Home Sitanii Jinsi ya kuanzisha biashara Tanzania (25)

Jinsi ya kuanzisha biashara Tanzania (25)

by Jamhuri

Wiki iliyopita nilihitimisha mada yangu kwa kuhoji: “Mpendwa msomaji, je, unafahamu kodi inayoitwa Kodi ya Ongezeko la Mtaji (Capital Gains Tax) na inatozwa kwenye bidhaa zipi? Ni bidhaa mbili ambazo kwa njia moja au nyingine watu wengi hata wasiokuwa wafanyabiashara kwa nyakati tofauti wameshiriki kufanya biashara hiyo, lakini aghalabu ni wachache wanaoilipa kodi hii, ila ikumbukwe kuwa kutolipa kodi ni jinai.”

Kodi ya Ongezeko la Mtaji ni nini?

Baada ya kuweka kidokezo katika aya ya mwisho ya makala iliyopita sehemu ya 24, nimeulizwa na wasomaji kadhaa hii kodi ni kodi ipi na inalipwaje. Kodi hii ni kodi inayotozwa katika faida anayopata muuzaji wa jengo au ardhi, baada ya kukata kiasi cha fedha alizonunulia awali na gharama aliyoingia kuendeleza na kuuza jengo au kiwanja husika.

Sitanii, kodi hii inalipwa pale mmiliki wa ardhi au jengo anapouza, kubadilishana na mmiliki mpya, kuhamisha umiliki, kugawanywa, kuharibiwa, kusalimisha, kukomboa na hata taasisi inayomiliki jengo au ardhi inapofilisika, hivyo muda mfupi kabla ya kufilisika inapaswa kulipa kodi hii. Sheria ya Kodi ya Mapato inataka mara tu mtu anapouza jengo au ardhi iliyopo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulipa kodi hii kwa mkupuo.

Kodi hii inalipwa kabla ya umiliki kuhamishwa kutoka kwa mmiliki wa awali kwenda kwa mmiliki mpya. Msajili wa Hati hapaswi kusajili hati mpya ya ardhi au miliki ya jengo hadi mwombaji awasilishe hati ya kulipa Kodi ya Ongezeko la Mtaji yenye kuonyesha kuwa kodi hii imelipwa kwa mkupuo. Muuzaji anapaswa kujaza fomu Na. ITX 204.01.E kuonyesha kuwa amehamisha umiliki wake na yeye si mmiliki tena wa ardhi au jengo husika.

Wapo watu walioniuliza kuhusu viwango vya kodi hii. Anayeuza ardhi au jengo, kama ni mzawa anapaswa kulipa kodi asilimia 10 ya faida iliyopatikana juu ya mtaji aliowekeza katika ardhi au jengo husika. Kwa mtu ambaye si Mtanzania mkazi, atatozwa asilimia 20 katika faida inayotokana na uuzaji huo wa ardhi au jengo.

Hata hivyo, kuna habari njema. Sheria ya Kodi ya Mapato inampa fursa mtu anayelipa Kodi ya Ongezeko la Mtaji kuitumia kodi aliyolipa kugharamia deni la kodi katika mwaka wa fedha husika.

Sitanii, Kodi ya Ongezeko la Mtaji hailipwi kwa kila mauzo ya ardhi au nyumba yanayofanyika. Kuna msamaha katika majengo ambayo ni nyumba ya kuishi ambayo mtu ameishi ndani ya nyumba hiyo kwa miaka mitatu mfululizo na ameiuza kwa bei isiyozidi Sh milioni 15 au ardhi anayoitumia kwa kilimo kwa miaka miwili katika miaka mitatu kabla ya siku ya kuiuza, basi hiyo nayo ikiwa thamani ya ardhi iliyouzwa haizidi Sh milioni 10, basi hatozwi Kodi ya Ongezeko la Mtaji.

Awali nimetaja gharama za uwekezaji katika jengo au ardhi husika. Gharama hizi ni pamoja na ushuru wa stempu, gharama za usajili, tozo za wanasheria na gharama za udalali. Kwa kampuni iwapo inanunua ardhi au jengo, Kodi ya Ongezeko la Mtaji inakuwa ni asilimia 30 ya faida inayopatikana juu ya gharama za uwekezaji.

Kwa upande mwingine Kodi ya Ongezeko la Mtaji inatozwa katika uuzaji wa dhamana, hisa na haki za umiliki katika uwekezaji. Kwa kampuni hulipishwa asilimia 30 ya kodi kwa mapato yatokanayo na kuuza dhamana, lakini kwa mlipa kodi mkazi, hutozwa kodi kulingana na viwango vilivyoainishwa kwa mlipa kodi mmoja mmoja.

Hata hivyo, sheria inatambua pia kuwa kuna uwezekano wakati mwingine mtu anaweza kuuza jengo au ardhi kutokana na hasara aliyoipata. Ikitokea hivyo, akiuza kabla ya kulipa kodi anapaswa kukata hasara aliyoipata kutokana na uwekezaji, hasara aliyoipata katika mwaka anaouza jengo au ardhi na mwaka uliotangulia. Pia anatoa gharama ya kununua jengo au ardhi (hata kama alijenga mwenyewe, basi gharama za ujenzi). Kwa upande wa hisa, ikiwa kampuni imesajiliwa kwenye soko la hisa na Mtanzania mkazi anamiliki zaidi ya asilimia 25, basi kodi hii halipwi.

Sitanii, kuna vigezo vya hasara zinazotambulika unapouza jengo au ardhi. Hasara hizo ni lazima ziwe zimetokana na mali inayouzwa na si vinginevyo. Lakini pia iwapo mmiliki atapata hasara wakati wa kuuza jengo, hasara aliyoipata anaweza kuifidia iwapo atauza jengo jingine akapata faida. Wawekezaji wa kigeni pia wanaweza kutumia hasara ya mauzo katika ardhi au jengo kufidia hasara waliyopata katika uwekezaji wa kigeni.

Mpendwa msomaji, katika kuanzisha biashara Tanzania kodi nyingine inayosumbua wafanyabiashara wengi ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Nimepata kugusia kuwa zipo nchi zilizohama kutoka kwenye mfumo wa Kodi ya Mapato kwenda kwenye Kodi ya Matumizi, ambayo wengi wanaiita VAT. Je, unaelewa VAT ni nini na inalipwaje? Usikose sehemu ya 26 ya makala hii wiki ijayo.

You may also like