Kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kila mwaka inapofika Oktoba 14, sasa ni fasheni.

Kila Mtanzania, mwizi, fisadi, bazazi, mlafi, mla rushwa, myonyaji, jangili, jambazi, fedhuli, mwanasiasa, kiongozi wa Serikali, mwanamichezo (hata ile ambayo Mwalimu hakuwahi kuijua), mkulima, mfanyabiashara, bepari (mweupe, mweusi, chotara) na hata yule aliyempiga Nyerere, mwanafunzi, mwalimu – ukifika wakati huu, wote santuri yao ni moja; wanamuenzi Baba wa Taifa.

Wote wanajidai kuwa wanamuenzi Mwalimu Nyerere aliyeaga dunia Oktoba 14, 1999 huko Uingereza katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, kwa mbwembwe, vibweka na kila aina ya vituko kuwaghilibu Watanzania kwamba bado tupo wamoja.

Mwalimu Nyerere ni kiongozi anayekumbukwa na mamilioni ya wanyonge na walalahoi wa Tanzania na Afrika, si kutokana na maneno yake matamu tu; bali  kutokana na matendo yake mema, na ya kutukuka kwa nchi yake na wananchi wake.

Hakuna Mtanzania mwenye nia njema na nchi yake anayemkumbuka Mwalimu Nyerere kutokana na Kiswahili chake safi na sanifu tu, lakini zaidi kutokana na falsafa yake ya kuheshimu utu, ubinadamu na kuhakikisha kila Mtanzania, Mwafrika na mwanadamu yeyote, madhali mahitaji yake ya msingi yanafanana, yaani kuvuta hewa, kula, kuvaa na kuwa na mahali pa kuishi, anaheshimiwa na kupewa haki stahili.

Mwalimu, kama kiongozi wa nchi asiye na tamaa wala uchu wa mali – kama walivyo viongozi wengi hivi sasa – hakuwahi kufikiria kujimegea mashamba na sehemu ya ardhi kwa ajili yake, wala kutumia rasilimali za nchi hii kwa manufaa yake binafsi na familia yake, ndugu na jamaa zake na hata marafiki zake wa karibu.

Angetaka, pengine leo hii kina Makongoro wangekuwa sawa na wenzao kama Uhuru Kenyatta, kwa kuwa na ardhi kubwa na yenye rutuba kuliko wazalendo wengine wa nchi na wenye kumiliki rasilimali zenye utajiri wa kupindukia kwa sababu tu walizaliwa au kukulia ikulu.

Mwalimu angeweza kukiuka taratibu, na hata kuvunja sheria kama angetaka, ili kujinufaisha yeye na marafiki zake au hata nduguze, kama tunavyoshuhudia leo kwa viongozi wetu, lakini kwa sababu aliamini katika kuheshimu sheria tulizojiwekea, hakufanya hivyo na daima alikuwa mkali kwa yeyote aliyekiuka masuala hayo ya msingi kwa nchi na watu wake.

Mifano ipo mingi, lakini ule wa waziri aliyekula mlungula akahukumiwa jela miezi 12 na viboko 24; kumi na viwili achapwe wakati anaingia na vingine 12 wakati anatoka akamwoneshe mkewe, unatosha tu kudhihirisha ujasiri wa Mwalimu katika kusimamia utawala wa sheria bila kujali cheo wala hadhi ya mhusika. Je, leo kuna anayethubutu hata kukemea uozo huo japo kwa sauti ya chini?

Lakini leo, dhana na maana ya uongozi, baada ya kifo cha Mwalimu miaka 14 iliyopita imebadilika mno, na imepata tafsiri nyingine inayowaumiza na kuwakandamiza mamilioni ya wanyonge huku mabepari uchwara wachache wakifaidi pepo, kwa mbwembwe nyingi, ingali bado wako duniani.

Wanasiasa sasa wanakimbilia bungeni na kwenye mabaraza ya halmashauri za wilaya, miji, manispaa na jiji, si kwa nia ya kuwatumikia Watanzania wajikwamue kutoka lindi la umaskini, maradhi na ujinga, bali kujinyakulia — kwa haraka na kwa wingi kadiri inavyowezekana — utajiri wa mali na rasilimali  kwa kutumia migongo ya walalahoi.

Wengi, kama si wote, wanatumia kila mbinu inayowezekana — ikibidi hata kuua — kuhakikisha wanafikia katika mrija huo wa unyonyaji na uporaji wa wazi wazi, tena mchana kweupe, wa mali za wananchi ambazo Mwalimu alizitunza kwa faida ya vizazi vya zamani, vya sasa na hata vile vijavyo.

Kwa kasi ya uporaji rasilimali za wananchi inavyaoendelea kwa visingizio vya uendelezaji na uwekezaji, hakuna shaka baada ya muda mfupi ujao nchi hii haitabaki na kitu chochote zaidi ya mashimo ya kumbukumbu kwamba tulikuwa na kila aina ya madini, mafuta na hata gesi asilia.

Sasa wanafiki na wazandiki hao wanaposhika matarumbeta ya kumuenzi Baba wa Taifa, wanataka kutuzuga nini? Wanataka kutuambia kwamba Watanzania tu vipofu na viziwi kiasi kwamba hatuoni wala hatusikii kinachoendelea ndani ya nchi yetu?

Wateule wachache wanaojaribu kufuata sheria, kanuni na taratibu kuhakikisha mali na utajiri Watanzania waliopewa na Mwenyezi Mungu vinawafaidisha wao, watoto wao na vizazi vyao, wanapigwa vita kutoka kila kona, tena kwa kutumia nguvu na rungu la kutisha na hata kutolewa kafara kama ilivyotokea kwa akina Edward Moringe Sokoine.

Katika Jiji letu la Arusha, na hasa kwenye Halmashauri ya Jiji, mambo ni yale yale. Ulaji wa kutisha unafanywa mchana kweupe kiasi kwamba wengine wanalewa madaraka na kujisahau kama wameteuliwa kuhudumia umma wa watu.

Baadhi ya madiwani na watendaji wa halmashauri, wakishirikiana na baadhi ya wafanyabiashara, wameligeuza jiji letu, linalosifika eti ni la kimataifa, kuwa shamba la bibi yao kwa kuvuna bila kutoka jasho, mamilioni ya shilingi huku ustawi wa Arusha ukizidi kuporomoka kwa kasi ya kutisha.

Cha ajabu, anapoingia mtendaji mzalendo na mwenye kutaka kurekebisha mambo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, kama alivyofanya Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake, anageuzwa kuwa adui nambari moja na kupangiwa njama, mikakati ya kumwondoa au ikiwezekana hata kummaliza kabisa. Eti hawa — majahili — ndiyo walio mstari wa mbele kumuenzi Mwalimu Nyerere, kweli tutafika?

Hawa madiwani na watendaji wa halmashauri wanaompiga vita Sipora Liana ambaye, kwa dhati kabisa, anatekeleza sera za Mwalimu Nyerere na chama cha ukombozi cha Tanganyika African National Union (TANU), wanajisahau kuwa wamefika hapo kutokana na kura zetu na kwamba shahada za kupigia kura bado tunazo na tutazitumia vizuri ‘kuwashughulikia’ wakati ukifika.

Tunawaambia kuwa heri ya akina Sipora wanaomuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo vitakatifu kuliko hawa waroho. Uroho wao utawafikisha pabaya siku moja!

Mwandishi wa makala hay ni mkazi wa Arusha. Anapatikana kupitia:

[email protected]

0754 299861

By Jamhuri