‘Hii ni awamu ya matendo makali’

DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi

Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan, ameendelea kufanya mabadiliko ya uongozi katika ngazi mbalimbali, lengo likiwa ni kuleta tija katika harakati za kuwahudumia Watanzania kuleta maendeleo na ustawi wa jamii.

Tangu alipokula kiapo cha kuongoza nchi Machi 19, mwaka huu, ameendelea kufanya teuzi mbalimbali huku akisisitiza na kuweka wazi suala la uwajibikaji na kwenda na kasi yake ya kuwahudumia wananchi kwa waledi mkubwa.

Kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Dk. John Magufuli, wakati wote akiwaapisha viongozi mbalimbali wa serikali, aliwaeleza bayana kuwa wasifurahie sana nafasi hizo kwa sababu hatasita kuwaondoa watakaoshindwa kutimiza wajibu wao.

Jumatano ya Machi 31, mwaka huu, Rais Samia alifanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, aliyeteuliwa na kuthibitishwa na Bunge Machi 30 kwa kupata kura asilimia 100.

Akizungumza kuhusu kupangua Baraza la Mawaziri, Samia anasema ameanza kuwapangua kutokana na ufinyu wa muda uliokuwapo tangu walipoapishwa Desemba 2020 na kusema ni muda mfupi kwake kujua yupi amefanya vizuri na yupi amefanya vibaya katika nafasi yake.

“Nimeona niwabadilishe kwa sababu tokea mlipoapa hadi sasa ni muda mfupi kusema nani kashindwa nani kafanya vizuri, lakini tunapokwenda tutaona nani tutakwenda naye, nani tunamuacha njiani, lakini kwa sasa tunakwenda hivyo,” anasema Rais Samia.

Akizungumza kwa sauti ya upole yenye ujumbe mzito, alitoa angalizo kwa watendaji hao wa serikali kwa kusema ushirikiano kati ya mawaziri na manaibu unaonekana bado ni tatizo katika baadhi ya wizara na kusisitiza kukomeshwa kwa tabia hiyo ambayo inarudisha nyuma jitihada za serikali katika jukumu la kuwahudumia wananchi.

“Mna mtindo huwa hamuwapangii kazi. Kuna kudharauliana na hata sasa hivi nina baadhi ya kesi manaibu waziri wanawadharau mawaziri wao. Waziri naye anamdharau Naibu Waziri. Dharau zikiendelea, basi tutajua cha kufanya huko mbele. Ninachotaka ni kazi, sitaki kusikia kingine,” anaonya.

Rais anaeleza sababu mbalimbali za kuwabadilisha baadhi ya mawaziri, akisema ameangalia ujuzi na uzoefu na kwamba amelenga kuwachukua mabingwa wa sekta na kuwasogeza kwenye sekta husika.

Ni wizara nane tu ndizo zilifanyiwa mabadiliko, nyingine zikaachwa vilevile. 

Zilizofanyiwa mabadiliko ni Wizara ya Fedha na Mipango ambako nafasi ya Dk. Mpango ilichukuliwa na Dk. Mwigulu Nchemba huku Wizara ya Mambo ya Nje akipewa Liberata Mulamula.

Katika hafla hiyo Rais aliwataka mawaziri na manaibu kufanya kazi kwa lengo moja; kuwatumikia  Watanzania, badala ya kutafuta umaarufu wa kisiasa.

“Sisi ni watumishi wa Watanzania wote. Nitakuwa na kipimo cha mabega. Nikiona mtu mabega yamezidi kupanda juu, ninajua huyo si mtumishi bali ‘ana-enjoy’ juu ya kiti chake. Ni jambo ambalo silitarajii, ninatarajia kusikia mko huko kwa Watanzania, kila mmoja kwa sekta yake achape kazi kwa maendeleo ya nchi,” anasema Rais.

Kuhusu wenye ndoto za urais 2025, amesema  waache mara moja badala yake wachape kazi kwa maendeleo ya taifa.

“Tuacheni tukafanye kazi, hili na lile tutajua mbele. Rekodi yako inakufuata katika maisha yako. Na mimi nitakuwa na jicho kubwa sana kuangalia rekodi zenu na safari ya mbele yenu. Lakini ninataka kuwaambia kila mwenye nia 2025 aache mara moja,” anasisitiza Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.

Septemba 12, mwaka huu, Samia amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, akiwaondoa mawaziri watatu na kuteua Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuziba nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha Elias Kwandikwa, Agosti 2, mwaka huu.

Mawaziri walioapishwa Ikulu ya Chamwino, Dodoma Jumatatu ya Septemba 13 ni January Makamba (Nishati) Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi na Uchukuzi), Dk. Ashatu Kijaji (Tehama) na Dk. Stergomena Tax (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).

Kuonyesha kwamba mabadiliko bado yanaendelea, Rais Samia wakati akitoa hotuba baada ya kuwaapisha, amewatakia kazi njema mawaziri wapya na kusisitiza kuwa anakwenda kuendelea na marekebisho zaidi.

Amesema katika miezi sita ya urais wake, amejaribu kuwa mkimya na mtulivu akizisoma wizara zote zinavyoendeshwa.

“Wakati  mimi ninawasoma wao, na wao walikuwa wananisoma mimi. Kama nilivyosema kati yao  walichukulia ukimya na utulivu wangu kama udhaifu na wakaanza kufanya yanayowapendeza, lakini wengine walichukulia ukimya na utulivu wangu kama ni njia ya wao kufanya kazi na kuonyesha kwamba wameweza,” anasema Samia.

Amesema katika kipindi hicho alipata muda wa kutosha kujifunza utendaji wa viongozi hao kwa sababu kabla ya hapo alikuwa Makamu wa Rais na hakuwa na fursa kubwa ya kujifunza utendaji wa ndani ya wizara.

Na kwamba kwenye uongozi kuna mbinu mbili; karoti na fimbo.

“Na mimi nimejichagulia njia yangu. Nataka niwaambie kwamba tunapoendelea huko serikali yetu itaendeshwa kwa matendo makali na si maneno makali. 

“Ninaposema matendo makali wala si kupigana mikwaju au mijeledi! Ni kwenda kwa wananchi na kutoa huduma. Inayotakiwa ni kila mmoja kufanya wajibu wake,” anasema.

Rais  Samia anayesimamia kauli ya serikali yake isemayo ‘Kazi Iendelee’, anasema mabadiliko na marekebisho anayofanya yanaendelea kutokana na jinsi alivyoona utendaji wa mawaziri na viongozi wengine kwenye wizara zao na maeneo mengine.

Katika hatua nyingine ya maboresho Septemba 25, Rais Samia amefanya mabadiliko katika Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa kuteua viongozi wapya, akiwamo Mkurugenzi Mkuu, Maharagande Chande, na Mwenyekiti wa Bodi, Omari Issa.

Waziri wa Nishati, January Makamba, pia amewateua wajumbe wapya wanane wa Bodi ya Tanesco na kuweka sura za baadhi ya wafanyabiashara maarufu nchini.

Mabadiliko hayo yanaelezwa kulenga kuleta ufanisi TANESCO baada ya kuwapo malalamiko mengi, likiwamo tatizo la kukatika kwa umeme.

Kwa upande wake Makamu wa Rais, Dk. Mpango, anasema: “Mumuone Rais kama kocha ambaye anajaza wachezaji wake wanaocheza na kila wakati anaitazama timu kama kweli inacheza na itakwenda kufunga magoli ili kupata ushindi.

“Ushindi wa Watanzania. Mkashirikiane na hao wote mnaowakuta ili matarajio ya Rais na matarajio makubwa ya Watanzania yaweze kutimia.” 

Kuhusu utendaji wa Rais, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, amesema Samia anaiongoza nchi vizuri na kwamba anaendelea kusimama imara na kuwaomba watendaji wa serikali na wananchi kuendelea kumuunga mkono.

Septemba 14, akiwa Halmashauri ya Chalinze, Kikwete anasema: “Jamani urais si kazi rahisi, ina mawimbi mengi, inahitaji mtu makini. Mpaka sasa Mama Samia ameanza na kipindi kifupi tumeona anaendesha nchi vizuri licha ya changamoto zilizopo.”

Mfuatiliaji wa masuala ya Siasa na Jamii, Hashimu Yahya wa Manispaa ya Morogoro, anasema Rais Samia amefanya mabadiliko ili kupata timu anayoamini itamletea mafanikio.

“Nafikiri Rais Samia anatumia uzoefu wake katika uongozi kuchuja baadhi ya watendaji kutokana na utendaji wao. Anachotaka ni timu ya kumletea ushindi katika kuwahudumia wananchi,” anafafanua Yahya.

0755985966