DAR ES SALAAM

ALEX KAZENGA

Watanzania tulio wengi tu wazuri kuzungumza, lakini kwenye kutenda baso tunasuasua.

Linapokuja suala la kutenda mipango tunayozungumza huwa tunakwama-kwama.

Sijajua nini tatizo na kwanini tuwe kwenye hali hiyo au kwanini hatupati suluhisho la kudumu.

Nikiutazama mradi wa Mabasi ya Mwendokasi (BRT) unaosimamiwa na UDART katika Jiji la Dar es Salaam, napata mtanziko.

Kwa namna usafiri huu unavyoendeshwa siku hizi ni ushahidi tosha kwamba uwezo wetu wa kuendesha mambo unapaswa kubadilika.

Huenda si mimi pekee ninayekosa raha kila ninapotumia usafiri huu, na huenda si mimi tu ninayefoka kimoyomoyo huku nikizihoji fikra zangu kwa hasira.

Hali ya kupigana vikumbo na kuvutana mashati wakati wa kuingia kwenye usafiri huo na kusafiri huku nikiwa nimesimamia kucha kwa sababu ya kubanana kupita kiasi inachosha.

Kinachonifanya nikose uvumilivu kuhusu usafiri huu ni jinsi huduma ya tiketi inavyotolewa katika vituo vyake kwa sasa.

Hakuna tofauti na daladala za kawaida zinazosafirisha abiria katika maeneo mengine ya jiji.

Ukiwa kwenye daladala unaweza kusikia habari za kondakta akilalamika kukosa chenji kwa abiria wake.

Unaweza kusikia kondakta akimgombeza abiria kwanini anatoa hela kubwa wakati yeye hana chenji.

Hali hiyo kwa sasa imejitokeza kwenye vituo vya mwendokasi. Wahudumu wanalalamika kukosa chenji za Sh 50 na Sh 100.

Ni jambo la kawaida kwa abiria sasa kusimama kwenye dirisha la tiketi akimsubiri apelekwe chenji.

Kitendo hicho kinaibua manung’uniko kwa abiria wengi kiasi cha kuibua hisia za malalamiko juu ya mfumo mzima wa utoaji wa huduma za mwendokasi.

Mbali na hali hiyo, kitendo cha sasa hivi ambacho wahudumu huruhusu abiria kupita kwa kuchana tiketi nacho kinatia dosari ubora wa huduma hii ya mwendokasi.

Nashauri wanaosimamia mradi huu mkubwa waone umhimu wa kurudisha mfumo wa kutumia mashine kuruhusu abiria kupita kwenye vizuizi wakati wakiingia na kutoka.

Pamoja na kasoro nyingine za abiria kukaa kwenye vituo kwa muda mrefu, inatosha kuwaamsha wasimamizi wa mradi huu na kuona umuhimu wa kuusimamia ipasavyo.

Lakini hali inavyoonyesha ni kama UDART ambao ni wasimamizi wakuu wa mradi huu bado hawajajua shida tunazopata sisi abiria.

Utaratibu umevurugika mno, lakini watu wanaotakiwa kujitokeza na kuweka mambo sawa ni kama wameridhika na kukubali mambo yajiendeshe kama yalivyo sasa.

Mimi nasema hata kama kuna mabadiliko yanatekelezwa katika kipindi hiki ni mhimu viongozi wanaosimamia mradi huu wakabuni mbinu za dharura za kuendesha huduma hii ili kuondoa adha kwa wasafiri.

Ni vyema kuusimamia mradi huu vizuri ili wale wanaowaza kufadhili miradi mingine inayofanana na huu katika maeneo mengine wasione kama tumeshindwa.

Ikimbukwe kuwa mradi wa kuondoa kero za usafiri katika Jiji la Dar es Salaam ni miongoni mwa miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Mradi huu kwa kipindi cha kwanza umehusisha njia za Kimara, Morocco, Kivukoni na Gerezani. Mipango ipo ili uenee hadi njia za Gongolamboto na Mbagala.

Hivyo ni vyema mradi huu uliopo kwa sasa ukasimamiwa vema ili kuwatia hamasa wafadhili wa miradi hii ili walete fedha bila kusita.

MWISHO.

1142 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!