Hoja ni kutii sheria, si kufuta kauli

Hivi karibuni niliandika makala nikizungumzia kauli za wanasiasa na athari zake kwa umma. Nilizungumza kuhusu kauli zinazochochea vurugu, migongano na kuleta chuki na uvunjifu wa amani.

Lengo la makala hayo lilikuwa kuwataka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliosema wana ushahidi kuhusiana na mlipuko wa bomu jijini Arusha, wauwasilishe kwenye vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake. Hata hivyo, hilo tuviachie vyombo husika, nina imani jibu litapatikana.

 

Kilichonisukuma kuandika makala hayo ndicho pia kilichonishawishi kuandika makala haya leo, lakini mtazamo wangu utakuwa tofauti na wengi waliosoma makala yaliyopita. Wanaweza kuwa na maswali mengi tu yatakayotokana na haya niliyokusudia kuyasema leo.

 

Hivi karibuni Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa kauli ambayo imeleta hisia tofauti miongoni mwa watu wa kada mbalimbali. Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali kudhibiti vurugu zinazotokea hapa nchini.

 

Pengine kwa matumaini kuwa kwa atakuwa ameleta suluhu ya kukomesha vurugu, Waziri Mkuu alisema kwamba wanaokaidi amri ya Jeshi la Polisi wanastahili kipigo kwa sababu hakuna namna nyingine ya kukabiliana nao zaidi ya kuwapiga. “Muwapige tu, tumechoka”, alisema bungeni mjini Dodoma.

 

Kauli yoyote inayotolewa bungeni na Waziri Mkuu ama kwa kuagizwa, au kwa fikra zake binafsi, ni kauli ya serikali, si kauli ya Mizengo Pinda yeye kama mtoto wa mkulima, la hasha! Hivyo, tunapomtaka Pinda afute kauli na kuwaomba radhi Watanzania, maana yake ni kuitaka serikali ibadili kauli ama kwa kupitia Waziri Mkuu huyo mwenyewe, mtu mwingine, au chombo chochote chenye mamlaka hayo.

 

Binafsi nilipomwona na kumsikia Pinda kwa kupitia runinga nilipigwa na butwaa! Nikajiuliza, “Huyu ndiye mheshimiwa Pinda niliyemzoea kumuona na kumsikia akijibu hoja na maswali mbalimbali ya wabunge kwa ustadi na umakini wa hali ya juu? Je, mbona amekatishwa tamaa mapema na matukio yanayoendelea na kutafuta suluhisho hasi? Je, ni kweli amechoshwa na vurugu, au majukumu aliyokabidhiwa?

 

“Je, yeye kama Mtendaji Mkuu wa Serikali alishindwa nini kukumbuka kuwa kuna sheria ambazo yeye anazisimamia na ambazo haziendani na kauli yake? “Je, ni kweli polisi na vyombo vingine vya usalama vimeshindwa kudhibiti kwa njia zilizopo mpaka wapewe kibali na uhalali wa kutembeza kipigo kwa raia?”

 

Maswali yapo mengi na ndiyo maana watu wa kada mbalimbali wameibuka na kuanza kulaani kitendo cha Waziri Mkuu kutoa kauli ile bungeni, ambayo naamini kwa sasa iko kwenye kumbukumbu za kibunge (Hansad). Lakini pamoja na yote hayo, hoja yangu ya msingi ni hii: Je, kwa kumshinikiza Waziri Mkuu afute kauli ya serikali ni kweli tutapata suluhisho la vurugu hapa nchini? Je, ni nani anayetakiwa kutii sheria – ni raia pekee au hata vyombo vya usalama?

 

Kwa mtazamo wangu, sidhani kwamba Pinda kwa kufuta kauli yake tutakuwa tumepata mwarobaini wa vurugu hapa nchini. Lazima tutambue kuwa utii wa sheria bila shuruti ndiyo suluhisho pekee la kuondoa vurugu, na wanaotakiwa kutii sheria za nchi ni sisi wote, raia na vyombo vyote vya usalama.

 

Ni imani yangu kuwa polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kama kweli vinazitii sheria zilizopo, hawataweza kuwapiga raia bila sababu zozote, kwani wakithubutu kufanya hivyo watakuwa wameshindwa kutii sheria zinazowataka kuwakamata wahalifu na kuwafungulia mashitaka bila kuwadhuru kwa namna yoyote ile.

 

Lakini ni vema tukajiuliza; Je, hakuna raia wanaokaidi amri halali ya serikali na wanapotakiwa kutii huanzisha vurugu? Mathalan, katika vurugu za Mtwara, kuna watu walichoma magurudumu na kuyaweka barabarani, nyumba na magari viliteketezwa kwa moto na baadhi ya watu kujeruhiwa.

 

Kuna matukio mengi ya kuchoma makanisa, vituo vya polisi, na hata kutumia mawe kutaka kuwadhuru walinda usalama wa raia na mali zao –  polisi. Sasa katika hali ya kawaida, mtu aliyejihusisha, mathalan na uchomaji nyumba za watu hufanywa nini?

 

Waziri Mkuu angetumia neno “wadhibitiwe kisheria” asingepata upinzani mkubwa. Lakini “wapigwe”; watu wanajiuliza, watapigwaje? Je, risasi zimeruhusiwa kutumika au viboko? Lakini kwanini Watanzania wamefikia hatua hii leo na kuona kuwa mleta vurugu na kusababisha madhara kwa wenzake asipate mkong’oto?

 

Hii inatokana na dhana iliyojengeka miongoni mwa watu kuwa polisi wapo kwa ajili ya kuwalinda walio juu. Polisi ni jeshi la kunyanyasa raia tu. Hivyo, panapotokea vurugu, uhasama unazuka baina ya raia na polisi. Kila kundi litajihami kwa mbinu zake. Sasa utii wa sheria bila shuruti unatoweka, baadhi ya raia wataanza kurusha mawe, polisi nao wataamua kutumia silaha walizonazo ili walinde uhai wao. Hapa tena tujiulize: Je, ni kweli hakuna polisi wanaopata madhara wakiwa katika harakati za kudhibiti vurugu? Je, ni nani mwanzilishi wa vurugu?

 

Vurugu, kwa mtazamo wangu, huanza pale watu wanapotakiwa kutofanya kile kisichotakiwa kisheria kukifanya kwa wakati huo. Mathalan maandamano yasiyo halali; ambayo hayaruhusiwi kisheria, mikusanyiko yoyote isiyo halali. Sasa tiba ya kutatua tatizo lililopo kwa sasa kati ya raia na polisi ni kuhakikisha kila mmoja anaheshimu na kutii sheria tulizojiwekea wenyewe kupitia Bunge letu. Lazima kila mmoja wetu ahakikishe anafanya mambo kwa kuzingatia sheria za nchi.

 

Tuepuke viashiria vyovyote vinavyoweza kusababisha upendo, mshikamano, amani na utulivu kutoweka nchini. Tuepuke kauli zenye mtazamo usio na matarajio mema kwa taifa letu. Viongozi wajaribu kuelezana, hususan kuhusu kauli mbalimbali na kutathmini athari zake kabla ya kunena. Siku zote kauli huweza ama kutujenga, au kutubomoa.

 

Waziri Mkuu ni mtendaji mkuu wa shughuli za serikali. Ndiye kiranja wetu. Sasa kiranja anapoharibu, walio chini wataharibu zaidi. Tujiulize nani alifuta kauli hizi; wanaowaua albino nao wauawe na liwalo na liwe wakati wa mgomo wa madaktari. Kama kauli hizi zilifutwa au zilifutika zenyewe, basi hata hii ya “wapigwe” itafutika kwa misingi ya sheria tulizojiwekea. Sitarajii polisi kwenda kinyume na sheria za nchi. Viongozi na raia wote hatuna budi kutii sheria tulizojiwekea sisi wenyewe.

 

Viongozi wakumbuke kuwa wamepewa dhamana na wananchi wote bila kujali itikadi  zao. Wananchi wajaribu kuepuka kutenda mambo bila kutafakari athari zake, hususan wanapokuwa katika mikusanyiko, hasa ya kisiasa.

 

Kila mmoja kwa nafasi yake lazima ajiulize ni nini anachotakiwa kukifanya nchi iweze kusonga mbele. Neno likitoka limetoka. Waswahili walisema: Chunga ulimi wako! Kwa sababu madhara yake ndiyo hayo tunayoyajadili leo hii. Sheria ni msumeno. Hii ndiyo Tanzania ya leo, ya kesho itakuwaje?

 

[email protected]

0763 – 400283