Mwishoni mwa wiki nimeshuhudia jambo kubwa. Jambo lenyewe ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kujiengua kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Amejiunga UKAWA kupitia NCCR-Mageuzi. Sumaye wakati anahama amerejea aliyosema Profesa Mark Mwandosya.

Sumaye amesema anahama CCM si kwa sababu nyingine, bali kutokana na kukua kwa udikiteta ndani ya CCM. Anasema kama alivyosema Prof. Mwandosya ni kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alifika na kikaratasi chenye majina ya aliowataka waingie kwenye tano bora. Lakini nimemsikia pia mtoto wa Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro, akilinganisha urais na chandimu.

Sumeya emeondoka baada ya mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa kuondoka ndani ya CCM akisema hakubaliani na utaratibu uliotumika kumpata mgombea wa CCM. Wawili hawa, hawakupata kumtusi mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli. Hawa wamekuwa wakisema wanapinga udikiteta uliofanywa na Mwenyekiti wa CCM, Kikwete.

Sitanii, ukiacha kuondoka kwa hao nimeendelea kumsikiliza Katibu wa Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye anayewaita wanaoondoka CCM kuwa ni oil chafu. Kauli hii ameirudia kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam siku ya Jumapili. Nimemsikiliza Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein. Amezungumzia umuhimu wa amani.

Vita kubwa ipo kwenye mitandao ya kijamii. Hata kwenye mkutano wa CCM wa uzinduzi wa kampeni, lugha za ubaguzi nimezisikia kwa mbali. Nimemsikia Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Amon Mpanju akiwataja baadhi ya wagombea kuwa ni wakabila na wana ukanda.

Lugha za ukabila na ukanda, zinazungumzwa kwa kasi ya kutisha kwenye mitandao ya kijamii. Si ajabu kwa Mpanju na wengine kuzigusia. Huenda kampeni za mwaka huu zitatawaliwa na lugha za ukabila, udini, umajimbo na wakati mwingine kuomba kura za huruma kutokana na wajihi, historia na chimbuko, vitu ambavyo ni hatari kwa ustawi wa taifa letu.

Sikutaraji, na sitaraji iwapo kampeni zilizoanza wiki iliyopita zitaendelea kwa mkondo wa kuwashambulia Lowassa, Sumaye na wengine. Nimempenda Dk. Shein alivyomnadi Magufuli. Alitaja sifa za Magufuli bila kuwashambulia akina Lowassa. Jaji Joseph Sinde Warioba naye hakutumbukia kwenye mtego wa kushambulia wawili hao.

Sina uhakika kama Rais mstaafu Benjamin Mkapa, amezeeka au ni hofu ya kushindwa iliyomfikisha hapo alikofika. Sikutaraji, hata kama anayo hoja ya msingi, kwa heshima aliyonayo alipaswa kuhashimu kinywa chake. Maneno aliyotamka kwa kuwaita Watanzania wake wapumbavu, malofa, naona na naamini ni uchochezi. Busara sawa na liyoitumia Mzee Ali Hassan Mwinyi ingeendeleza heshima yake.

Inawezekana, kwamba Mkapa anayo hofu ya wazi kuwa CCM inaweza kushindwa kutokana na wimbi lililopo, lakini hata kama ndivyo, hatua yake ya kurudia neno upumbavu mara mbili, sina hakika kama amelitendea haki taifa. Najiuliza, hivi ikitokea wapinzani nao wakaanza kumwaga matusi ya aina hii majukwaani taifa litaelekea wapi?

Katika hili naamini Mkapa ameteleza. Mkapa anapaswa kuwaomba radhi Watanzania. Tukiruhusu nchi hii wakati wa kampeni viongozi wakafungua midomo watakavyo bila kukemewa au kurejeshwa kwenye mstari, wananchi watawaiga. Kuitwa mpumbavu mbele ya mama mkwe, usipopigana watakuwa na shaka iwapo binti yao yuko katika mikono salama. Nilidhani Mkapa amevuka mstari huu!

Nimemshuhudia pia Rais Kikwete jukwaani akilindwa na walinzi watatu. Anaye bodyguard ambaye ni askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), nyuma ya askari huyo anasimama mlinzi mwanamke na nyuma ya mlinzi mwanamke anasimama mlinzi wa kiume pia. Kiwango hiki cha ulinzi kimewatisha wengi na kujiuliza kulikoni?

Rais Kikwete kwa hali ya ajabu kabisa, akarejea kauli yake. Kwamba Chadema wanachukua picha za zamani za Dk. Slaa, wanaunganisha na kuzichapisha kwenye magazeti. Sina uhakika kama Kikwete alipata kufanya kazi gazetini au katika maisha yake amepata kufanya mchezo huu wa kuunganisha picha. Nasema hilo la pili linawezekana, pengine anasisitiza kwa kujua walivyokuwa wakifanya wakati wa kampeni zake!

Dhana ya Kikwete kudhani kuwa mikutano ya wapinzani picha zinaunganishwa, inaweza kuleta kiama mbele ya safari. Yapo mambo ya msingi aliyozungumza Kikwete, kuwa hataki Rais maskini, lakini hataki Rais ambaye haifahamiki mali yake aliipataje. Alimsifia Magufuli kuwa ni mwaminifu, ni mwadilifu,

Sitanii, mengi kati ya yaliyotokea Jangwani ndiyo mambo niliyosema tangu mwanzo. Nilisema uchaguzi wa mwaka huu utakuwa tofauti na uchaguzi wa miaka yote iliyotangulia. Niliona na nilijua kuwa itakuwpao mihemko. Hofu ya kushinda na kushindwa itakuwa kubwa katika uchaguzi wa mwaka huu. Si CCM wala upinzani wenye uhakika wa kushinda mapema.

Kauli za kejeli  badala ya sera juu ya elimu, afya, maji, reli, umeme, miundombinu kama barabara, maendeleo ya sayansi na teknolojia, ajira kwa vijana, viwanda vidogo, vikubwa na vya kati, asilimia 90 ya muda wa mkutano imetumika kuwasema waliohama CCM. Naamini hili halitaendelea na wala wapinzani hawatajibu mapigo kwa kuzungumza matusi dhidi ya viongozi wa CCM.

Nimefurahi, Samia Suluhu Hassan alipopewa fursa akazungumza walau kuwa atajenga mabweni, atahakikisha kila kijiji kinapata Sh milioni 50, akasema atasimamia na kuhakikisha kina mama wanapata maji safi na salama. Akazungumza kuwa atausimamia Muungano na kuudumisha kwa njia ya mazungumzo, walau huyu anatia moyo.

Dk. Magufuli alipopanda jukwaani, alianza kwa kuonyesha ukomavu mkubwa. Alizungumza na Watanzania kwa kutambua kuwa hata hapo Jangwani waliokuwapo si wote ni wafuasi wa CCM, hivyo akawasabahi kama Watanzania. Hotuba ya Magufuli ilijielekeza katika kuzungumza na Watanzania badala ya vijembe vya kichama.

Magufuli alitambua kazi iliyofanywa na marais waliomtangulia na akasema kuwa anatambua kiu ya mabadiliko makubwa waliyonayo Watanzania katika utendaji ndani ya Seriali, kasi katika uchumi na hasa kwa wanyonge. Akasema shida na matarajio ya Watanzania anayajua na anao uwezo wa kuyashughulikia.

Amani, usalama na umoja wa kitaifa ni msingi wa maendeleo ya kweli. Wizi, ubadhilifu, rushwa ameahidi kuvikomesha haraka. Ametoa mfano wa hospitali mgonjwa kuandikiwa cheti hospitalini na kuambiwa akanunue dawa kwenye duka jirani na akahoji hilo duka limepataje dawa na hospitali ikazikosa?

Amegusia elimu, mikopo ya wanafunzi, ajira kwa vijana, wakulima kupata miliki ya ardhi, pembejeo, mbegu za gharama nafuu, masoko ya uhakika na bei nzuri za mazao. Akasema wakulima kukopesha serikali hili halitatokea wakati wa serikali yake.

Umoja wa kitaifa, Muungano wa Tanzania, ulinzi na usalama wa nchi, kuhesimu mihili, kwamba Bunge litafanya kazi bila kuingiliwa na Mahakama hataiingilia. Pia kwamba ataunda mahakama ya mafisadi na majizi wafungwe haraka, ataimarisha utawala bora, uhuru wa kuabudu, ataheshimu mawazo ya vyama vingine yenye lengo la kujenga nchi yetu na atajenga viwanda vingi.

Sitanii, hayo na mengine mengi aliyosema ikiwamo ujenzi wa reli, barabara za juu, bandari na viwanja vya ndege yanafurahisha kuyasikia. Ninachosema sasa, baada ya Magufuli kutueleza hayo, anapaswa kuanza kutoa ufafanuzi jinsi gani atakavyotekeleza hizi ahadi zake. Akitoa ahadi hizo, amesema kuwa wakati wa serikali yake hakutakuwapo msamiati wa neno mchakato unaendelea. Najiuliza, na ningependa Magufuli afafanue atatumia mbinu zipi kudhibiti mfumo uliowakwamisha watangulizi wake.

Mfano mzuri ni Kikwete anayempokea kijiti. Aliahidi kujenga reli ya kisasa, lakini hadi anaondoka madarakani hili limebaki kuwa historia. Aliahidi kufufua shirika la ndege Tanzania, lakini hadi anaondoka madarakani imekuwa historia. Wakati wa kampeni napenda kusikia kutoka kwa Magufuli akifafanua atawezaje kujipambanua na Kikwete.

Magufuli amegusia nia yake ya kuhakikisha wafanyabiashara wakubwa wanalipa kodi. Nasubiri kwa hamu kusikia kauli yake hao wakubwa walioko karibu na vigogo wa serikali wasiolipa au wanaolipa kidogo na kuua biashara ya uagizaji mizigo nje ya nchi atawashughulikiaje?

Sina uhakika iwapo Magufuli anatambua kuwa kwa sasa wapo wapambe waliokwishaanza kutengeneza himaya. Wapo watu tayari wanaiaminisha jamii kuwa ni marafiki wakubwa wa Magufuli na wameanza hata kuwaahidi watu kazi. Ukienda pale CCM makao makuu utawaona. Wanaona nchi sasa iko mikononi mwao, je, Magufuli akifanikiwa kushinda ataendelea kuwakumbatia hawa?

Mwisho, Waswahili husema lisemwalo lipo kama halipo laja. Je, kwa Lowassa na Sumaye kuondoka wakilalamikia mfumo uliotumika katika uchaguzi ndani ya CCM, hivi naye anaamini hakuna cha kubadili mambo yanapaswa kwenda sawa na alivyokuwa anaendesha Kikwete? Kwa upande wa wapinzani, Magufuli tumemsikia. Tunasubiri sera zenu Agosti 29. Tufanye yote tufanyayo, kubwa tutambue Tanzania ndiko nyumbani. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri