Hongera Wizara ya Kilimo, hongereni wapambanaji

Wizara ya Kilimo imezuia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) iliyopo Makutupora, Dodoma kuendelea na utafiti wa mbegu za GMO.

Uamuzi huo ni majibu kwa kilio cha wazalendo waliojitokeza kupaza sauti kuhoji uhalali wa chepuo linalopigwa ili kuruhusu mbegu hizo kuanza kutumika nchini.

Wasomi, wakulima na watu wa kada mbalimbali wamejitokeza kueleza kisayansi madhara ya mbegu za GMO yakiwamo magonjwa ya saratani yanayosababishwa na ulaji wa vyakula vilivyotokana na mbegu hizi.

Jambo jingine baya lililoelezwa kwa uwazi mkubwa kuhusu mbegu za GMO ni athari zake kwa wakulima, hasa wakulima wadogo, kwani kwa kuzitumia watakuwa hawana namna nyingine, isipokuwa kununua mbegu kila watakapohitaji kulima mazao fulani.

Kwa miaka mingine wakulima, hasa wadogo, wamekuwa wakilima, wakivuna na kutenga mbegu kama za mahindi, mihogo, maharage na kadhalika ili kuzitumia kuzalisha chakula au mazao mengine. Kwa GMO, maana yake ni kwamba unafuu huo hauwezi kuwapo, kwani mkulima hulazimika kwenda kununua mbegu kila anapotaka kulima.

Wasomi wameeleza bayana kuwa kuruhusu mbegu za GMO maana yake ni kuruhusu ukoloni mwingine hatari mno. Hizi ni mbinu za mabeberu ambao kwao wanachokiangalia ni faida zaidi kuliko madhara na adha zinazowapata watu maskini.

Tunaipongeza serikali tukiamini msimamo huu haukutolewa kwa bahati mbaya, bali ni kwa kuzingatia masilahi marefu na mapana ya wananchi na taifa letu.

Tunatambua kuwa msimamo wa serikali ni mwanzo wa vita mpya. Mabeberu kwa kuwatumia vibaraka wao waliojaa ndani na nje ya Tanzania hawafurahi. Wamenuna. Wataanza kupiga kelele, hata kuhimiza mikakati ya Tanzania kutendwa kwa sababu tu tumeukataa ubeberu huu.

Hii ni vita halali inayopaswa kupiganwa na kila Mtanzania mpenda nchi hii na Bara la Afrika. Hatutarajii kuwaona au kuwasikia vibaraka wa mabeberu wakishiriki kuihujumu serikali na wakulima makabwela wa Tanzania.

Hatuhitaji mbegu za GMO kwa sababu kama ni uzalishaji wa chakula, tunazalisha hadi ziada. Mahindi yanakosa wanunuzi. Korosho ziko tele. Zabibu zinaoza mashambani. Shida ya Watanzania ni masoko, kamwe si mbegu.

Tunaipongeza Wizara ya Kilimo na serikali kwa jumla kwa kusimama kidete kupinga sumu hii ya GMO kuanzishwa na kuenezwa nchini mwetu. Sote kwa pamoja tuungane kuhakikisha msimamo wa serikali unakuwa ndio msimamo wa Watanzania wote bila kujali tofauti zetu.

8974 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons