Habari tuliyoipa umuhimu wa pekee kwenye toleo hili inahusu mkwamo wa ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi ya mikoani eneo la Mbezi Luis, Dar es Salaam.

Tumeeleza namna vitendo vya rushwa vinavyotishia mradi huo mkubwa kwenye sekta ya usafiri wa mabasi nchini na katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Ni jambo la bahati mbaya kuona kuwa bado tunao baadhi ya watendaji serikalini wenye ujasiri wa kukwamisha mambo makubwa kama haya kipindi hiki cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Tunayo mifano mingi ya mkwamo wa maendeleo uliosababishwa na mivutano isiyokuwa na tija kwa umma. Mara nyingi mikwamo ya aina hii imesababishwa, ama na rushwa, hujuma, au urasimu usiokuwa na tija.

Maendeleo katika ulimwengu wa leo yanakwenda kwa kasi kubwa mno. Tanzania, kama yalivyo mataifa mengi ya Afrika tumekwama kimaendeleo kwa sababu za rushwa na urasimu usiokuwa na maana yoyote.

Tunatoa mwito kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha zinaingilia kati ujenzi wa stendi hii ya mabasi ili iweze kukamilika mapema, hivyo kusaidia kuboresha maisha ya watu na kukuza uchumi wa taifa letu.

Tunawaomba watumishi wenye mapenzi mema kwa taifa letu kutosita kutoa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyokwamisha maendeleo.

Kwa bahati mbaya wapo viongozi wakubwa waliopewa mamlaka kisheria kushughulikia kero kama hizi, lakini kwa kuwa wamezoea kusukumwa kufanya kazi, wako kimya.

Hatutarajii kuona suala hili akisukumiwa rais kulishughulikia ilhali zipo mamlaka zenye nguvu kisheria za kumaliza mkwamo huu.

Pia tunashauri wale wote wanaohusishwa na hujuma hii wawajibishwe kwa mujibu wa sheria ili kutoa salamu kwa wengine wenye mawazo au matamanio ya aina yao.

Tunapaswa kusimama imara kuhakikisha tunajiletea maendeleo kwa kasi ili kwenda sambamba au hata kuwapita washindani wetu wakuu katika ukanda huu wa Afrika.

Muda wa kubembelezana kwa mambo ya maendeleo haupo tena. Tusikubali kucheleweshwa kwa sababu ya tamaa za wachache wasioitakia mema Tanzania. Wananchi wanachotaka kuona ni matokeo ya kazi zinazofanywa kutokana na kodi zao.

Tunashauri zabuni ya ujenzi wa stendi hii itazamwe kwa jicho pevu ili kuuokoa mradi huu muhimu kwa maendeleo ya taifa letu. Rushwa ni kikwazo kikubwa mno kwa maendeleo ya nchi. Wananchi wote tushiriki kwa pamoja kuipiga vita.

Please follow and like us:
Pin Share