kupokea misaada kwa ajili ya maendeleo, kudumisha mila na utamaduni wa Kiislamu, na ustawishaji wa hali njema za Waislamu wa Tanzania. 

13. Kuweka uhusiano na ushirikiano kati ya Bakwata na Waislamu wa nchi nyingine, na kuishi kwa amani na watu wa dini mbalimbali nchini Tanzania. 

14. Kukopa toka Benki au taasisi za fedha za ndani au nje ya nchi, kukopesha, kununua, kuuza, kuhamisha, kuondosha, kuweka rehani, kujenga, na au kuwa na haki juu ya ardhi kwa ajili ya kutimiza shabaha na madhumuni ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

15. Kuanzisha Miradi ya Uchumi na uzalishaji mali na kuwekeza katika taasisi za rasilimali. 

16. Kupokea Sadaka na Misaada ya vitu mbalimbali kutoka kwa wafadhili wa ndani na nje ya nchi, kwa madhumuni ya kuendeleza shughuli za Bakwata.

17. Kukagua na kupokea taarifa kutoka katika taasisi zote za Kiislamu nchini.

Baada ya ufafanuzi huu, nihitimishe kwa kusisitiza kuwa Bakwata ni nyezo ya kuwaleta pamoja Waislamu kufikia kuwa na “Kauli Moja” na ni jukwaa la kujiletea maendeleo kwa kutekeleza kwa kauli na vitendo madhumuni 17 yaliyoainishwa katika Katiba ya Bakwata na wala Waislamu hawana haja ya kujikusanya na kuanzisha “Umoja wa Waislamu wa kata fulani” na kuhangaika kuusajili umoja huo wa kata, wakati muundo wa Bakwata tayari umeshawapa fursa ya kupata uongozi wao wa kata unaojumuisha Sheikh wa Kata na Baraza lake la Masheikh kwa ajili ya kushughulikia mambo ya dini na kuchunga nidhamu ya Uislamu; Mwenyekiti na Halmashauri yake ya Kata kwa ajili ya kushughulikia mambo ya Utawala na Fedha.

Wajibu wa Waislamu nchini ni kuifanyia kazi falsafa ya Mheshimiwa Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Bin Zubeir Bin Ally Mbwana ya “Jitambue, Badilika na Acha Mazoea” na kuitikia wito wake wa kuunganisha nguvu za masheikh na wataalamu wetu mbalimbali katika kutafsiri kwa vitendo madhumuni 17 ya Baraza badala ya kufikiria kuunda “taasisi mpya” kila uchao za kutekeleza kazi zilezile zilizoanishwa kupitia madhumuni ya kuundwa kwa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania. 

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata). 

Simu: 0713603050/0754603050

By Jamhuri