Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amezungumza maneno mazito ambayo kwa yeyote anayeitakia heri nchi yetu yamemgusa.

Maneno aliyoyasema yanaweza yasiwafurahishe wengi, hasa ndani ya chama chake, lakini huo ndio ukweli wenyewe.

Ameonya juu ya mmomonyoko wa haki miongoni mwa wananchi na vyombo vya utoaji haki, na kuonya kuwa mataifa kama Sudan ambayo utawala wake umeangushwa yamekumbwa na hali hiyo kwa sababu ya kupuuza haki kwa wananchi wake.

Tunaungana na Dk. Bashiru kwenye kauli hii. Ukweli ni kuwa amani ni matokeo ya haki. Jamii yoyote isiyo na haki haiwezi kuwa na amani.

Vyombo vya habari, likiwamo Gazeti la JAMHURI, vimekuwa vikiripoti habari nyingi na nzito za malalamiko ya watu wasiotendewa haki. Hawa ni wale wanaodhulumiwa na wengine ni wale walio magerezani au mahabusu kwa kubambikiwa kesi.

Mathalani, tuna taarifa za Ecobank kutiwa hatiani kwa kumwibia mteja wake Sh milioni 66 kutoka kwenye akaunti yake. Licha ya mahakama kuitia hatiani benki hiyo, mwananchi huyo mnyonge ameendelea kunyimwa haki. Kuna taarifa kuwa Polisi, Ofisi ya DPP kwa kushirikiana na watumishi wa benki waliomuibia mteja huyo wameungana kuhakikisha hawashtakiwi. Kesi imekaliwa.

Mifano ya aina hii ni mingi mno. Watu maskini wanapata shida sana mbele ya vyombo vya utoaji haki.

Wapo viongozi wengi wanaotumia madaraka yao kuwakomoa wenzao kwa kuwabambikia makosa ya uongo na kuhakikisha wanateseka. Wanasahau au kupuuza ukweli kuwa uonevu wa aina hii unajenga chuki ambayo matokeo yake yanaweza yasionekane leo, lakini mwishowe yakawa janga kwa jamii.

Ripoti ya CAG inadhihirisha wazi uonevu unaofanywa na mamlaka mbalimbali kukwapua mabilioni ya fedha za miradi mbalimbali. Hii ni dhuluma ambayo matokeo yake yanawafanya wananchi waichukie serikali yao kwa kutowapelekea maendeleo.

Kauli ya Dk. Bashiru ni ya msingi kwa sababu suala la haki si la hiari, bali ni hitaji la msingi la ujenzi na uimarishaji amani nchini mwetu.

Tungependa viongozi wengi wawe wakweli kama yeye ili hatimaye mamlaka zote zinazohusika kwenye utoaji haki ziweze kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.

3119 Total Views 7 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!