Minara 292 ya mawasiliano iliyojengwa na Kampuni ya Simu ya Excellentcom Tanzania mwaka 2008, imetelekezwa bila kutoa huduma yoyote, JAMHURI linaripoti.
Baada ya kuitelekeza kwenye viwanja ambavyo baadhi vina makazi ya wamiliki wa ardhi hiyo, kumefanya kampuni hiyo sasa kudaiwa mamilioni ya shilingi ya kodi za pango la eneo.
Kampuni ya Excellentcom Tanzania Limited ilisajiliwa kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Septemba 13, 2006 ikiwa na wanahisa wawili — Jitco Limited ikiwa na hisa 3,500 na Excellentcom Systems hisa 6,500.


Mara baada ya kusajiliwa, kampuni hiyo ilianza mchakato wa kusimika minara yake ya mawasiliano mwaka 2008 kwa kuingia mikataba ya pango na wananchi wanaomiliki maeneo ambayo minara hiyo imejengwa, lakini imeshindwa kutimiza masharti ya mikataba hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika ambazo JAMHURI imezipata, Excellentcom kwa sasa imeshindwa kuiendeleza sambamba na kulipa kodi za pango kulingana na mikataba hiyo na kufunguliwa kesi za madai na wananchi hao.
Helena Mafita, mkazi wa Mtaa wa Litapwasi, Chang’ombe Uwanja wa Taifa, Temeke jijini Dar es Salaam anasema kwamba kwa sasa hakuna walinzi wanaolinda minara hiyo iliyojengewa mitambo pamoja na jenereta kubwa.


Nyumbani kwa Helena mitambo hiyo imefungwa kwenye pointi ya longitudo nyuzi 039.26935 latitudo nyuzi 06.85363 kiwanja namba 28 ambako aliingia mkataba wa kampuni hiyo kwa miaka 20 kuanzia Agosti 15, mwaka 2008.
Katika mkataba huo ambao Helena alikuwa analipwa Sh 300,000 kwa mwezi ungefika ukomo Agosti 14, 2028.
Helena anadai kuwa hajalipwa na kampuni hiyo tangu mwaka 2010 na kila anapofuatilia ofisi za Excellentcom, Mikocheni, hafanikiwi kuwaona wahusika baada ya kuelezwa kuwa “ofisi hiyo haipo kwa sasa hapo.”
Hali hiyo ilimfanya Helena aende kwa wanasheria ili kufuatilia haki (pango) yake kwa njia ya mkondo wa sheria ambako sasa amewakodi mawakili wa Kampuni ya CERW.


Katika barua hiyo ya Novemba 18, 2013 yenye Kumb. Na. CERW-ADV/HELENA/2013/01, mawakili hao waliandika, “Tumeelezwa na mteja wetu Helena Mafita, ulipojengwa mnara wa mawasiliano ya simu Dar 134 kwamba umechelewesha malipo ya kodi hadi Oktoba 19, 2010. Alikuwa anakudai limbikizo la Sh. 7,800,000 kwa mnara wa mawasiliano,” inasema sehemu ya barua ya mawakili hao iliyosainiwa na C.E.R. William, ambayo gazeti hili imeona nakala yake.
 Wakili William, anayemtetea Helena, anasema pia mteja wake aliamini kwamba angelipwa deni lake mara baada ya kampuni hiyo kumwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Jitco na Excellentcom, lakini deni lake halikulipwa na hakuna kinachoendelea hadi sasa.
Anasema kwa sasa deni hilo limeongezeka na kufikia zaidi ya Sh. 14 milioni ikijumuishwa na deni la nyuma na wanahisa hao hawajalipa na kuzidi kumletea usumbufu mdai huyo.


Wakili William anaeleza kusikitishwa kwake akisema kitendo hicho cha kutolipwa mteja wake na kuwaondoa walinzi bila kuwapa taarifa yoyote “si (kitendo) cha kiungwana kwa kuwa wameamua kukaa kimya na kukiuka makubaliano ya mkataba kama unavyosema.
“Mteja wetu ametuelekeza tukuandikie barua hii kuutaka uongozi wa kampuni umlipe malimbikizo yake kwa haraka na Sh. milioni 10 ikiwa ni gharama za usumbufu wa kimwili na kisaikolojia alioupata kwa mshtuko kwa kutokulipwa deni lake hadi sasa,” inasema sehemu ya barua hiyo.
Anasema, barua hiyo kwa uongozi wa kampuni hiyo ya simu, ilitoa notisi ya siku 30 tangu tarehe iliyoandikwa kulipa deni hilo kwa mteja wao, sambamba na gharama za usumbufu na kwamba iwapo watakaidi kufanya hivyo wameelekezwa kufungua madai dhidi ya wahusika na matokeo yake hakuna utekelezaji wowote.
Mbali ya Helena, mtu mwingine aliyeilalamikia Kampuni ya Excellentcom ni Stephen Mafuru ambaye amefungiwa mitambo hiyo ya mawasiliano nyumbani kwake kiwanja Na. 5 kilichopo mtaa wa Maili Sita, Wilayani Hai mkoani Kilimanjaro. Mtambo huo umefungwa Longitudo nyuzi 37.27111 na Latitudo nyuzi 03.32786.
Katika mnara huo uliojengwa kwenye ukumbi wa mita 15 za mraba, Mafuru anasema kwamba mara ya mwisho kulipwa fedha ilikuwa ni 2011 kiasi cha Sh milioni 4.8


Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura, alipoulizwa kama anafahamu taarifa za Kampuni ya Excellentcom iliyotelekeza mitambo yake na kushindwa kulipa kodi ya pango kwa wateja walioingia nayo mikataba, anasema wao hawahusiki na minara ya kampuni nyingine na kwamba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wanaweza kuwa na majibu sahihi.


Naye Meneja wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Innocent Mungy, alipolizwa na JAMHURI kuhusu Kampuni ya Simu ya Excellentcom anasema walitoa matangazo muda mrefu kwamba hawana leseni kutoka Mamlaka hiyo.
Anasema suala la kujenga miundombinu ya kampuni za simu katika maeneo mbalimbali liko chini ya halmashauri za miji au majiji inapojengwa minara hiyo, kulingana na utafiti wa kitaalamu wa kampuni husika.

 

By Jamhuri