KATAVI

Na Walter Mguluchuma

Kila msiba una mwenyewe. Msemo wa wahenga unaolenga kuweka msisitizo katika umiliki wa suala lolote lile; liwe baya au zuri.

Kupuuza msemo huu na mingine kadhaa iliyobeba ujumbe mzito ni kujitakia balaa na aghalabu, ni kujicheleweshea maendeleo na hata mafanikio katika jambo lako.

Kuna kila dalili kwa maofisa wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi kuupuuza msemo huu, hivyo kusababisha kutofahamika sawasawa kwa uzuri wa hifadhi yenyewe; moja ya hifadhi kubwa na za kuvutia sana nchini.

Kwa hakika wataalamu hawa wa uhifadhi wanapaswa kukaa chini na kujipanga ili kuwatendea haki wenyeji wa mikoa ya Katavi na Rukwa wenye ndoto za kuiona hifadhi ikiwanufaisha wao na taifa zima.

Hifadhi ya Katavi inakaribia umri wa ‘utu uzima’ sasa, ina nusu karne tangu ilipoanzishwa. Kwa nini bado haijafahamika na kuuzwa kitaifa na kimataifa?

Bila shaka ni kutokana na kuwapo kwa watendaji au maofisa wasioitakia mema; wenye malengo binafsi na hata kuwa na dalili za chuki kwa mafanikio ya hifadhi hii na watu wanaoizunguka.

Mmoja wa maofisa hao (JAMHURI linahifadhi jina lake kwa kuwa halikumpata na kuzungumza naye kwa wakati) anatajwa kutotoa ushirikiano stahiki kwa Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi, alipoitembelea hifadhi akiongozana na waandishi wa habari na wanachama wa Katavi Press Club wiki chache zilizopita.

“Ninaamini fursa hii (ya waandishi wa habari kutembelea hifadhi) ingepaswa kuchukuliwa kwa uzito wa aina yake na maofisa wa Katavi tofauti na walivyofanya,” anasema Kapufi.

Kapufi anasema lengo la ziara yake na wanahabari ilikuwa ni kuwapa nafasi waandishi kuifahamu Hifadhi ya Katavi, kujionea vivutio vilivyopo, hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kuitangaza kitaifa na kimataifa.

“Ni wajibu wetu kama viongozi kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye mwezi uliopita alitoka ofisini na kutembelea vivutio kadhaa vya utalii akilenga kuvifanya vijulikane zaidi ulimwenguni.

“Alichofanya Mama Samia ni kuvutia watalii wa ndani na nje na aliongozana na waandishi wa habari wa kimataifa, ndiyo maana na mimi nikawachukua waandishi wa habari wa Mkoa wa Katavi ili nao wajionee uzuri wa maliasili tulizonazo,” anasema.

Mwandishi wa makala hii ambaye pia ni Mwenyekiti wa Katavi Press Club alikuwa miongoni mwa ‘watalii’ hao wa ndani katika ziara iliyoratibiwa na mbunge.

Kundi la waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari 14 vilivyoko Katavi lilitembelea Hifadhi ya Katavi na kwa hakika halikuridhishwa na mapokezi waliyopewa na maofisa wa hifadhi.

Wakati mbunge akifahamu umuhimu wa kundi hilo kutembelea hifadhi, maofisa wenye dhamana ya utalii hawakuonyesha si tu ushirikiano, bali hata kujali na ‘kujiongeza’, kwa mujibu wa msemo maarufu wa mtaani.

Hatimaye ziara hiyo ilihitimishwa katika eneo maarufu la Mto Iku; eneo ambalo Rais Dk. John Magufuli na msafara wake walipumzika mwaka 2019 na kupata ‘asusa’ ya nyamapori, kisha akatoa maelekezo ya kufunguliwa kwa mabucha ya nyamapori maeneo mbalimbali nchini ili wananchi wapate kitoweo hicho.

Mto Iku ni nyumbani kwa idadi kubwa ya mamba na viboko; lakini pia tembo, simba, twiga na wanyama wengine hupatikana kwa wingi.

Kosa la maofisa wa Katavi kumpa mwongoza watalii mwanafunzi jukumu la kuwaongeza waandishi wa habari, lilionekana katika eneo hilo wakati wa kuhitimisha ziara.

Kijana huyo, Godlisten Isaya, akawaeleza waandishi wa habari akisema: “Katavi ndiyo hifadhi yenye viboko wengi zaidi, kwa kuwa ina viboko 2,770,000.”

Viboko karibu milioni tatu? Hii ni idadi kubwa mno na kila aliyemsikia kijana yule, alishituka. 

Ni wazi idadi ya viboko ipo na maofisa wa hifadhi wanaifahamu, lakini kwa nini walimruhusu mwongoza watalii mwanafunzi kuzungumzia takwimu nzito namna hii?

Katika mitandao ya kijamii, ofisa mmoja wa Hifadhi ya Katavi, badala ya kutoa ufafanuzi kuhusu idadi hiyo ya viboko, anamsukumia mbunge lawama!

Anapotosha nia ya mbunge ya kuwatumia waandishi wa habari kuitangaza hifadhi, na kusema lengo lilikuwa ni kuitangaza ‘kampuni yake ya utalii!’

Kauli hii imewakera sana waandishi wa Katavi na ni vema wahusika wakaomba radhi badala ya kuingiza hoja dhaifu katika masuala mazito kama haya.

Katika kuhakikisha ziara hiyo inafanikiwa na kufikia malengo yake, Mbunge wa Mpanda Mjini, Kapufi, alitoa taarifa kwa uongozi wa Hifadhi ya Katavi siku tatu kabla.

Kwa wahusika kusita kutoa ushirikiano pamoja na kupewa taarifa mapema kumewafanya watu kudhani kuwa huenda kuna hujuma zinafanywa kwa makusudi na maofisa kutoka upande fulani wa Tanzania, kuhujumu utalii wa upande mwingine.

Kapufi akagharamia kila kitu katika ile kuthibitisha ukweli wa msemo wa wahenga kuwa ‘kila msiba una mwenyewe’; na hivyo msiba wa Katavi unamgusa yeye moja kwa moja kama mzawa wa mkoani hapa.

Anafahamu kuwa Katavi ikitangazwa na kukubalika, itasukuma mbele maendeleo ya wananchi wake na kuchangia katika pato la taifa.

Pamoja na hayo, hakupewa ushirikiano. Kwa nini? Majibu yanabaki kwa maofisa hasa wanaosimamia utalii ndani ya Hifadhi ya Katavi ambao kwa hakika wamepambanua misimamo yao kwenye mitandao ya kijamii.

Walipaswa kufahamu kwamba hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa mbunge huyu kuwapeleka wadau hifadhini, kwani amewahi kuwapeleka wenyeviti wote wa mitaa wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda.

Yaani, msiba wa Katavi ameubeba yeye peke yake na waliotarajiwa kumfuta machozi, wanamtelekeza hadharani na mitandaoni kana kwamba hawaoni kuwa nao ni jukumu lao.

TANAPA wa Katavi mnafeli wapi? Hamna uchungu na hifadhi? Hamuoni aibu kupokea mishahara na posho kutokana na utalii wa Serengeti na Kinapa?

Lini mtasimama kwa miguu yenu na kulipana mishahara kutokana na mapato mnayotengeneza wenyewe?

Mmoja wa waandishi waliokuwa kwenye ziara hiyo, Ezron Mahanga, anasema waandishi hawakutaka hata kuzungumza na Mhifadhi wa Utalii wa Katavi anayemtaja kwa jina moja, Shirima.

“Shirima hakuonyesha ushirikiano kwetu wala kwa Kapufi na sisi kwa kutambua mchango wa mbunge huyo, tukaona hakuna haja ya kuzungumza naye.

“Tukamuacha na takwimu zake za viboko milioni mbili. Angeweza kutumia nafasi ya kuwapo kwetu mbugani kuitangaza hifadhi, na si kumuaibisha mbunge kwa kumtoza kiingilio cha waandishi ghafla tu,” anasema.

Anasema kama Shirima angetumia busara, angetumia nafasi ya waandishi kupelekwa huko na mbunge kutangaza hifadhi lakini sasa akitaka kufanya hivyo atalazimika kuwaita waandishi kwa gharama za hifadhi, na hata wengine atawaalika kutoka Dar es Salaam.

“Sasa hiyo ni gharama kubwa na ya kujitakia,” anasema.

Hata hivyo, mwongoza watalii aliyeambatana na waandishi, Godlisten Isaya, hakukosea katika kila takwimu.

“Wanyama wanaopatikana kwenye hifadhi hii ni wakubwa kuliko wanaopatikana kwenye hifadhi nyingine nchini,” anasema Isaya.

0769 163 353/0784 909 721

By Jamhuri