Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii kwa kuhoji hivi: “Je, unaelewa VAT ni nini na inalipwaje? Usikose sehemu ya 26 ya makala hii wiki ijayo.” Leo nashindwa kuanza makala hii bila kutoa pole kwa taifa letu kutokana na msiba mkubwa uliotokea mkoani Morogoro, baada ya watu zaidi ya 70 kufariki dunia na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa kutokana na lori lililokuwa linasafirisha mafuta kuanguka likawaka moto.

Nafahamu uchungu tulionao Watanzania kuhusu kupotelewa wapendwa wetu, lakini pia ninasikitika kuna utaratibu mpya ulioanza kujengeka hapa nchini kwamba inapotokea ajali, watu wanafika kwenye eneo la tukio kupora mali na si kusaidia kuokoa maisha na kuhifadhi mali za waliopata ajali.

Sitanii, nafahamu katika mazingira tuliyomo wengi wanaona si vema kuwalaumu watu waliopoteza maisha au wenye majeraha, ila wakati nikitoa pole kwa wahusika, naomba Watanzania tukubali kumeza dawa chungu kuponya ugonjwa.

Bunge litapaswa kutunga sheria kali ya kushitaki yeyote anayevamia aneo la ajali kuiba mali badala ya kuokoa maisha. Tukiwafikisha mahakamani wenye kufanya uhalifu wa aina hii, tutarejesha uadilifu kwa mkono wa sheria siku za usoni. Mungu awarehemu waliofariki dunia na awape uponyaji wa haraka majeruhi wote.

Baada ya utangulizi huo, naomba katika safu hii nianze na swali la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni nini. Kodi hii ni kodi ya matumizi. Inatozwa katika bidhaa na huduma, mali isiyohamishika ya kibiashara, pale thamani inapoongezwa katika hatua mbalimbali na katika hatua ya mwisho. Kodi hii inatozwa kwa bidhaa zote zilizomo kwenye orodha, iwe ni za ndani au zinazoingizwa nchini. Hata hivyo, kodi hii inatozwa na wale tu waliosajiliwa kuitoza.

Kodi hii inatozwa kwenye shughuli zote za kiuchumi, ikiwamo biashara na mali zisizohamishika zinapofanya biashara au kuuzwa. Kwa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi, kodi ya VAT ni sifuri.

Sitanii, wapo watu wanaojiuliza usajili wa kulipa VAT unakuwaje? Kila mfanyabiashara ambaye ndani ya miezi 12, kwa maana ya mwaka mmoja mzunguko wa mauzo yake ukifikia Sh milioni 100 au Sh milioni 50 katika muda wa miezi 6, basi hiyo biashara inapaswa kusajiliwa kwa ajili ya kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

 Takwa hili la kisheria linawahusu wafanyabiashara wote, isipokuwa watoa huduma binafsi za kitaaluma, vyombo vya serikali na taasisi zake zinazofanya shuhguli za kiuchumi, na wafanyabiashara watarajiwa baada ya kutimiza masharti ya msingi kama mikataba, zabuni, ramani za majengo, mpango wa biashara na mikopo ya benki.

Mtu anayefikisha kiwango cha kulipa VAT anapaswa kujisajili mara moja kwa Kamishna Mkuu wa TRA ndani ya siku 30 tangu alipofikisha kiasi hicho, lakini wafanyabiashara wenye nia ya kupata kazi wanajisajili muda wowote wanapokamilisha masharti ya kimkataba.

Baadhi ya watu wanaweza wakaamua kwamba hawataki kujisajili, lakini kumbe huo si ujanja. Sheria inampa mamlaka       Kamishna Mkuu wa TRA kumsajili mtu yeyote na kumjulisha ndani ya siku 14 kuwa amesajiliwa kulipa VAT bila mtu huyo kuomba, ikiwa anaona kuna mapato ya serikali yanakaribia kupotea. Kwa utaratibu wa kawaida, mwombaji anapaswa kujaza fomu maalumu ya kujisajili na VAT. Kawaida ni mara moja kwa mwaka mhusika anapofikia kiwango kinachotakiwa kisheria.

Baada ya kusajiliwa, mlipakodi atakabidhiwa cheti cha kusajiliwa kuwa analipa VAT. Cheti hiki kinapaswa kuonyesha jina, eneo la biashara, tarehe ya kusajiliwa, Namba ya Mlipakodi (TIN) na namba ya usajili wa VAT. Cheti hiki anapaswa kuhakikisha kinaonekana sehemu iliyo wazi katika eneo la biashara.

Kila mwezi mfanyabiashara aliyesajiliwa kulipa VAT anapaswa kuwasilisha marejesho ifikapo tarehe 20 ya mwezi mpya kwa njia ya mtandao au kwa kujaza fomu maalumu. Sheria inasema ikiwa tarehe 20, ambayo ni siku ya kupeleka marejesho inaangukia Jumamosi, Jumapili au sikukuu, basi mlipakodi anapaswa kufanya marejesho siku ya kwanza ya kazi inayofuata baada ya siku hizo.

Sitanii, wapo wanaojiuliza, VAT inatozwaje? Utaratibu uko wazi. Katika kila bidhaa inayouzwa iliyopo kwenye orodha za bidhaa za kutozwa VAT, kila mtu anayefanya biashara hiyo aliyesajiliwa kulipa VAT anatoa kodi hiyo, kisha naye anaitoza kwa anayemuuzia bidhaa bila kujali idadi ya waliopo kwenye mnyororo wa biashara hiyo.

Baada ya kulipa kodi hiyo wakati wa kununua bidhaa husika, mfanyabiashara akiuza anapaswa kukata kodi yake ya VAT aliyolipa mwanzo na iwapo bei yake iko juu kidogo na hivyo anakusanya kodi nyingi zaidi ya aliyoitoa wakati ananunua bidhaa aliyoiuza, basi anapaswa kulipa kwa TRA kiwango cha kodi kinachotofautiana na kiasi alicholipa yeye wakati ananunua mzigo.

Mfumo huu wa kodi hauumizi biashara kwa njia yoyote, badala yake mlipakodi anakuwa ni mtumiaji wa mwisho. Somo hili ni pana na nitatafuta fursa ya kulifafanua zaidi, kwani mfumo huu ukifanya kazi vema, basi hakutakuwapo tena shida ya kukimbizana na wananchi kwenye kodi ya mapato. Tutahamia kwenye kodi hii ya matumizi. Usikose sehemu ya 27 ya makala hii kusoma mwendelezo Jumanne ijayo.

737 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!