Wananchi wa Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wameandamana wakitaka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lipelekwe nchini humo liwakung’ute waasi wanaoua mamia kwa maelfu ya watu.

Bado wananchi wengi wa DRC wanatambua na kuenzi kazi kubwa iliyofanywa na majeshi ya Umoja wa mataifa ya kulinda amani yaliyoongozwa na JWTZ baada ya kuwafurusha waasi wa March 23 (M23).

Maandamano hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki yalikusudiwa kwenda hadi katika Makao Makuu ya Jeshi la Umoja wa Matiafa linalolinda amani Kaskazini Mashariki mwa DRC (MONUSCO).

Waandamanaji wengi walikuwa wanawake, na licha ya kutawanywa kwa mabomu walihakikisha kilio chao wanakiwasilisha kwa Kamanda wa MONUSCO aliyeko katika mji wa Beni.

Jeshi hilo la Umoja wa mataifa linaundwa na askari kutoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini.

Wanasema MONUSCO kwa kuzingatia sheria za UN, imeshindwa kukabiliana na waasi wa kundi la ADF kwa kuwa hawaruhusiwi kutumia silaha kukabiliana na waasi hao.

Ni kwa sababu hiyo, wananchi hao wanapendekeza DRC iombe Tanzania ipeleke askari wake wa JWTZ kwa imani kuwa ni shupavu na watakabiliana na waasi bila kuzingatia sheria za UN kwa vikosi vya MONUSCO.

“Wanajeshi wa Tanzania walifanya kazi kubwa na tukaanza kukaa kwa amani kabisa. Lakini walibanwa na sheria za MONUSCO. Wana silaha zote kubwa kubwa, wana vifaru na zana zote za kivita, lakini wanabanwa na sheria. Tunaona huu ni mpango wa Wazungu wa kuona vita haimaliziki DRC.

“Kama JWTZ wataletwa hapa na kupambana na waasi hawa bila vikwazo vya UN, tunaamini nchi yetu itakuwa na amani,” amesema mmoja wa waandamanaji hao.

Taarifa kutoka katika mji wa Beni zinasema waasi wa ADF wanaodaiwa kutoka Uganda, wameweka ngome katika misitu iliyoko Beni, ambayo inapakana na misitu mikubwa ya Mlima Rwenzori (Uganda) na Mbunga ya Virunga (DRC).

Wiki iliyopita mauaji yametokea katika mji wa Mbau, kaskazini mwa mji wa Beni; na kabla ya hapo yalitokea maeneo mengi jirani.

Waasi hao wanadaiwa kubadili staili ya mauaji ya raia, na sasa wanawachinja na kutenganishwa vichwa na viwiliwili. Awali, walikuwa wakiua watu kwa kuwapiga shoka vichwani na pia kuwapasua matumbo.

Jenerali Mbangu wa Jeshi la DRC anasema kuna kundi jipya la waasi la TMT ambalo mwelekeo wake ni wa kigaidi. Kundi hilo linahusishwa na Waislamu wenye siasa kali; na kwamba linaundwa na vijana kutoka mataifa yanayopakana na DRC.

Taarifa hiyo inapingwa na Marekani ambao katika taarifa ya ujumbe wake uliopelekwa DRC hivi karibuni imesema kundi hilo halina itikadi za kigaidi.

Lakini Serikali ya DRC inasema kundi hilo ni la kigaidi kwa sababu wapiganaji wake huteka watoto na vijana na kuwapeleka msituni ambako huko hufundishwa itikadi kali.

Wananchi wanasema Umoja wa Mataifa uko DRC kwa miaka zaidi ya 20, wana vifaa vyote vya kivita, lakini wanasema hawaelewi kwanini Jeshi la Kulinda Amani la Umoja huo limeshindwa kuwadhibiti waasi.

Katika tukio la mauaji katika Mji wa Mbau, wananchi wanasema waliwaona hao waasi, wakapeleka taarifa serikalini na kwa MONUSCO, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa. Usiku waasi hao waliwachinja wananchi.

Wananchi na wabunge katika eneo la Beni wanaona kuna njama zinazofanywa na Serikali ya DRC na hata Umoja wa Mataifa zinazosababisha wananchi waendelee kuuawa.

Redio ya Sauti ya Amerika (VOA) imetangaza kuwa wanaokufa  wengi ni watoto na wanawake; na kuwa mauaji ya sasa watu wanakatwa vichwa.

“Mauaji mengine yalikuwa ya kupiga shoka kichwani au kupasuliwa tumbo. Lakini sasa wanakata shingo na kutenganishwa na kiwiliwili,” imesema VOA.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, amezungumza na JAMHURI kuhusu ombi la wananchi wa DRC na kusema maombi yoyote ya aina hiyo yanapaswa kupitia Umoja wa Afrika (AU) au UN.

“Hiyo taarifa binafsi sina, sijaipata, lakini ninachojua ni kuwa huwezi kupeleka jeshi katika nchi nyingine bila kupitia kwenye utaratibu wa Umoja wa Mataifa au Umoja wa Afrika. Hiyo mandate unaipata kupitia taasisi hizo. Ndiyo maana jeshi letu liko pale likiwa ni sehemu ya Jeshi la Umoja wa Mataifa. Sehemu yetu sisi tuko na Malawi na Afrika Kusini – Force Intervention Brigade.

“Kama kilio chao kuwa huko yalikotokea matukio hii FIB haiko huko, na kama hivyo ndivyo, basi maana yake ni kweli – MONUSCO wanaweza kuamua wapelekwe huko, lakini si kupitia nchi kwa nchi.

“Ninachoona ni kweli kwamba kuna FIB iko pale na moja ya madhumuni yake ni kuhakikisha inalinda raia dhidi ya hivyo vikosi – negative forces. Kwa maana hiyo ni kwamba inapotokea matukio, basi ni wajibu wa Umoja wa Mataifa kupitia MONUSCO kupanga vikosi vilivyoko pale kwa sababu kuna nchi nyingi sana ziko pale. Wapange ni wapi hivi vikosi vikachukue nafasi, lakini sidhani kama kunahitajika kupeleka vikosi vingine kwa sababu tayari kuna kikosi kikubwa.

“Hawa MONUSCO kuna mandate mbili – moja inaitwa Chapter 6, ambayo ni ‘peace keeping’. Wale hawaruhusiwi kupambana na hao magaidi [waasi]. Halafu kuna Chapter 7, ambako ndiko kuna FIB ambayo ndiyo sisi tumo – hiyo ina mandate hiyo ya kupambana na kuwatetea wananchi. Kinachotakiwa pale nadhani kwa mujibu wa hao wananchi wa huko ni kwamba wale Chapter 6 inaonekana kama kazi yao haipo, kwa sababu watu wanashambuliwa, na wao kama hawawezi kujibu mashambulizi yale maana yake hakuna peace ya kulinda, inatakiwa ku – enforce hiyo peace kwanza, kwa maana hiyo ni kuwa hiyo Chapter 6 ingekuwa kwenye utaratibu kama wa Chapter 7 ingesaidia, hivyo nguvu zingekuwa nyingi na kwa sehemu nyingi,” amesema Dk. Mwinyi.

Kichapo cha JWTZ kwa M23

JWTZ imejijengea heshima kubwa nchini DRC kutokana na kazi iliyotukuka ya kuwakung’uta waasi wa kundi la March 23 (M23)

Baada ya kupigwa na kukimbia uwanja wa mapambano walisema hawana hamu na wapiganaji na makamanda wa JWTZ.

Wakizungumza na JAMHURI kutoka nchini Uganda na Rwanda, Novemba, 2013 baadhi ya waasi hao walieleza kushangazwa na uwezo mkubwa wa JWTZ, na wanasema ‘wanaume’ hao walipoingia Goma tu, ghafla maisha yao yaligeuka na kuwa magumu.

Mmoja wa waasi hao anayezungumza Kiswahili kwa ufasaha, alisema kuwa yeye pamoja na kuhama makundi kadhaa ya waasi kabla ya kuundwa kwa M23, anamshukuru Mungu kuona bado yuko hai kwani kipigo walichopata kutoka kwa askari wa JWTZ kilimwogopesha.

“Wale askari Wazungu tangu walipofika mwaka 2000 ilikuwa tuko kwenye ‘sherehe’ tu. Tulikuwa tukiishiwa fedha tunaanza kupigana, nao wanakimbia. Wale Wazungu ilikuwa ikinyesha mvua, hawathubutu kuingia msituni.

“Kila ilipokuwa inafika jioni, wanakwenda kwenye hoteli kunywa pombe na kutafuta vimwana, nasi tulikuwa tunakutana nao wakati huo tumeacha silaha zetu porini kwenda mjini kustarehe.

“Wazungu walikuwa wanakuja wanakula bagger (mikate iliyochanganywa na nyama), tena wakati mwingine ikitokea jua likawa kali wanatafuta vivuli, lakini tangu Mei askari wa JWTZ wamechafua hali ya hewa.

“JWTZ hawajali mvua, utelezi, msitu, giza au jua kali… tulifika mahala tukajiuliza hawa wanakula saa ngapi? Mafunzo yao walipata wapi? Maana kilichotukuta hatukutarajia. Walikuwa wanatushambulia kwa kasi ya ajabu, usiku, mchana, wakati wa jua na mvua na hawaogopi kuingia msituni.

“Tulifika mahala tukashindwa hata kupika chakula, maana ilikuwa ukiinjika sufuria tu unashtukia JWTZ hawa hapa, sasa kwa sababu tulikwishaingiwa hofu, ikawa ukiwaambia wenzako mpambane na JWTZ wanakimbia, wanasema ‘wanaua hao ni hatari, ni balaa si watu hawa.’

“Ilifika mahala tukadhani hawa JWTZ hawali, bali wanaishi kwa kuvuta hewa tu! Hatukuona wanakaa chini ya mti kupata kivuli, tulikuwa na bainokola nzuri tu, lakini zilikuwa haziwaoni, tunashtukia wameishafika kwenye kambi zetu, mpaka leo hatupati jibu,” alisema mmoja wa waasi aliyekimbilia Rwanda.

Muasi mwingine wa M23 aliyekimbilia Uganda, alisema hata kabla ya jamii ya kimataifa kuzishinikiza Rwanda na Uganda kuacha kuwaunga mkono, wao wapiganaji walikwishawaeleza makamanda kuwa kipigo walichopata Agosti, wasingeweza kukivumilia kwa mwezi mmoja zaidi.

“Pale ndo wakuu wetu wakasema tutumie mbinu ya kusema sasa tunataka mazungumzo walau vita ipoe kidogo. Kweli tulipotangaza kuwa tuko tayari kwa mazungumzo, wanaume hawa wakasitisha kutuchapa. Tukawa tunajipanga, sasa kumbe tulifanya kosa. Tulidhani wakati tunajipanga wao wako likizo.

“Kumbe nao walikuwa wanajipanga vizuri zaidi. Makamanda wetu waliposema tukashambulie sasa mwishoni mwa Oktoba, hali ikawa ngumu kinyume cha matarajio yetu.

“Mara tukasikia [Sultani] Makenga amekimbilia Uganda, tukaona ametuacha peke yetu JWTZ watuue. Tulimwambia ukae kwenye uwanja wa mapambano ikibidi ufie hapa kama alivyofanya Muammar Gaddafi wa Libya, yeye kupitia wapambe wake akasema tuendelee tu, yeye anakwenda kutafuta mbinu mpya.

“Ilipofika hapo tukaona hapana. Huyu anataka tufe peke yetu na watoto wetu wataabike. JWTZ si wa kuchezea, ukizubaa wanaweza kuua kikosi chote kwa muda mfupi. Tukaona tukimbilie Uganda alikokwenda Makenga,” alisema na kuongeza:

“Kilichotushangaza zaidi ni pale JWTZ walipokuwa wanafika kwenye maeneo yetu, wananchi tuliokuwa tunaishi nao wanatugeuka, wanawashangilia, nao wanawapa bisukuti, maji ya kunywa, wanapiga nao picha, wanabeba watoto wao wakishangiliwa, lakini sisi ilikuwa tukiwapa hata maji ya kunywa, wananchi wanayakataa wakidai yamewekewa sumu wakati si kweli.”

 Mamia ya wapiganaji wa kundi hilo wamesalimu amri na kuamua kutimkia katika nchi za Rwanda na Uganda.

 Majeshi ya Umoja wa Mataifa ya Kulinda Amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yaliongozwa na Brigedia Jenerali [amestaafu akiwa Luteni Jenerali] James Mwakibolwa wa JWTZ. Pamoja na Tanzania, nchi nyingine zilizochangia kwenye brigedi hiyo ni Afrika Kusini na Malawi.

 Mwanzoni mwa Novemba, 2012 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa ruhusa maalumu kwa majeshi ya UN yaliyoko DRC kutumia nguvu za kijeshi kuwafurusha M23 na makundi mengine ya waasi, yakiwamo ya Mai Mai.

Hatua hiyo ililifanya Jeshi la DRC lipate nguvu za ziada kutoka brigedi hiyo, hatua ambayo iliwalazimu waasi kubwaga manyanga, kujisalimisha na wengine kukimbilia mataifa jirani.

Baadhi ya waasi waliozungumza wakiwa mpakani mwa DRC na Uganda, walisema ueledi uliotumiwa na majeshi ya Umoja wa Mataifa chini ya uongozi wa JWTZ umewafanya wasiwe na hamu ya kuendelea na mapambano.

 JWTZ kwa kushirikiana na vikosi vya Umoja wa Mataifa walikamilisha kazi waliyotumwa ya kupambana na kuwanyang’anya silaha waasi wa M23 katika DRC.

Makundi mengine nayo yasalimu amri

Makundi ya uasi katika eneo la Mashariki mwa DRC, nayo yalikubali kuweka silaha chini na kurejeshwa katika maisha ya kiraia kwa baadhi; na wengine kujiunga katika Jeshi la Serikali (FARDC).

Novemba 2013 viongozi zaidi ya 10 wa makundi ya waasi walikutana kwa mazungumzo na Gavana wa Mkoa wa Kivu ya Kaskazini [wa wakati huo], Julien Paluku, kwa upande mmoja na kwa upande mwingine na Waziri wa Kitaifa wa Mambo ya Ndani [wa wakati huo], Richard Muyej Mangez, aliyezuru katika eneo hilo kuzungumzia kuhusu hatua hiyo.

Mmoja wa viongozi wa makundi hayo ya waasi – Izabayo Kabasha Ephrem, kutoka kundi la MPA Nyatura, alisema waliingia msituni kukabiliana na waasi wa kundi la M23, lakini kwa sasa kundi hilo si tishio tena, kwa hiyo hakuna sababu za kuendeleza mapigano.

2962 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!